Na Mwandishi Maalumu
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal amewataka waumini wa dini ya kiislamu kote nchini wakati
huu wakiadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) kufanya rejea na kuishi kama alivyoishi kiongozi huyo.
Katika salamu zake kwa waislamu na Watanzania kwenye maadhimisho hayo Dkt. Bilal alibainisha kuwa kiongozi huyo wa dini ya kiislamu alikuwa mfano wa maadili mema, mjenzi wa amani na ushirikiano miongoni mwa waumini wa dini hiyo na kati ya waislamu na waumini wa dini nyingine.
“Mtume (SAW) ndio chuo cha maadili. Na sisi waislamu hatuna budi kila wakati kurejea katika chuo hiki ili kupata tiba ya mmomonyoko wa maadili katika jamii yetu.
Mmomonyoko umekuwa mkubwa,” alieleza Makamu wa Rais na kuongeza kuwa maovu yamekuwa mengi katika jamii ya Watanzania kutokana na mmomonyoko huo wa maadili.
Dkt. Bilal alifafanua kuwa wakati wa ujio wa Mtume Muhammad (SAW) maovu yalikuwa mengi katika jamii ambapo ilitawaliwa na uonevu dhidi ya wanawake na watoto wa kike, watu walikuwa hawaheshimiani na hakukuwa na uadilifu, hivyo kazi yake ilikuwa kurejesha heshma, amani na uadilifu katika jamii.
Aliwakumbusha waislamu kutafuta ufumbuzi wa matatizo yao kwa ushirikiano na kwa utulivu pamoja na kupendana, kuhurumiana na kuheshimiana na kuonya kuwa hakuna neema mahala ambapo watu hawaelewani.
“Katika mkusanyiko huu mkubwa,naona ni wajibu wangu kusisitiza suala la umoja, mshikamano na upendo miongoni mwetu sote. Hakuna rehema za Mwenyezi Mungu pahala palipojengeka uhasama na mifarakano," alisema na kutolea mfano wa Mtume Muhammad (SAW) alivyofanikiwa kuwaunganisha makundi ya waislamu wakati alipofika katika mji wa Madina.
Na kwa upande wa mahusiano kati ya waislamu na watu wa dini nyingine aliwataka waislamu wajitahidi “kuboresha mahusiano mema kati yao na watu wenye imani tofauti na wajadiliane nao kwa namna nzuri kama alivyoelekeza Mwenyezi Mungu(SW) na Mtume Muhammad (SAW),” alieleza
Kwa hiyo alizipongeza jitihada zinazofanywa na viongozi wa dini mkoa wa Dar es Salaam ambao hivi karibuni walikutana na kuzungumzia kwa mapana wajibu wa viongozi wa dini katika ujenzi wa amani na kubainisha kuwa “ni jambo jema sana na linafaa kuendelezwa kwa mustakabali wa amani ya nchi yetu kwani uislamu ni amani”.
Makamu wa Rais aliwakumbusha pia waislamu umuhimu wa kutilia mkazo elimu zote ya dini na dunia na kusisitiza kuwa huo ni wajibu wao na ni maamrisho ya kiongozi wao.
“Mafundisho ya kiislamu yametuhimiza kujifunza elimu zote mbili, elimu-dunia na elimu-akhera…tunatakiwa tutafute elimu hata katika nchi za Uchina ambapo ni dhahiri kuwa huko kulikuwa mbali na tusingeweza kupata elimu ya akhera lakini tunaweza kupata elimu ya dunia,” alibainisha.
Maadhimisho hayo yaliyofanyika katika msikiti wa Manyema Kariakoo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini ya kiislamu kutoka mikoa mbali mbali nchini pamoja na viongozi wa serikali akiwemo Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi.
No comments:
Post a Comment