17 February 2011

Mgawo wa umeme wadaiwa ni hujuma

*Yadaiwa lengo kushawishi kuwasha Dowans
*Bosi wa TANESCO akiri kusikia, akanusha


Na Waandishi Wetu

WAKATI mgawo wa umeme ukizidi kulitikisa taifa habari za hivi
karibuni zimesema kuwa ni hujuma iliyoandaaliwa kitalaamu ili kuweka mazingira ya kununua au kukodi mitambo ya Dowans kwa kisingizio cha kuinusuru nchi.

Tayari hatua hiyo ya kuwasha mitambo ya Dowans imeelezwa kuwa inaweza kuliingiza taifa katika matatizo makubwa.Habari za uchunguzi ambazo limelifikia Majira zimesema kuwa mbali na matatizo ya maji yaliyoanza kujitokeza siku za karibuni, mgawo wa umeme ulianza muda mrefu ukihusishwa na kuharibika kwa mitambo kadhaa ya kufua umeme, jambo ambalo limetajwa na chanzo chetu kuwa ni sehemu ya mkakati huo.

Ingawa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Bw. William Mhando alikanusha kuwapo kwa mpango huo, alikiri kuwapo kwa madai hayo akisema yameshafanyiwa uchunguzi na kubaini kuwa hayana ukweli kwa kuwa mgawo huo hautokani na hujuma.

Mmoja wa wabunge waliozungumza na Majira ambaye hakutaka kutajwa gazetini, amesema anazo taarifa kuwa sh milioni 500 zimetengwa na kuwalipa baadhi mafundi wa shirika la umeme TANESCO kuhujumu mitambo ya shirika hilo ili tatizo la umeme lionekane kubwa na kushawishi umma katika matumizi ya mitambo hiyo.

Mtoa habari wetu alisema kuna kituo kimojawapo jijini Dar es Salaam mafundi wa TANESCO walilazimishwa na bosi wao kuingiza umeme mkubwa zaidi ya uwezo wake, na walipofanya hivyo ukalipuka.

"Wamepewa tip ya milioni 500/-, linapokwisha tatizo hili linajitokeza jingine, lengo ni kushinikiza Watanzania waone kuna tatizo, ili serikali iruhusu mtambo wa Dowans kuzalisha," alisema.

Akifafanua suala hilo, Bw. Mhando alisema madai hayo yalijitokeza kwenye kituo kidogo cha Kipawa ambacho kina uwezo wa kuzalisha kv 132, na ndio umeme ulioingia na si zaidi ya hapo.

"Kama ungeingia umeme unaofikia kv 400 hapo tungesema sawa kuna hujuma," alisema. Bw. Mhando na kufafanua kuwa uchunguzi wa tuhuma hizo ulifanywa na mafundi wa ndani na nje ya nchi.

Taarifa hizo zimejitokeza wakati mitambo ya Dowans imeanza kupigiwa chapuo na baadhi ya wanasiasa akiwamo Mwenyekiti mpya wa Kamati ya Nishati na Madini, Bw. Januari Makamba, kuwa iwashwe kwa mkataba maalumu wa miezi mitatu ili kuinusuru nchi ambayo inaelekea kuwa gizani.

Tayari kauli hiyo ya Bw. Makamba iliyokaririwa juzi kwenye Kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na TBC1, imeelezwa inaweza kuliingiza taifa katika majanga mengine makubwa.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino, Profesa Mwesiga Beregu kauli zilizotolewa na baadhi ya viongozi kutaka mitambo ya Dowans iwashwe ili kunusuru tatizo la umeme nchini ni hatari kwa taifa na zitakuwa hatua za zimamoto ambazo hazitasaidia nchi kuondokana na tatizo.

"Hizi ni hatua za zimamoto. Tunatoka katika janga hilo na tunaingia katika janga jingine bila ya kufikiria. Ni lazima watu watambue kwamba kuna sheria za kimataifa zimetawala kwenye hiyo Dowans, wasikurupuke," alisisitiza.

