Na Omari Moyo, Arusha
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro wamepinga maamuzi ya serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, kuhusu rasimu iliyoandaliwa na tume ya taifa ya matumizi bora ya ardhi katika wilaya hiyo.
Walisema kwamba mpango huo hauna lengo zuri kwa wakulima na wafugaji waliomo ndani ya wilaya hiyo kwa eneo kubwa la matumizi ya ardhi linakwenda kwenye vitalu vya kuwinda na siyo kwenye
matumizi ya binadamu.
Wakizungumza na waandishi wa habari kupitia mwenyekiti wa baraza hilo, Bw. Elias Ngorisa alisema kuwa maamuzi hayo ya matumizi ya ardhi wilayani humo yalifanywa kimya kimya bila kuwashirikisha
wananchi wala vyombo vya uwakilishi.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa uamuzi huo ni tishio kubwa la amani ya nchi, kwa kuwa kutowashirikisha wananchi katika suala muhimu kama hilo la ardhi na kutoa maamuzi ya kuwanufaisha wawekezaji, suala hilo halikubaliki.
“Suala hili limekuwa na matatizo mengi sana ikiwa mapigano ya sisi kwa sisi wa jamii ya wafugaji kuhusu kugombea ardhi na kuuana bila sababu na maamuzi hayo yametuacha tukiteseka sana tunaomba wabatilishe maamuzi hayo,” alisema mwenyekiti huyo.
Akiilalamikia serikali, Bw. Ngorisa alisema kuwa serikali imeshindwa kutambua umuhimu wa wafugaji wilayani humo ikiwa ni pamoja na kuwaita raia wa Kenya, waharibifu wa mazingira, na kuchomewa moto makazi yao na kuacha kuwashirikisha kwenye mipango ya matumizi bora ya ardhi kwenye wilaya hiyo.
“Sisi walitakiwa kutushirikisha kwa kila hatua kuhusu matumizi bora ya ardhi ya wilaya yetu, kama hawatushirikisha sisi kauli yeti ni kwamba hatukubali kuonewa na sisi ni wazaliwa halali na hatutahama hapa,” alisema Bw. Ngorisa.
Moja ya masuala wanayolalamikia ni kubadilishwa kwa pori la akiba kutoka Game Controlled Area (eneo linaruhusu uwindaji na shughuli za kibinadamu) na kuwa Game Reserve, hatua itakayofanya wakazi wote wa eneo hilo kuondoka kwa kuwa matumizi yoyote ya shughuli za binadamu hayataruhusiwa.
Hatua hiyo inaelezwa kuwa itawamaliza wafugaji kwa kuwa hawana sehemu nyingine ya kukimbilia na asili yao ni Ngorongoro.
Kwa pamoja wamemuomba Rais Jakaya Kikwete kuangalia suala hilo kwa umakini zaidi ili kuwanusuru wananchi wake na matumizi ya Ardhi wilaya ya Ngorongoro na yeye ndiye mwenye mamlaka ya mwisho.
Uhaba wa ardhi umesababisha mapigano ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji na kusababisho vifo vya watu wasio na hatia na wengine kupata vilema vya maisha.
No comments:
Post a Comment