17 February 2011

Ni Maafa

*Mabomu JWTZ yatikisa Gongo la mboto
*Mamia wahofiwa kupoteza maisha

John Mapinduzi na Rose Olotu

MAELFU ya wakazi wa eneo la Gongo la mboto  na vitongoji jirani jijini Dar es salaam, jana walilazimika kuyakimbia makazi yao baada ya kutokea
milipuko mikubwa ya mabomu kwenye kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) iliyopo eneo hilo.
Milipuko hiyo ilianza saa mbili usiku na kusababisha anga lote la eneo hilo kutapakaa moto uliosababishwa na mabomu huku wakazi hao wakihaha kukimbia huku na kule kuponya maisha yao.
Tukio hili ni la pili kutokea ndani ya kipindi cha miaka miwili ambapo  Aprili, 2009 watu zaidi ya 20 walipoteza maisha kufuatia  kutokea mlipuko katika ghala la kuhifadhia mabomu  la JWTZ kambi ya Mbagala jijini Dar es Salaam.
Mlipuko huo ulisababisha uharibifu mkubwa wa mali. Nyumba nyingi zilivunjwa na mamia kubaki bila makazi jambo lililosababisha serikali kulipa fidia ya mamilioni ya fedha wananchi hao.
Tukio la jana lilitikisa jiji lote la Dar es salaam na vishindo vya mabomu kutetemesha maeneo mengi huku waliokuwa mbali na eneo hilo, wakishuhudia anga la eneo hilo, likiwiva mithili ya mawio ya jua.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi alikaririwa akisema mkasa huo ulitokana na mlipuko katika ghala namba tano la kuhifadhia mabomu kambini hapo.
Naye Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo aliwataka wakazi wa eneo hilo kuondoka haraka na kwenda kwenye maeneo ya mabondeni ili kujisalimisha.
Wakati hayo yakiendelea wanajeshi walikuwa wakihangaika kujaribu kuzuia moto huo usihamie kwenye maghala mengine.
Mamia kwa maelfu ya wakazi wa maeneo hayo walikimbia huku wengine wakisahau kufunga milango ya nyumba zao,  wanawake wakibeba watoto migongoni na kuburuza wengine waliokuwa na umri wa kuweza kutembea.
Eneo la barabara ya Nyerere kuanzia njiapanda ya Jet Club, (iliyokuwa Kipawa) hadi TAZARA, lilifurika maelfu ya watu waliojawa hofu na kupoteza matumaini kutokana na tukio hilo baya la kutisha na kusikitisha.
Eneo la TAZARA mkabala na kiwanda cha Azam, liligeuka kambi kubwa ya ÔwakimbiziÕ waliokuwa wakiponya maisha yao, huku wengine wakitembea kwa miguu kufuata barabara ya Mandela kuelekea Ubungo na kituo cha Polisi Buguruni, kikifurika wanawake na watoto. 
Misururu ya magari ya wagonjwa na yale ya watu binafsi, ilijaa  barabarani kama inavyokuwa saa za mchana watu wanapokwenda au kurudi kazini, huku hospitali  za Amana, Kisarawe na Muhimbili, zikipokea mamia ya majeruhi na watu waliokufa.
Polisi walilazimika kufunga barabara ya Nyerere eneo la Uwanja wa ndege mara baada ya milipuko hiyo kupamba moto na  kuwalazimisha abiria wote waliokuwa wakitokea maeneo ya mjini, kutoingia eneo hilo hatari.
Maeneo jirani ya Majohe, Ukonga, Kitunda, Uwanja wa Ndege  Yombo Vituka, Lumo, Kipunguni, Pugu, Kazimzumbwi yalijaa misururu ya watu waliokuwa wakikimbia makazi yao huku wengine wakibeba mabegi na ndoo.
Wakazi hao walikimbilia maeneo mbalimbali ya jiji  na wengine wakienda nje ya mji Kisarawe, Mwanagati  na Chamazi. Karibu usiku kucha wa kuamkia leo, mamia ya watu wasiokuwa na ndugu maeneo mengine, walikesha nje.
 Hata hivyo serikali ya mkoa wa Dar es Salaam ilitangaza kuwapa hifadhi waathirika hao kwenye Uwanja wa Uhuru, maarufu kama Shamba la Bibi.
Hadi tunakwenda mitamboni idadi kamili ya vifo na majeruhi, ilikuwa haijapatikana lakini kulikuwa na taarifa mchanganyiko huku mmoja wa watu waliokimbia eneo hilo, akiliambia Majira kuwa alishuhudia zaidi ya watu 10wakiwa wamekufa jirani na nyumba yake.
Hata hivyo Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam  Bw. Mecky Sadick  alikaririwa na kituo kimoja cha redio, akisema kwa mujibu wa Jeshi la Polisi,  mtu mmoja aliripotiwa kupoteza maisha na wengine 40 kujeruhiwa.