Alisema kama watu hawatafikiria kwa makini na kisha kulazimisha mitambo hiyo ya Dowans iwashwe, Tanzania itaingia katika matatizo mengine mapya, ambapo alisisitiza kwamba kabla ya maamuzi wafikirie kwanza wasije wakaingiza nchi katika majanga hayo.

Prof. Beregu alisema kuwa tatizo la serikali bado inajikanyaga, haijajiandaa kuweka mikakati ya muda mirefu bali wanayozungumzwa ni zimamoto.

"Tatizo ni kwamba hakuna mikakati madhubuti ya kuzalisha umeme nchini, eneo hili limegubikwa na ufisadi wa namna fulani, ndio maana tumefikia hapa tulipo sasa na ndio maana yote yanayoongelewa ni kama zima moto," alisema.

Alisema kuwa maamuzi Tanzania yamekuwa ya ovyo onyo, hakuna changamoto ya kufikiri na matokeo yake miaka mitano imepita lakini hakuna kitu ambacho Watanzania wanaweza kusherehekea.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Bi. Ananilea Nkya aliitaka serikali kuwaeleza kwa kina wananchi kwa nini Taifa limefikia hapa lilipo sasa.

Bi. Nkya alisema kuwa tatizo kubwa la viongozi walioko madarakani wamekuwa wakidharau wananchi na ndio maana nchi inakwenda shaghalabaghala.

"Taifa lilipofikia sasa ni hatari serikali ieleze wananchi ni kwa nini imewafikisha katika hali hii ngumu ni kwa nini wanadharau wananchi, wamekaa kimya bila ya kutoa maamuzi yoyote kuhusu umeme wanafikiria nini,"alihoji.

"Wananchi wanahitaji umeme, sasa angalia Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) limesema viwanda 50 kati ya 280 huenda vikafungwa na vingine kupunguza uzalishaji endapo makali ya mgawo wa umeme yataendelea hadi mwezi ujao, serikali inafikiria nini," alihoji.

Katika kipindi cha Jambo Tanzania cha TBC1, ambacho kilikuwa kikijadili hali ya umeme nchini juzi, Bw. Makamba alisema ni ujinga kuruhusu gridi ya Taifa izimike huku kukiwa na mtambo wa Dowans uliozimwa.

"Hatuwezi kuwa katika dharura huku kuna mtambo umezimwa kwa sababu ya kisiasa...tutumie hata sheria za kuhujumu uchumi mitambo iwashwe

"Wote tutaonekana hatuna akili wakati tukokosa umeme huku kuna mtambo wa Dowans ambao una uwezo wa kuzalisha megawati 120. Uwashwe hata kama ni kwa mkataba wa siku 90," alisema.

Akichangia hoja hiyo, mbunge mmoja wa CCM ambaye hakupenda kutajwa jina lake kutokana na ugumu wa suala hilo anavyoliona alisema anaweza kuzungumzia jambo lingine lolote atakaloulizwa lakini si
kuzungumzia masuala ya umeme na Dowans.

“Unaweza kuzungumza lolote na mimi lakini hili la mitambo ya Dowans naomba nisichangie kwa sababu miongoni mwetu wabunge wa CCM wapo wenye maslahi yao, hivyo unaweza kutoa maoni ukawa katika hali mbaya,” alisema.

Waziri wa zamani wa Ujenzi, Bw. Nalaila Kiula alisema kuwasha mitambo ya Dowans ni kujivuruga wenyewe na kutengeza mazingira ya kuonesha kwamba mkataba ulivyunjwa kimakosa.

Mkataba ulivyunjwa kwa sababu za msingi, serikali ikijiingiza katika kutatua matatizo ya umeme kwa faida ya muda mfupi itakuja kusumbua baadaye ni bora mitambo hiyo isiwashwe.

Alisema mvua ziko karibuni kunyesha, maji yatajaa katika mabwawa yetu umeme utapatikana na pia alirejea hoja la aliyekuwa Waziri Mkuu, Bw. Edward Lowassa kuwa kama hilo linaonekana litachelewa ni vyema wakakodi wataalamu wa kutengeza mvua wafanye hivyo ili kujaza mabwawa kwa muda hadi masika.

