LONDON, England
MICHUANO ya Klabu Bingwa Ulaya, inatarajia kuendelea tena wiki hii kwa kuikutanisha tena miamba mingine minane, kati ya miamba 16 inayowania
ubingwa wa michuano hiyo.
Miamba hiyo itakayoshuka kwenye viwanja vinne tofauti kesho na keshokutwa ni FC Copenhagen ya Denmark itakayoikaribisha Chelsea na Lyon ya Ufaransa, ambayo itakuwa ikiumana na Real Madrid huku Inter Milan ikikwaruzana na Bayern Munich, wakati Marseille itakuwa ikiikaribisha Manchester United.
Mechi hizo zinatarajiwa kuwa na vuta ni kuvute kutokana na historia ya timu hizo na viwango zilivyonavyo kwa sasa katika michuano mbalimbali barani Ulaya, hususani kwenye michuano ya Ligi za nchi zinakotoka.
Hata hivyo macho na masikio ya mashabiki vinatarajiwa kuelekezwa katika mechi ambazo zinazikutanisha timu za England Chelsea na Manchester United, kutokana na kuwa ndizo zina mashabiki wengi hususani wanaolipenda soka la Uingereza. .
Katika mchezo utakaoikutanisha Chelsea na Copenhagen, mabingwa hao wa Uingereza wao watashuka uwanjani wakiwa na nia moja ya kurekebisha makosa, ambayo wameyafanya katika mechi zao za nyuma baada ya kuboronga kwenye michuano ya Ligi Kuu na kocha wa timu hiyo, Carlo Ancelotti ameshatangaza jihadi akisema kuwa anataka kuhakikisha timu hiyo inatwaa taji hilo msimu huu.
Ili kuhakikisha timu yake inafanya vyema, wakati wa usajili wa dirisha dogo wa mwezi uliopita kocha huyo aliimarisha kikosi chake kwa kusajili mchezaji aliyeweka rekodi katika usajili wa England, Fernando Torres kwa kitita cha pauni milioni 50.
Lakini hata hivyo mchezaji huyo, bado hajaonesha cheche zake baada ya kushuhudiwa mechi yake ya kwanza akishindwa kupachika bao, dhidi ya timu yake ya zamani Liverpool na mchezo wa pili na Tottenham pia akishindwa kufurukuta na kuifanya timu yake ya Blues iambulie sare.
Mbali na mchezaji huyo pia kiungo wa timu hiyo, Frank Lampard naye ameshatangaza kuweka kando michuano ya Ligi Kuu na kuelekeza jitihada zake katika kuhakikisha timu yake inashinda taji hilo la Klabu Bingwa.
Kwa upande wao Manchester United, watashuka uwanjani wakiwa na rekodi nzuri, baada ya kushinda mechi nyingi za Ligi Kuu pamoja na mashindano mbalimbali England.
No comments:
Post a Comment