Na Nayla Abdulla
KAMPUNI ya simu za mkononi, Airtel Tanzania imetangaza zawadi za washindi wa michezo mbalimbali zitakazotolewa katika tamasha la waandishi wa
habari litakalofanyika Jumamosi katika viwanja vya TTCL Kijitonyama, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Meneja Uhusiano wa Airtel Muganyizi Mutta, alisema wameandaa zawadi za kuvutia katika kuongeza hamasa ya ushindani miongoni mwa vyombo vya habari, vitakavyoshiriki michezo husika.
Alisema pamoja na vikombe kwa washindi wa mpira wa miguu, netiboli, kuvuta kamba, kucheza dansi na kuimba, lakini pia kutakuwa na zawadi za papo kwa papo kwa michezo mbalimbali ya kubahatisha itakayochezeshwa na kampuni hiyo ambapo pia kutakuwa na zawadi ya kombe kwa ajili ya mshindi wa jumla.
“Tumeandaa zawadi mbalimbali za kuvutia katika kuongeza hamasa na ushindani kwa washiriki, lakini pamoja na hilo kutakuwa na zawadi za promosheni kwa michezo tofauti ya kubahatisha itakayochezeshwa na Airtel, yote hayo ni katika kuhakikisha watakaoshiriki wanaburudika kwa kiwango chake,” alisema Mutta.
Hii ni mara ya pili kwa Airtel iliyobadilishwa jina kutoka Zain kufanya tamasha kwa wanahabari, ambapo la kwanza kama hili kwa wanahabari lilifanyika mwaka 2009.
Kwa upande wa burudani alisema bendi ya Msondo Ngoma 'Baba ya Muziki' italipamba tamasha hilo na tayari bendi hiyo ipo kamili kuporomosha burudani siku hiyo ya aina yake kwa wanahabari nchini.
Kwa upande wake Mratibu wa tamasha hilo, Mawazo Waziri wa Kampuni ya Capital Plus International alisema maandalizi yamekamilika na kila kitu kipo katika mstari kusubiri siku ya tamasha, ambapo alitoa rai kwa washiriki kuwahi ili ratiba ya michezo iweze kwenda kama ilivyopangwa.
No comments:
Post a Comment