        Eneo la tukio
Mkazi mmoja wa Gongolamboto, Bw. Zuber Mohamed alilimbia gazeti hili kuwa hali katika eneo hilo ni mbaya familia yake imesambatika huku mwanawe mmoja akiwa ameumia. 
ÒHali ni mbaya mwanangu  ameumia, familia zimetawanyika hatujui ziko wapi na kuna taarifa za bomu moja kuangukia  Chuo Ualimu Rada,Ó alisema Bw. Mohamed na kuongeza;
ÒHapa nipo hoi sana, natokea Msongola nilikokimbilia  ingawa tumesikia taarifa kuwa tusirudi, lakini huko tulikokuwa hatujapata msaada wowote wa hifadhi sasa tufanyeje?
ÒNimechukua watoto watatu ambao namjua baba yao anaitwa Burhan Said, pia Tumeokota kichanga wa siku tatu mwingine mtoto wa mwaka mmoja. Vile vile kuna mama, mjamzito kajifungulia porini katika harakati za kukimbia, karibu na maeneo ya Mbande, hatujui hali yake itakuwaje.Ó 
Bw. Mohamed, alisema alikimbia bila kufunga mlango wa nyumba yake huku mama mmoja jirani yake akikimbia na khanga moja kutoka bafuni alikokuwa anaoga.
Alisema jirani yake mwingine aliyemtaja kama  Mama Yasin amepotelewa na wanawe watatu huku mama mwingine aliyemtaja kwa jina la Salma Hamza na mwanawe Saad, hawajulikani waliko.
ÒKwa ujumla hali ni mbaya sana na kuna uharibifu mkubwa wa majengo,Ó alisisitiza
Katika eneo hilo viungo mbalimbali vya binadamu ikiwemo mikono na moyo viliendelea kuokotwa usiku wa kuamkia leo.
          Hali hospitali ya Amana
Majira lilipofika katika hospitali ya Amana lilikuta vilio vimetawala huku magari ya wagonjwa yakipishana kuleta majeruhi na vipande vya miili ya watu iliyookotwa huku mengine yakipeleka majeruhi waliozidiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Mganga mmoja wa hospitali hapo aliyeomba kutoandikwa jina gazetini, alisema hajawahi kuona tukio la kutisha kama hilo kwani maiti na majeruhi waliofikishwa ni wengi na inasikitisha.
ÒJamani ukweli ni kwamba sijawahi kuona tukio la kutisha kama hili, maiti na majeruhi wanaoletwa hapa ni wengi na wanatisha ingawa siwezi kujua kwa haraka idadi yao. Usinitaje jina mimi si msemaji hatutakiwi kusema lolote,Ó alisema mganga huyo.
Hospitali hiyo ilionekana kuzidiwa majeruhi, huku waliopoteza fahamu wakiwa wamelala kwenye viambaza. Baadhi ya wanawake walichanganyikiwa na kulia kwa sauti wakihoji waliko watoto na waume zao.
Mwanaume mmoja alilazimika kuwakunjia ngumi polisi waliokuwa wakijaribu kumzuia asiingie ndani kumtafuta mkewe ambaye hakujua yu hai au amekufa kutika tukio hilo. Baada ya tafrani hiyo, walimruhusu kuingia.
    Kilio cha wahanga
Mwandishi wetu aliyefika eneo la TAZARA alikutana na  malalamiko ya wahanga hao hususan wanawake walioeleza kusikitishwa na kitendo cha polisi kushindwa kuwapa ulinzi eneo hilo.
ÒAngalia watu wote hawa tumekaa hapa lakini hakuna hata polisi mmoja sijui wanataka tutoe pesa ndio waje au vipi!Ó alilalamika mama mmoja aliyekataa kutaja jina lake.
Mhanga mwingine alijitaja kwa jina moja la Ismael, alimwomba Rais Kikwete kuwawajibisha mara moja  Waziri wa Ulinzi, Dkt. Mwinyi na Mkuu wa Majeshi, Jenerali  Davis Mwamunyange.
ÒHawa viongozi kwanza hawana sababu kusubiri Rais awawajibishe, walipaswa kesho(leo)asubuhi saa mbili wawe wametangaza kujizulu wao wenyewe. Mambo haya yalipotokea Mbagala, Dkt. Mwinyi alisema baada ya Ripoti ya Tume angejiuzulu, tukaona yuko kimya hadi leo.
ÒSasa tunamwambia Rais Kikwete awawajibishe hawa, kosa si kosa lakini kosa ni kurudia kosa, huu ni uzembe yalitokea haya haya Mbagala tukanyamaza tu lakini kwa hili hapana , hawa lazima waondoke ni uzembe wa kutisha huu, wasisubiri, Tume ya kazi gani wakatu uzembe wa moja kwa moja unaonekana hapa! ...Ó alilalamika mwathirika huyo akiwa ameshika wanawawe wawili eneo la TAZARA, kando ya barabara ya Nyerere.Ó
Kufungwa Uwanja wa Ndege
 Majira  lilipofika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere  (JNIA) lilikuta hali ni tete huku ndege zilizotakiwa kuruka zikiwa zimezuiwa na nyingine zikiambiwa kutafuta viwanja vingine vya kutua.
Hata hivyo haikuwa rahisi kubaini mara moja kama kulikuwa na uharibifu wowote ndani ya uwanja huo uliotokana na milipuko hiyo.







