01 March 2011

Nemanja Vidic ampania Torres leo

LONDON, Uingereza

BEKI Manchester United Nemanja  Vidic, anataka kumfunika Fernando Torres katika mechi ijayo dhidi ya Chelsea.Mshambuliaji huyo wa Kihispania
, Torres alipokuwa Liverpoo alikuwa akiifunga Man United kwenye mechi nyingi alizokuwa akicheza, pia alimchambua Vidic na kufunga katika mechi ambayo Liverpool ilishinda mabao 4-1 katika Uwanja wa Old Trafford.

Kutokana na kupitwa na mshambuliaji huyo, ilifanya watu kuanza kuhoji kuhusu uwezo wa beki huyo kutoka Serbia.

Leo United inacheza ugenini katika Uwanja wa Stamford Bridge na nahodha huyo wa Manchester United anajiandaa kuthibitisha kuwa hana matatizo na mchezaji mpya wa Carlos Ancelotti, aliyesainiwa kwa pauni milioni 50.

Alisema: "Wakati mwingine nimekuwa nikisoma kwenye magazeti watu wakisema nimekuwa na wakati mgumu kumkaba, lakini hilo limenifanya kwua na mtazamo zaidi katika kufanya kazi yangu.

"Nimekuwa nikijaribu kwa kadri ya uwezo wangu na mwishoni mashabiki na vyombo vya habari hutoa maoni yao. Siwezi kubadili mawazo yao kwa kuzungumza, naweza kuwabadili kwa kile nitakachofanya uwanjani."

Ushindi wa United wa mabao 4-0 dhidi ya Wigan, umeifanya United kufikisha pointi 60 wakiwa pointi nne zaidi ya Arsenal walio katika nafasi ya pili.

Ushindi dhidi ya mabingwa watetezi Chelsea, unaweza kufanya United kuwa katika nafasi nzuri ya kuweza kutwaa ubingwa na kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kutwaa kombe hilo mara nyingi (19).

Liverpool imetwaa ubingwa wa Uingereza mara 18 sawa na United.

Winga aliye katika kiwango cha juu Nani, ambaye amefunga mabao 10 na kusaidia mengine 14 msimu huu, hatacheza kutokana na kuumia katika mechi dhidi ya Wigan.

Alisema: "Tuna baadhi ya mechi ngumu zinazokuja.

"Ni kipindi muhimu zaidi katika msimu na tunaweza kuifunga Chelsea na Liverpool kisha kuwa na nafasi ya kutwaa ubingwa.

"Lakini hilo ni rahisi kusema na ni ngumu kufanya."

No comments:

Post a Comment