Na Gladness Mboma
MKE wa Waziri Mkuu Bi. Tunu Pinda ameiomba serikali kuhakikisha kwamba inaangalia maghala mengine ya silaha ili kuepuka matatizo ya milipuko
kama yaliyotokea Gongolamboto na Mbagala.
Kauli hiyo aliitoa jana Dar es Salaam wakati akiongoza ujumbe wa baadhi ya wake wa viongozi ambao walitembelea waathirika wa mabomu yaliyotokea katika kambi ya 511KJ Gongolamboto Februari 16 mwaka huu.
"Tumekuja kutoa pole kwa wananchi wenzetu waliopatwa na haya majanga ya mabomu, lakini pia tungeomba hayo maghala mengine yaangaliwe ili isiweze kutokea matatizo kama hayo," alisema.
Bi. Pinda alisema kuwa anawaombea Mungu awape uvumilivu na ustahimilivu watu wote waliokumbwa na majanga hayo, ambapo ameishukuru serikali kwa kuwahudumia waathirika hao.
Alisema kuwa inapotokea majanga kama hayo, wakina mama ndio wanaoumia zaidi kutokana na kubeba mzigo wote wa watoto kukimbia nao.
Wake wa viongozi hao wametoa msaada wa vitu mbalimbali kwa waathirika hao vyenye thamani ya sh. milioni 1.5.
Naye Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Meck Sadick akitoa ufafanuzi kuhusiana na mlipuko wa mabomu hayo kwa wake wa viongozi hao, alisema kuwa Jeshi limejipanga vizuri na kwamba matukio yote ya mabomu yaliyotokea ni kama bahati mbaya.
"Siku tatu kabla ya mlipuko ukaguzi ulifanyika katika maeneo yote yanayotunzwa silaha na walijiridhisha. Hili ni tatizo lilotokana na mapenzi ya Mungu," alisema.
Alisema kuwa mpaka sasa wanashindwa kuelewa ni nyumba ngapi zilizopatwa na maafa hayo pamoja na watu wangapi wanahitaji msaada kutokana na kupata taarifa tofauti.
Bw. Sadick alisema mpaka sasa kuna maiti sita ambazo zimeripotiwa kutokana na milipuko ya mabomu, lakini wanazifanyia uchunguzi kuangalia kama kweli zinatokana na mlipuko huo au la.
"Kati ya maiti hizo nne zimetambuliwa wakati mbili mpaka sasa hazijatambuliwa lakini zina majina, ambapo moja wapo haijulikani ni ya jinsia gani kutokana na kukatika katika vipande," alisema.
Alisema kuwa maiti nne zimekwishasafirishwa na nyingine kuzikwa hapa jijini, ambapo serikali imegharamia mazishi na usafiri na kwamba kilichobaki kwa sasa ni kutoa mkono wa pole kwa wafiwa wote.
Bw. Sadick alisema kuwa kwa wale waliopata ulemavu wa kudumu serikali itawapatia kifuta machozi na kwamba kwa sasa wanafanya tathmini ya mali na nyumba zilizoathiriwa na mabomu hayo.
Alisema kuwa bado kunahitajika misaada kwa waathirika hao kutokana na tathmini kuchukua miezi miwili hadi mitatu na kwamba jumla ya familia 120 zimejengewa mahema.
Bw. Sadick ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kama kuna kiwanda kinanunua masalio ya mabaki ya mabomu kama chuma chakavu ili kiweze kuchukuliwa hatua.
Alisema kuwa mabomu yaliyosambaa katika maeneo mbalimbali jijini ni mengi na hayawezi kuisha kwa sasa na kuwataka wananchi kutoa taarifa pale wanapoyaona.
Bw. Sadick alisema kuwa tatizo hilo linatokana na ghala hilo kuwa kuu la silaha tofauti na yale ya Mbagala na kusisitiza kwamba mengi yamesambaa.
Hao waheshimiwa wanaopanga mstari kwenda kuwajulia hali walioumia kwa mabomu,wanafanya hivyo kwa masilahi yao.Huo ni ubinafsi tu.Waache wagonjwa watulie na wahudumiwe na ndugu zao tu. Wagonjwa hawawezi kupata hata usingizi kama kila mheshimiwa atataka kuwatembelea. Waende wakaongee na Jeshi ili kitu kama hiki kisitokee tena.
ReplyDelete