“Dowans tuna matatizo nao alafu unataka kuwasha mitambo yao, tutakuwa tunafuta makosa na kuonesha tulikosea kuvunja nao mkataba, mambo haya yanaweza yakawa ya kisiasa, tuzingatie maadili tusikubali kutumika,” alisema.

Bw. Kiula alisisitiza kwamba mitambo hiyo isiwashwe kwani TANESCO ndio wanaohusika na masuala ya umeme nchi nzima, bado hawajatoa wazo la kuwasha mitambo hiyo ya watu wenye utata.

Alisisitiza kwamba wazo hilo linawezekana kuwa la kisiasa ili kuwanusuru waliojiingiza na kuleta kampuni hizi ili Dowans ionekane kuwa ni halali kwa kuwa walirithishwa na Kampuni ya Richmond.

Mbunge wa Ukonga (CCM), Bi. Eugen Mwaiposa akizungumzia hilo alisema anaunga mkono hoja ya kuwasha mitambo ya Dowans kwa sababu mahitaji yaliyopo ni kupata umeme.

Alisema kukosekana kwa umeme kunaathiri sana wafanyabiashara ndogondogo hivyo kama kuna uwezekano wa kuwasha hizo mashine ziwashwe ili kuondokana na kiza.

“Sijajua Serikali itaingia gharama kiasi gani katika kuwasha mitambo hiyo lakini naunga mkono iwashwe,” alisema.

Wakati huo huo, Mbunge wa Jimbo la Ubungo (CHADEMA), Bw. John Mnyika amekanusha taarifa zilizomkariri akishauri kampuni ya Dowans ipewe mkataba wa miezi mitatu.

Bw. Mnyika alisema kuwa gazeti moja (sio majira) lilimnukuu vibaya, likidai alitoa kauli hiyo wakati akizungumza katika mahojiano katika Kipindi cha Jambo cha TBC1.

"Napenda watanzania wenzangu wakumbuke kwamba kipindi hicho kilirushwa moja kwa moja, na katika kipindi husika hakuna kauli yoyote niliyoitoa ya kutaka mitambo ya Dowans iwashwe kwa mkataba wa miezi mitatu, badala yake niliitaka serikali itumie sheria hususani ya uhujumu uchumi kuiwasha mitambo husika kwa maslahi ya taifa," alisema.

Sambamba na hilo alisema atatoa tamko la kina hivi karibuni kutokana na nafasi yake ya uwaziri kivuli kuhusu suala la umeme kwa kuzingatia hali ya maisha ilivyo nchini.
 
Bw. Mnyika alisema kwa mtazamo wake ni muhimu ili kupunguza adha ya mgawo wa umeme, serikali itumie mamlaka yaliyopo kwenye katiba na sheria ikiwemo sheria ya uhujumu uchumi, sheria ya kupambana na rushwa, sheria ya mali zilizopatikana isivyo halali na sheria nyinginezo, itaifishe mitambo hiyo haraka iwezekanavyo na kuiwasha kwa maslahi ya umma.

"Ikumbukwe kwamba kampuni ya Dowans ilirithi mkataba kutoka kampuni ya Richmond ambayo ilithibitishwa kwa maazimio ya bunge kuwa ilipata mkataba katika mazingira ya ukiukwaji wa sheria ikiwemo sheria ya kupambana na rushwa, na pia kampuni hiyo ina utata kuhusu usajili, umiliki na uhamasishaji wa mkataba wake kama suala zima likitazamwa kwa undani wake yakirejewa yaliyojiri Costa Rica na Tanzania," alisema Bw. Mnyika.

Alisema wakati mjadala kuhusu MW 120 za Dowans ukiendelea na kwa kuwa kiasi hicho hakiwezi kuziba pengo la takribani MW 240 ambalo linakabili taifa hivi sasa, ni muhimu kwa Waziri wa Nishati na Madini kutoa maelezo ya kina kuhusu hatua ambayo serikali inataka kuchukua ya kukodi mitambo ya MW 260.