  









  

5 comments:

  1. eng mwakapango,E.P.AFebruary 17, 2011 at 6:04 PM

    watanzania sasa tumekuwa wapole mno. Naomba kwanza niwape pole watanzania wote na hasa wahanga wa tukio hili. ndugu yangu Dr. Hussein Mwinyi alipokuwa anatolea ufafanuzi mlipuko wa mbagala alisema wamejifunza tukio hilo halitatokea tena. ilikuwa ni kauli ya kisiasa mno kwani Dr hussein Mwinyi hana ABC za kijeshi na sidhani kama alipata tena kutembelea maghala ya silaha katika kambi yoyote ya kijeshi Tanzania tokea kipindi hicho cha huzuni kwa watanzania na naamini hajui Taifa hili lina kasma ya silaha kiasi au ikoje na madhara yake. nasema hivyo kwa sababu huyu bwana alitoroka hata jeshi la kujenga taifa 1988 akakimbilia ugiriki kufanya udaktari. sasa mtu ambaye hana interest hata ya jeshi la kujenga taifa tunampa wizara ya ulinzi mnadhani ataperform? awamu ya kwanza waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga taifa alitokana askari hao hao ninawakumbuka mawaziri kama Major General Abdalla Twalipo turudishe mfumo ule kondokana nadhana ya kuwa na unproffession soldiers ndani ya jeshi la ulinzi ili watoe ushrikiano wa moja kwa moja kwa MKUU WA MAJESHI. Katika hali ya kawaida Dr Hussein mwinyi atamwambia nini Gen.Davis Mwamnyange? mimi namshauri Dr Hussein Mwinyi awajibike ili kuonyesha mfano wa utawala bora. mkuu wa kikosi cha Gongolamboto afikishwe kwenye court mashal na maofisa wengine kwani hatuwezi kusikiliza excuse kwenye damu za watanzania. vilevile suala hili si la kuficha tunaomba kupata idadi ya kweli ya watu waliokufa na majeruhi. wabunge gomeni kula mpaka Dr mwinyi aweke daruga pembeni. Dr JK aibu hii utaficha wapi uso wa serikali yako.

