21 February 2011

Mabomu yasitumike kutafuta umaarufu

Na Charles Mwakipesile, Mbeya

WATANZANIA wametakiwa kuacha malumbano kwa lengo la kutafuta  umaarufu kutokana na milipuko ya mabomu iliyokea katika Kambi ya Jeshi la
Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kikosi cha 511 KJ  Gongolamboto badala yake watumie muda huo kumuomba Mungu ili maafa mengine yasitokee.

Onyo hilo lilitolewa na Askofu Kiongozi wa Kanisa la Moravian Tanzania, Alinikisa Cheyo wakati akitoa tamko la kanisa hilo na salamu za rambirambi kwa Rais Jakaya Kikwete kutokana na vifo vya zaidi ya watu 20 na majeruhi zaidi ya 315 kutokana na milipuko hiyo ya mabomu kwenye kambi hiyo JWTZ.

Alisema kuwa kanisa hilo linatambua kuwa Watanzania waliopata maafa hayo ni sehemu ya waumini wake hivyo limeguswa na kuona huruma kutokana na mahangaiko makubwa yanayofanywa na serikali kwa maafa hayo hivyo si wakati wa kulaumiana.

"Unajua kulaumiana na kutumia siasa wakati huu maana yake ni kupoteza lengo la tukio hilo na kuingilia kazi ya wapiganaji ambao kwa sasa wamejipanga na kuunda kikosi kazi kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo na hatimaye kuibuka na majibu ambayo yatakuwa mwendelezo wa amani na utulivu uliopo nchini," alisema.

Askofu Cheyo alisema kuwa Watanzania lazima wajifunze kutambua  wakati wa malumbano na wakati wa kufarijiana ambao alisema kuwa ndio huu, ambapo aliwasihi wadau wote wakiwemno wanasiasa kusahau tofauti zao na kuungana katika kuhakikisha kuwa hali ya usalama  na faraja kwa waathirika vinapatikana.

No comments:

Post a Comment