"Waziri atoe ufafanuzi wa kutokukamilika kwa mipango ya serikali wakati ambapo dharura ya umeme ilijulikana tangu mwaka 2002, serikali ikaijadili kwa kina mwaka 2006, bunge likapitisha maazimio mwaka 2008 na serikali ikaahidi tena mwaka 2009 kuweka utaratibu wa kukabiliana na dharura hiyo.

"Katika muktadha huo ni muhimu kwa bunge kupata fursa ya kujadili kwa kina suala la umeme katika mkutano unaoendelea wa bunge kama jambo la dharura ili kuweza kulinusuru taifa," aliongeza.

21 comments:

  1. Januari Makamba ni mtoto wa Fisadi. Hapa kilichobakia ni kumwondoa joka pangoni kwakwe kama walivyofanya Misri.

    ReplyDelete
  2. Mmeanza kumsuta January na kumpamba Mnyika,waswahili kwa unafiki mmehitimu!Sote tulisikia alichosema Mnyika,hakika aliunga mkono mitambo ya Dowans kuwashwa,kipi kimemfanya leo asahihishe kauli yake?Unafiki tu wa kisiasa!Na huyo Profesa Baregu naye aongee kama msomi,haitoshi tu kusema kuwasha mitambo ya Dowans kutaingiza nchi katika matatizo mengine...YAPI HAYO,kama anayajua si ayaseme?Anataka nani afikiri badala yake?Naye huyu Mama Nkya ajifunze kunyamaza!

    ReplyDelete
  3. Hilo sipingani nalo huyu na wabunge wake wa ccm hawana jipya kwani DOWANS ni mhasibu wa ccm na baba yake makamba ni katibu mkuu wa ccm. HIVYO ROSTAM NA MAKAMBA CHAI WANAKUNYWA PAMOJA,LUNCH PAMOJA NA VINYWAJI PAMOJA!!!!!!!!!!hatutegemei sikio likakua likazidi kichwa na ndio maana january anatetea tena tumlipe dowans!!1

    ReplyDelete
  4. Someni magazeti yote ya leo na mtakuta wanasheria wakisema hivi:“Ninachofahamu ni kwamba Dowans hawajahujumu uchumi wala kushitakiwa kwa kosa hilo la
    jinai, sasa sheria ya kuhujumu uchumi kwa suala lao itaingilia mlango gani?"Mnyika anaelewa sheria sawasawa?I mean,we must seek a legal solution to a legal problem,not a political solution to a legal problem!!!

    ReplyDelete
  5. Ama kweli sisi wadanganyika ndio tunaoliwa na kama tutaendelea kuwa na mawazo ya kijinga kiasi hiki basi safari yetu kufikia maendeleo na maisha bora kwa kila Mdanganyika itatugharimu miaka kama 1,000 hivi, Mimi nasema ninyi WATAWALA, HAWA WATANZANIA MNAOWAONA KAMA MBUMBUMBU siku zaja ambazo HAMTAONA pa kutokea, na mkumbuke siku itakapotokea FUJO ndani ya nchi yetu ninyi ndio mtakaokuwa wa kwanza kufa, MSIDHANI MTAKUWA SALAMA! ANZENI sasa kujenga usawa ACHENI KUJIGAWIA MALI YETU! kwa Watanzania kukaa kimya msidhani kuwa HAWAMJUI DOWANS NI, MNAJIDANGANYA. NANI

