Na Zahoro Mlanzi
TIMU ya taifa Tanzania 'Taifa Stars', jana ilitoka kifua mbele dhidi ya Palestina baada ya kuilaza bao 1-0 katika mechi iliyopigwa Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Bao hilo la ushindi wa Stars lilifungwa dakika ya 62 na Mrisho Ngassa, ambaye alimchambua kipa wa Palestina Abdallah Alsadawi baada ya kupokea pasi kutoka kwa Mohamed Banka.
Mechi hiyo ilianza kwa kasi na timu zote kushambuliana kwa zamu, ambapo Stars ndiyo iliyokuwa ya kwanza kubisha hodi kwa wapinzani wao dakika ya tano baada ya Mussa Hassan 'Mgosi', aliyepokea pasi ya Ramadhan Chombo 'Redondo kupiga shuti kali lililopanguliwa na kipa Abdallah Alsadawi.
Palestina ilijibu shambulizi hilo dakika ya 16, ambapo mshambuliaji wake Shatrif Ali kukosa bao la wazi akiwa na kipa Shaban Kado, lakini hata hivyo alikosa baada ya kupiga shuti dhaifu lililodakwa na mlinda mlango huyo.
Dakika ya 18 Ngassa, aliikosesha Stars bao la wazi baada ya kupasiwa mpira mrefu na Jabir Aziz, lakini hata hivyo alipiga mpira fyongo.
Kipindi cha pili kilianza kwa Stars kuliandama lango la wapinzani wao na dakika ya 51 Mgosi, akiwa ndani ya 18 alishindwa kuifungia bao timu yake baada ya kupiga mpira ovyo.
Palestina ilijibu shambulio hilo dakika ya 54, Fahed Aftal alipiga shuti kali lililookolewa na mabeki wa Stars.
Dakika ya 86 Julius Mrope wa Stars aliyechukua nafasi ya Ngassa aliwalamba mabeki wanne wa Palestina na kutoa pasi murua kwa Godfrey Bonny aliyeingia badala ya Mgosi kupiga mpira nje akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga.
Sawa na jeshi la Tanzania lilivyotamba kumfingisha virago President Bacari wa Anjuan, Comoro. Mnapendaz kujisifia mnapowashinda vibonde, ha ha haaa.
ReplyDelete