01 March 2011

Cole amfyatulia mwanafunzi risasi

LONDON, England

KLABU ya Chelsea imesema kwamba inachukua hatua za dhati dhidi ya mchezaji wake, Ashley Cole kutokana na taarifa za kwamba kwa bahati mbaya
, alimfyatulia risasi mwanafunzi kwenye uwanja wa mazoezi wa klabu hiyo.

Taarifa za jarida la News of the World, zilidai kuwa Cole alikuwa hafahamu kama bunduki yake aina ya rifle, ilikuwa na risasi wakati alipomlenga mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 21, Tom Cowan.

Lilieza kuwa mwanafunzi huyo wa sayansi ya michezo, ambaye yupo katika klabu hiyo kwa muda wa mwaka mmoja kwa ajili ya mafunzo ya vitendo, alijeruhiwa na risasi hiyo kwenye uwanja wa mazoezi wa klabu hiyo wa Cobham.

Timu ya wataalamu wa Chelsea, iliripoti kuwa walimpatia matibabu ya jeraha alililopata, Cowan lakini hakuhitaji kupelekwa hospitali.

Taarifa iliyotolewa jana na klabu hiyo ilieleza kuwa: "Tunafanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo na tutachukua hatua za dhati, ila hatuwezi kutoa kauli yoyote kuhusu suala hili la ndani."

Msemaji wa Polisi wa eneo hilo, alisema kwamba hakuna mashtaka yaliyofunguliwa kituoni kwao na suala hilo walilisoma kupitia vyombo vya habari na watakachofanya ni kuwasiliana na Chelsea, ili kuangalia kama kuna makosa yoyote yaliyotendeka.

1 comment:

  1. Huo ni uzembe iweje awe na bastola halafu hakagui kama ina risasi au laa? Ashukuru kuwa hakumtoa roho na pia hakujeruhiwa sana,na pia inakuwaje wanaruhusu wachezaji kuwa na silaha ktk viwanja vya mazoezi wkt kuna vyumba vya kuhifadhia mifuko yao?

    ReplyDelete