    ReplyDelete
  6. HIVI JAMANI, HEBU TUAMBIANE UKWELI, TUACHE USHABIKI, TUULIZANE KWANZA, NI NCHI NGAPI HAPA AFRIKA ZINAZOPITIA HALI HII? NILITAMANI SANA NIJUE NANI MWENZETU KATIKA HILI NA WANAFANYA NINI KUEPUKANA NA JANGA KAMA HILI. NA KAMA HAKUNA WA KUFANANA NAE, KWA NINI SISI? HIVI NCHI ZOTE ZINA MITO NA MABWAWA YA KUTUNZIA MAJI KAMA SISI? WANATUMIA UMEME GANI BASI? MBONA MAMBO KAMA MIPANGO YA KODI TUNAIGA KWA WENGINE, KWA NINI MAZURI PIA TUSIIGE KWAO? HIVI TUTAENDEKEZA SIASA HADI LINI? INACHEKESHA PALE AMBAPO TUNAJIDAI TUNA SERIKALI, HUKU JAMBO MOJA TU KAMA HILI TUNASHINDWA KULIPATIA UFUMBUZI MIONGO KIBAO! NAOMBA NIIASE TU SERIKALI, MIPANGO YA MAENDELEO HAIPANGWI NA KAMATI KUU YA CHAMA, NI KAZI ZA WATAALAMU NA SIO WANASIASA, TUWAACHIE KWA NAFASI NCHI ISONGE MBELE TUONDOKANE NA AIBU HII. SASA TUNAWATAFUTA WAWEKEZAJI WA NINI HUKU UMEME HATUNA, HUU SI UTAKUWA UTAPELI JAMANI? AAH! MUNGU TUSAIDIE WATANZANIA TUIONE NJIA....

    ReplyDelete
  7. Huyu January Makamba amewekwa hapo kwa maslahi ya kundi fulani.Dowans hatuitaki,afadhali tuendelee na mgawo wa umeme kuliko kurudiana na Dowans.Hivi mke mliyekatiana talaka,na mko kwenye kutathmini madai juu ya haki zake;unawezaje kuimbia mahakama Ha! naomba huyu mke turudiane???? Hawa viongozi wetu wajue wana dhamana ya kuongoza nchi siyo kundi la mafisadi.Naomba viongozi wabadilike.Waache tamaa.Ni bora mtanzania akae giza mwaka mmoja,halafu baadae tujenge vyanzo vyetu.Hizi dharura ni miradi ya mafisadi ambao wana nafasi za juu serikalini.

    ReplyDelete
  8. Wee unayejifanya ni Farmer hujui dili za viongozi wa nchi hii.Ungejua usingesema hivyo.Hali hii ya kutokuwa na umeme wa kutosha imefanywa na viongozi wa juu kabisa kwa makusudi ya kuleta mikataba ya dharura ili wapate pesa zao hapo.Au kama unajua basi wewe ni rafiki wa mafisadi.

    ReplyDelete
  9. Kumbe wabunge wengi hakuna kitu kabisa.Sikutegemea kama wataleta wazo la kutumia tena Dowans.Hii inaonyesha Tanzania haina viongozi bali wababaishaji tu.

    ReplyDelete
  10. Naomba mjue kuwa wapo viongozi wa juu serikalini ambao wanatumia mashirika ya umma kujipatia pesa.Hawana mpango na kumsaidia mtanzania masikini.Viongozi wa haya mashirika wanaendeshwa na walioshika nchi na hivyo kutumia mbinu yoyote ile ili kuchota pesa za walipa kodi.

    ReplyDelete
  11. Nchi ina wataalamu wa kutosha lakini hawawatumii.Wanaweka watu wao kila sehemu ili wachote vizuri pesa za walipakodi.Kama tungeamua kutumia wataalamu wetu hata watano tu kwenye nishati, Tanzania inaweza kupata umeme wa kutosha kwa miaka 50 ijayo.Lakini kwa sababu za wanasiasa basi hali hii ya kubabaisha katika umeme itaendelea tu hadi watapoondolewa kama Misri na Tunisia.

    ReplyDelete
  12. KWANI DUNINI MOOOTE KUNA MITAMBO YA DOWANS PEKEE YA KUFUA UMEME???????????

    HUU UFISADI UTATUMALIZA.
    SIJAWAHI KUONA VIONGOZI WANAJIPANGA KUIHUJUMU NCHI KAMA TANZANIA.

