Na Mussa Soraga, Zanzibar
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limesogeza mbele mechi mbili za kimataifa za KMKM na Zanzibar Ocean view zilizopangwa kufanyika
ugenini mwishoni mwa wiki hii, dhidi ya timu za Motema Pembe na AS vita zote za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa jana na Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), kupitia Katibu Msaidizi Masoud Attai alisema mechi hizo sasa zitafanyika mwishoni mwa mwezi huu ambapo KMKM itacheza na Motema Membe Februari 25 na Ocean view itachuana na Vita Februari 27, mwaka huu.
Attai alisema, chama chake kimepokea barua kutoka CAF iliyotoa uamuzi huo wa kuaharishwa kwa mechi hizo mbili baada ya kuyakubali maombi ya timu za Congo kutokana na wachezaji wao kuwemo kwenye timu yao ya taifa.
Alisema DRC hivi sasa ipo nchini Sudan na inashiriki kwenye michuano ya nchi za Afrika, ambazo hazina wachezaji wa kulipwa na kwa mujibu wa Katibu huyo wa ZFA, Vita ina wachezaji wanne wakati Motema Pembe inao watatu.
"Tumepokea taarfa hiyo kutoka CAF iliyotoa agizo la kuzitaka timu zetu za KMKM na Ocean view, kusubiri hadi mwishoni mwezi huu," alisema Attai.
Attai alisema kati ya timu hizo mbili, KMKM ambayo ilikuwa iondoke jana ndiyo iliyoathirika zaidi kwani ilikuwa tayari imekwishakata tiketi, ambapo imebidi ilipe fidia kutokana na kutaka iisogezewe mbele safari yao.
Katika michezo ya awali Ocean view ilitoka sare ya bao 1-1 na Vita na hivyo kuhitaji ushindi wa bao 1-0 ili iweze kusonga mbele, wakati KMKM ina kazi ya ziada kwani inahitaji ushindi wa mabao 5-0 kutokana na kufungwa mabao 4-0 ikiwa nyubnani na timu ya Moterma Pembe.
No comments:
Post a Comment