    ReplyDelete
  2. LAA Nashindwa hata kuhema napata taabu sana juu ya Jeshi lawananchi wa Tanzania (JWTZ) kashfa hii wataficha wapi nyuso zao? Hapa inaomyesha wazi jeshi halina wataalamu wawajibikaji lina wanasiasa tu waliojawa uroho wa kutawala kisiasa kama hao akina bw. Shimbo. Hii ni mara ya pili sasa mauaji ya kutisha yanatokea mwanzo walisema wamejufunza na hali hiyo haitatokea tena. sitaki kuendlea nimejawa na hasira huu ni mtihani wa pekee kwa Rais na mkuu wake wa Majeshi. Mwinyi msimlaumu anapaswa alaumiwe kama kuna mgonjwa aliyekufa kutokana na kukosa huduma maana ndiyo taaluma yake. Hapa wa kulaumiwa ni Kikwete na Mwamunyange marafiki hawa wawili wanalo jambo. Jeshi gani lina-perform unprofessional? POLENI WATANZANIA MAANDAMANO YA MISRI SASA YAMEWADIA HAPA TZ WATU HATUTAVUMILIA KUFA BILA HATIA KUTOKANA NA UZEMBE WA JESHI AU MMTUMWA NINI?

    ReplyDelete
  3. NAPATA KIGUGUMIZI KUSEMA HUU SI MPANGO WA RAIS NA MKUU WA JESHI LAKE, KWANI KWAKUTAMKO LA RAIS KUJISIFU KUWA HAKUNA ASKALI ALIYE KUFA NIWAZI WALIJUA NA WAKAJIAHAMI MAPEMA. KIKWETE KWAKUWA WALIOKUFA KWAKO SI KITU SASA WATANZANIA WENZANGU TUFUMBUE MACHO NA TUANZE KWA VITENDO KUAAJIBISHA SERIKALI INAYO TUMALIZA. HIZI ZOTE NI SIASA TU KWA KIWETE, WATANZANIA MNATEGEMEA NINI RAIS KUWEKA UONGOZI KIRAFIKI, NINI KIFANYIKE KAMA SI KUUWA WATU TENA KWA KUKUSUDIA, WATANZANIA TUANGOJA NINI? KWANI MISRI SIYO NNCHI? ASKALI WAMEUWA RAIA ARUSHA SERIKALI HAIKUSIKITIKA, MABOM YALILIPUKA MABGALA SERIKALI HAIKUCHUKUA TAHADHALI, LEO MABOM YAMELIPUKA CAHKWANZA KUTANGAZIA UMAA NI KUWA HAKUNA ASKALIAALIYE KUFA NA KUSEMA JENGO LA JESHI NA BAADHI YA NYUMBA ZIMEBOMOKA KAMA ALIVYOSEMA PINDA,KIWTE NA PINDA KWAO ASKALINA JENGO LA JESHO KUTOBOMOKA NDIYO KITU CHA KUUMIZA. RAIA WALIOKUFA KWAO NI SAWA NA HAKUNA. MNATUONYESHA MIOYO YENU ILIVYO JAA USALITI KWA WATANZANIA. MMMEKUWA KAMA MMILIKI WA GALI ASIYE MTHAMINI DREVE WANI GARI LIKIPINDUKA CHAKWANZA KUULIZA NI JA GALI NI ZIMA? LINWEZA KUTENGENEZEKA KWA KIASI GANI? AKIPATA MAJIBU NDIPO ATASEMA NA DREVE NA UTINGO WAKE JE? KIKWETE, PINDA, NA MAOFISA USALAMA MJIHUZURU MSISUBIRI TUJIPANGE. WATANZANIA TACHE UPOLE TUTAZIDI KUUWAWA NA SERIKALI HII. POLENI SANA WENZANGU WATANZANIA.

    ReplyDelete
  4. kwani watanzania mnaogopa kuandamana? mnauwawa bila sababu si bora mfe kwenye maandamano kwa faida ya kizazi chenu cha baadae. hamuoni kama mnatawaliwa na group ya mafia wacha mfe mnajifanya wajinga sana.

    ReplyDelete
  5. Tena tufe kweli! Misri na Tunisia wao hwakuwa na mjadala tena baada ya kuuchoka utawaka dhalimu. Ukondoo wetu jamani utatumaliza! Hivi tutawaambia watoto na vizazi vyetu kwamba tuliogopa kuuondoa utawala usiotufaa, watatuelewa kweli? Tunasubiri hadi tumalizike hadi mtu wa mwisho ndiyo tuwaondoa wauwaji hawa kwenye uongozi? LA HASHA, SAA YA UKOMBOZI NI SASA!!!!!

    ReplyDelete