    SASA MAKAMBA KUIPIGIA DEBE DOWANS MAANA YAKE NINI?

    ReplyDelete
  13. Watanzania wezangu hili swala la kuwasha mitambo ya dowans limepangwa mezani na wahusika wanaohitaji hizo 95 bilioni,hivi sasa wanahujumu tanesco ili ionekane kwa sisi wadanganyika kuwa kuna shida kubwa ya umeme,ameandaliwa january makamba, kwanza awe mwenekiti wa kamati ya madini na nishati hilo wakashinda. la pili january kuonyesha sisi wadanganyika jinsi alivyo na uchungu na swala hili ,na hatua za haraka zijukuliwe ambalo kutumia mitambo ya DOWANS...JAMANI'' hivi kweli nchi yetu inaelekea wapi, kundi la watu wachache tu wanalitikisa taifa letu huku tunajua na kuona.wazee wetu, wahasisi wetu wapo kimya yote haya wanayaona lakini hawana huruma tena na kizazi hiki na lijalo,tayari watu hawa washajikamilisha na hivi sasa kilicho baki ni kupigiwa magoti.. wazee wetu iwapo mmetuacha watoto wenu tutapigania haki yetu japokuwa tutakufa wengi lakini msilie kwasababu mmetutenga..MUNGU TUBARIKI IBARIKI NCHI YETU..AMIN

    ReplyDelete
  14. Wanasiasa wa Tanzania watumieni wataalamu walioko vyuoni. Msijifanye tumewachagua kwa kuwa mna akili sana au mnajua mambo yote ya uchumi, sheria, fedha, na UMEME?

    Heshimuni umma mnaowaongoza.

    ReplyDelete
  15. Janauary makamba ninashuku hiyo nafasi ya uwenyekiti wa Nishati na madini, tunaelewa ulivyo karibu na JK na kwa hivyo upo karibu na Rostam pamoja na Lowassa na kwa hivyo inawezekana utakuwa umewekwa hapo kwa sababu maalum. Mzee wangu Shelukindo ktk jimbo lako ambaye umerithi viatu vyake huko aliko anatikisa kichwa kwa masikitiko, kijana wa jimbo lake unavyotaka kuendeleza na kufanikisha maslahi ya mafisadi. Tuna wasiwasi hata upungufu huu wa umeme kuwa yawezekana ni hujuma kwani mafisadi wana nguvu sana ya kifedha, wanaweza hata kuamuru maji yafunguliwe kwenye mabwawa ili tu ku-create situation mbaya na huku mkianzisha hoja ya kuwasha mitambo ukiwa kijana umewekwa kitini.

    Ni maajabu kampuni Dowans inatudai 94Bl za kifisadi then uanze kuipa biashara ya kufua umeme kwa siku 90, watch out young boy, mwanaume hawi hivyo, ni sawa kama mtu akatembea na mkewo na kesi iko mahakamani then kwa shida zako ukakubali akuletee vyakula na nguo kwa watoto wako kisa unashida.

    Jambo la kufanya, mkurugenzi wa TANESCO atathimini hali iliyopo kuwa ni ya dharura then afanye utafiti wa kampuni yenye mashine zilizo tayari kuletwa nchini for installation (for renting), aipe zabuni yenyewe peke yake (single sourcing) then mkataba uandaliwe haraka na baada ya muda mfupi tutaweza kupata mtambo unaohitajika kwa muda mfupi. Sheria ya manunuzi ina mruhusu kufanya hivyo ili mradi tu serikali ihakikishe fedha zipo kwa hitaji hilo.

