21 February 2011

'Mungu asisingiziwe maafa Gongolamboto'

*Padri asema viongozi wanatakiwa kuwajibika

Na Gladness Mboma

UMATI wa wakazi wa Mzambarauni, Gongolamboto na vitongoji vyake jana walijitokeza kuaga miili ya familia moja
iliyofariki kutokana na mlipuko wa mabomu yaliyotokea Februari 16 mwaka huu katika Kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kikosi cha 511 KJ.

Mazishi hayo ambayo yalitawaliwa na simanzi yalihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa, ambapo walielezea masikitiko yao.

Miili iliyoagwa ni ya watoto Clementi na Stela na mama yao Roseneema Nyajiego ambaye ni mke wa Bw. Jacob Nyajiego aliyeonekana kuchanganyikiwa baada ya kuona majeneza ya familia yake.

Akizungumza katika ibaada ya mazishi Paroko wa Parokia ya Ukonga, Padri Stephano Nyelawila aliwataka viongozi nchini kutomsingizia Mungu kutokana na milipuko hiyo bali watu kutowajibika katika kazi zao.

"Siyo kwamba kila kitu Mungu anapanga kitokee bali viongozi hawakuwajibika, watu wasimsingizie Mungu moja kwa moja, tatizo watu hawakuwajibika,"alisema .

Paroko Nyelawila alitoa kauli hiyo baada ya Mbunge wa Ukonga Dkt. Makongoro Mahanga kuelezea masikitiko yake kwa kuadai kwamba  milipuko hiyo ilitokana na mipango ya Mungu.

Baada ya ibada hiyo marehemu wote walisafirishwa kwa ajili ya maziko katika Kijiji cha Manila Wilaya ya Rorya Musoma.

Wakati huo huo Meya wa Manispaa ya Kinondoni Bw. Yusufu Mwenda alisema kuwa siyo Manispaa ya Ilala pekee walioathirika na mabomu hayo bali hata Kinondoni yamefika na yametapakaa katika maeneo ya Kimara.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jana Dar es Salaam alisema kuwa kuna nyumba zimeathiriwa na mabomu hayo huku maeneo ambayo mabomu hayo yameangukia wananchi wamekimbia makazi kwa kuhofia usalama wao.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Bw. Charless Kenyela alisema kuwa mabomu nane yamezama ardhini katika maeneo mbalimbali Kimara.

Alisema kuwa kunahitajika wataalamu wa mabomu kufika katika maeneo hayo kwa ajili ya kuyaondoa na kwamba mpaka sasa wamekusanya mabomu sita ambayo yamehifadhiwa katika Kituo cha Polisi Mbezi kwa Yusufu, wanasubiriwa wataalamu kwa ajili ya  kuyachukua.

Alisema kuwa mabomu hayo yaliokotwa katika maeneo ya Kibamba Hospitali, Saranga, Temboni kwa Msuguli na katika maeneo ya Kiwanda cha kufyatulia tofali cha Mbezi Luis.

Hta hivyo Bw. Kinyela alisema kuwa mabomu hayo ambayo yamedondoka mashamba, barabarani na mengine maeneo ya makazi ya watu hayajaleta athari zozote kwa binadamu.

Alisema serikali inasisitiza wananchi kurudi katika maeneo yao kwani halia ni shwari.

Kamanda wa Polisi wa Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Bw. Suleiman Kova aliwaamabia wanadishi  wa habari kuwa hali ni shwari na wananchi wanatakiwa kutoa taarifa pale ambapo wanaona bomu.

Hata hivyo wakati serikali ikisisitiza wakazi hao kurudi katika mkazi yao ya kawaida wananchi wa maeneo ya Kitunda wamekuwa wakitoa malalamiko yao kwamba kuna maeneo ambayo wanaona mabomu lakini wanapotoa taarifa polisi hakuna hatua zozote zinazofanyika licha ya kusisitizwa kutoa taarifa.

 

1 comment:

  1. padre umesema ukweli. mawaziri husika na viongozi waandamizi wa jeshi wanapaswa kuwajibika. hapa hata mama makinda anapawsa kuwajibika kwa kukataa bunge kujadili hii habari...tanzania chini ya kikwete si salama

    ReplyDelete