17 February 2011

Nchimbi ataka vitambulisho vya waandishi kila miaka mitatu

Na Masyeba Charles

WANAHABARI nchini wameiomba serikali na wanasiasa waache kudharau waandishi wa habari na kuondoa urasimu katika kutoa vitambulisho
vya uandishi wa habari unaowalazimisha kuviomba kila mwaka.

Maombi hayo yalitolewa hivi karibuni katika hafla fupi ya chakula cha jioni kwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dkt. Emmanuel Nchimbi mjini Dodoma.

Akijibu maombo hayo, Waziri Nchimbi aliahidi kwamba wizara yake itafanya kazi kwa kutoa ushirikiano wa karibu na wa kutosha kwa wanahabari na huo ndio msimamo wa Serikali. Pia aliongeza kwamba atakuwa akikutana na wanahabari kila mara.

Kuhusu urasimu wa kupata vitambulisho kwa waandishi, Dkt. Nchimbi alisema ataelekeza idara ya maelezo zitolewe kwa miaka mitatu badala ya kila mwaka kama ilivyo sasa.

Kauli hiyo ya Waziri Nchimbi inajibu kilio cha muda mrefu cha waandishi wa habari dhidi ya masharti ya kuomba vitambulisho vya uandishi wa habari kila mwaka kwa gharama ya sh. 20,000.

Hafla hiyo ilihudhuliwa na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari ambao walimwambia waziri kuhusu usumbufu wanaoupata wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kila siku ikiwemo kudharauliwa, kunyanyanswa na kunyanyapaliwa sehemu mbalimbali.

Waliwashtumu polisi na wanausalama na watendaji wa Idara ya Habari ya Bunge kila mara kuwa wamekuwa wakikwaza utendaji wa waandishi bila kuzingatia kwamba wanapotumwa na vyombo vyao wanakuwa wameaaminiwa na wana uwezo wa kufanya kazi husika.

Walimwambia Waziri kwamba wamefedheheshwa mnao na kauli ya Spika Anna Makinda kwa wabunge bungeni kwamba wasome magazeti kama barua nyingine, kuwa ni matusi na dharau kwa wanahabari wote na imewadhalilisha sana.

Waziri Nchimbi aliwataka wanahabari kuwa wavumilivu wakati serikali inakamilisha mchakato wa sheria ya vyombo vya habari ambayo kwa sasa iko katika sekretarieti ya Baraza la Mawaziri.

Alisema atashauriana na wahusika ili waandishi wapate nafasi ya kutosha bungeni na kupata vitendea kazi na atahakikisha kila mkoa unakuwa na ofisa habari ambaye atasaidia na wanahabari kulinda na kudumisha utamaduni wa taifa.

No comments:

Post a Comment