    ReplyDelete
  16. ndugu zangu tanzania kuna chuo kimoja tu cha muhimbili vingine vyote walivyosoma kina mnyika hakuna kitu hata kwenye vyuo bora 2000 duniani havimo?vyuo vinafundisha watu kuongea sanaaaaaaaaaaa utaalam hakuna poleni sana wabongo

    ReplyDelete
  17. WALA SIONI AJABU KWANI WATANZANIA TUNAVUNA TULICHOKIPANDA OKTOBA 31, 2010!!!! ULIONA WAPI NCHI IKAONGOZWA NA RAIS ANAYEOGOPA KUZUNGUMZIA MATATIZO! WAKATI WOTE YEYE KIMYA TU UTAFIKIRI TATIZO LA UMEME LIPO NCHI NYINGINE NA YEYE YUPO NCHI NYINGINE! HALI INATISHA NDG ZANGU. AMKENI WATANZANIA, HAKUNA TENA KILICHOBAKI ISIPOKUWA WANASIASA KUWA WAHANDISI NA WAHANDISI KUWA WAKULIMA!!!!!

    ReplyDelete
  18. Kwani Majira haikuona breaking news ya last night? mabomu kama ya mbgala huko Gongolamboto! Mbon basi kimya hawajafanya coverage yoyote, wao pao na dowans tu! Mtakufa kwa na dowans mwaka huu! ripotini habari moto moto, dowans, dowans, richmond richmond, wenzenu weshachukua caho nyie mnabaki mnapiga kelele!

    ReplyDelete
  19. Kama Tanesco walizuia mitambo ya watu ya Dowans toka kipindi hicho kwa misingi gani wakati mitambo si yao?

    Ina maana basi walipanga kuzalisha umeme wa Dowans toka zamani. Kisha acheni kumshambulia Makamba wa watu wenye Dowans wamo humo humo Tanesco ila kwa kuwa nyinyi mmegubikwa na Rostam, Rostam, Rostam wakati nchi inaliwa na wachaga, kalaghabaho!

    Tena wachaga hawa ni wakubwa na wazito, mke wa mmoja wa wakurugenzi wa Dowans ni mchaga, mtoto wa mchaga mmoja maarufu! Lakini wanapeta tu sasa na kubaki kumlaumu Rostam. Rostam kama alihusika na Richmond wakati huo hahusiki na Dowans sasa hivi! Mkurugenzi mmoja wa Dowans aliwahi kuwa mkurugenzi wa uzalishaji hapo hapo Tanesco! Kila kitu kiko hapo hapo Tanesco. Tegueni hicho kitendawili, kinawashinda kutegua kwa kuwa mmeng'ang'ania siko, toeni mji tuwape majibu!

    Kalaghabaho,

    ReplyDelete
  20. hatutaki mitambo ya DOWANS unless imetaifishwa

    ReplyDelete
  21. MWALIMU KAMBARAGE ALISEMA IKULU SI PANGO LA WALA RUSHWA, WEZI NA MAFISADI, NADHANI HATUKUMWELEWA VIZURI. MIPANGO YA DOWANS IMESUKWA IKULU(MSIFIKIRI NGELEJA YUKO PALE KWA BAHATI MBAYA NA JANUARY KUONGOZA KAMATI HIYO NI BAHATI). NI MPANGO KABAMBE AMBAO ULIANZIA KUMTAFUTA SPIKA WA BUNGE ATAKAYELINDA MAASRAHI YA WEZI, UKAFAULU. ANGALIA SPIKA ANAVYOWAPINGA WANAOTAKA KULETA HOJA ZINAZOPINGANA NA MAASRAHI YA WEZI. HILO HATA MTOTO WA MKULIMA ANALIJUWA. SITAKI KUMZUNGUMZIA KIKWETE, LAKINI MWANAO ANAPOKUWA NI RAFIKI WA MWIZI HUHITAJI MTAALAMU WA KUKWAMBIA TABIA ZA MWANAO. HIVI WEWE DOWANS (ROSTAM, LOWASA..., JK) HAMNA HATA CHEMBE YA UTU? YA MBAGALA NA G'MBOTO NI SALAM KWAKO JK NA GENGE LAKO, WATU WAMECHOKA, AFSA WA JESHI KUJENGA NYUMBA HADI ASTAFU BAADA YA KUPEWA MAFAO YAKE,HUKU WATU WACHACHE WANAISHI MAISHA ZAIDI YA NCHI ZILIZOENDELEA?!

    ReplyDelete