21 February 2011

Pinda ataka mawakili kupunguza gharama

Na Omari Moyo, Arusha

MAWAKILI nchini wametakiwa kuangalia upya gharama zao za kutoa ushauri wa kisheria na kuendesha kesi, ili Mtanzania mwenye kipato kidogo aweze
kuzimudu gharama hizo wakati akitafuta msaada huo kutoka kwa kwao.

Akisoma hotuba ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda juzi wakati wa  kufunga mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Waziri wa Sheria na Katiba, Bi. Celina Kombani alisema kuwa Watanzania wengi hawana fursa ya kupata haki zao mapema ama kwa wakati kutokana na kukosa ushauri wa kisheria.

Alisema kuwa Watanzania walio wengi wangependa kupata ushauri wa kisheria kutoka kwenu kuhusiana na masuala mbalimbali ya kisheria, kama vile kucheleweshewa mirathi, matunzo ya watoto na mengineyo mengi lakini kutokana na uwezo wao mdogo hushindwa kumudu gharama zenu na hivyo kupelekea kukosa haki zao ama kucheleweshewa.

“Wananchi wengi wa Tanzania, hasa wale wenye vipato vidogo na wanaoishi vijijini wanapata tabu kubwa saana, wanapotafuta haki zao..na hilo linachangiwa pia na nyie mawakili kutoza gharama  kubwa kwa kutoa ushauri wa kisheria kwa mtu kupata haki yake mliangalie hili kama changamoto kwenu,” alisema Waziri Mkuu.

Aliongeza “Sisi wanasiasa tunayaona haya kila siku, pindi akina mama, wajane, wazee kwa vijana wanapokuja kulalamika kudhulumiwa au kucheleweshewa haki zao za mirathi, matunzo ya watoto na nyinginezo nyingi na utaona haswa wanahitaji ushauri wa kisheria ambao wengi hawamudu,” alisema Waziri Mkuu.

Hata hivyo Waziri Mkuu alisema kuwa serikali inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na mawakili katika kuhakikisha kuwa hata mnyonge anaweza kufika kwenye vyombo vya kutatua migogoro zikiwemo mahakama.

Mkutano huo wa mawakili ambao ulikuwa na ajenda kuu moja katika mkutano wa mwaka huu ambayo ilikuwa ni suala la katiba mpya nchini, alisema chama hicho cha mawakili ni waledi na hivyo lazima kiwe mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa mawakili wanatoa ushauri na michango yao muhimu katika kufanikisha azma ya katiba mpya nchini.

“Pia katika hili serikali inaandaa Muswada wa Sheria wa Mchakato  wa Kuandaa Katiba Mpya, ambao unatarajiwa kufikishwa bungeni Aprili mwaka huu kwa majadiliano na kuwa mwanzo mzuri kuelekea katiba mpya,” alisema Pinda.

Alisema kuwa Chama cha Mawakili Tanzania Bara (TLS), ama kupitia wanachama wake mmoja mmoja, kiendelee bila kuchoka kutoa ushirikiano ili kuwe na katiba bora zaidi yenye kuzingatia umoja wa kitaifa, amani na mshikamano baina ya Watanzania, na yenye kusimamia haki bila ubaguzi wowote.

Rais wa TLS aliyemaliza muda wake, Bw. Felix Kibodya akizungumzia alisema chama hicho kitashirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo serikali kuhusiana na suala la katiba hiyo.

Mkutano huo wa mwaka wa chama cha Mawakili Tanzania Bara (TLS), umekutanisha wataalam mbalimbali wa sheria wa ndani na nje ya nchi wanaofikia 1,000 na kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya uundwaji wa katiba.

No comments:

Post a Comment