Na Waandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete amesikitishwa na mlipuko wa mabomu katika kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Brigedia 511 Gombo la Mboto Dar es salaam na
kuweka wazi kuwa tukio hilo ni maafa makubwa na la kushtua.
Pia Rais Kikwete amewataka wananchi kutulia na kurejea kwenye makazi yao kuendelea na shughuli zao kama kawaida kuwa kipindi cha hatari kimepita na kuwataka kupuuza taarifa za uzushi kuwa mlipuko zaidi utatokea.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kutembelea kambi hiyo na kujionea uharibifu mkubwa kambini hapo jana, Rais Kikwete alisema serikali imechukua hatua za haraka juu ya tukio hilo hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi.
"Nilipata taarifa za tukio hilo jana usiku, na nikataka nikutane na Mkuu wa Majeshi lakini akanitaarifu kuwa wanaendelea na harakati za kuangalia tatizo hilo. Baadaye saa tisa usiku nilikutana naye na kunipa taarifa za tukio hilo.
"Ni maafa makubwa, siyo jambo dogo ni la kushtua, lakini kipindi cha hatari kimepita, wananchi wasiwe na wasiwasi, wapuuze taarifa kwamba milipuko zaidi itaendelea hizo ni taarifa za radio mbao, hakuna mabomu yatakayoendelea," alisema Rais Kikwete na kuongeza
"Leo (jana) mchana nitakuwa na kikao cha Kamati ya Usalama na baada ya kumaliza nitatoa taarifa," alisema.
Rais Kikwete ambaye alifika katika kambi hiyo saa 6:00 mchana, alisema kambi ya Gombolamboto ndio ghala kubwa ya kuhifadhia silaha na kwamba kulipuka kwa kambi hiyo ni jambo la kushtua, lakini bado nchi iko salama kwa vifaa vya kutosha.
Waziri wa Ulinzi
Hata hivyo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dkt. Hussein Mwinyi, hakuwa tayari kusema lolote juu ya tukio hilo kwa maelezo kuwa aliyosema Rais Kikwete yanatosha.
"Siwezi kusema lolote aliyokwishasema mheshimiwa Rais yanatosha kwa sasa," alisema Dkt. Mwinyi.
Luteni Generali Abdulrahaman Shimbo
Akijibu maswali ya waandishi Habari Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Abdulrahaman Shimbo, alisema licha ya mlipuko huo hali ya usalama wa Taifa kiulinzi ni nzuri na kwamba wananchi wasifikiri kwamba Jeshi hilo linaweza kuwa na upungufu wa silaha kutokana na tukio hilo.
Alisema tayari Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange ameunda kikosi cha uchunguzi kubaini chanzo cha tukio hilo na kwamba taarifa kamili itatolewa baada ya kazi hiyo kukamilika.
Alisema watu 20 walikuwa wamepoteza maisha kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa hadi jana mchana huku zaidi ya 300 wakiwa wamejeruhiwa na kwamba mlipuko wa mabomu yaliyolipuka yanaweza kusafiri hadi umbali wa kilomita 20 lakini yakiwa kwenye mtutu wake.
Alisema kazi ya kukusanya mabaki ya mabomu katika makazi ya wananchi ilitarajiwa kuanza muda mfupi baada ya Rais Kikwete kuondoka katika kambi hiyo na kuwaomba wananchi wasiwe na wasiwasi kwa kuwa mabaki hayo hayawezi kulipuka tena bila shinikizo mkubwa.
"Nawaomba wananchi wasiwe na wasiwasi, hayo mambomu hayawezi kulipuka tena , hata kama yapo katika makazi yao, lakini wasiyacheze wala kuyagongagonga.
Kazi ni kubwa sana, niwahakikishie, lakini uko wanakoishi watu ndipo tutakapoanzia kukusanya mabomu hayo, tunayo orodha ya wananchi waliotupigia simu," alisema Luteni Jenerali Shimbo.
Alipoulizwa kuhusu chanzo cha tukio hilo kwa kuzingatia kuwa hii ni mara ya pili kwa mabomu kulipuka ndani ya kipindi cha miaka miwili alisema matukio hayo hayalingani wala hayafanani kwa kuwa yana vyanzo tofauti.
Alisema mlipuko wa Aprili mwaka 2009 ulitokea katika kambi ya Mbagala ulitokea wakati wanajeshi wakiwa kazini lakini tukio la juzi usiku ulitokea usiku wakati mabomu hayo yakiwa yametulia.
"Kwanza haya matukio hayafanani, tukio la kwanza ni tofauti na tukio hili, la kwanza lilitokea watu wakifanya kazi ndani ya ghala, hili limetokea usiku ghala likiwa peke yake, msije mkalinganisha matukio haya," alisisiza.
Alipotakiwa kueleza iwapo JWTZ itahitaji msaada kutoka nje wakati wa uchunguzi wa tukio hilo na muda wa uchunguzi na kutoa taarifa hiyo alisema watalamu wa jeshi hilo wanatosha kufanya kazi hiyo lakini akakiri kuwa ni kazi kubwa.
"Uchunguzi wa kitaalamu ni muhimu sana, tunao wataalamu wa kwenda kuchunguza, tunajua ni ghala namba tano ndio lilianza kulipuka, tutachgunguza vitu vilivyokuwa ndani ya gahala hilo na takwimu zake, kutoka hapo tutajua kila kitu, ndio maana tumezuia watu kuingia pale ili kutoharibu ushahidi wakati wa uchunguzi," alisema.
Alipoulizwa iwapo mlipuko wa mabamu hayo umetokana na muda wake kupita, alisema tarifa hizo ni za uzushi kwa kuwa tukio hilo limetokea siku tatu tu baada ya ukaguzi uliobaini kuwa silaha hizo ni salama.
Alisema baadhi ya sialha hizo ni za septemba mwaka jana hivyo hakuna wasiwasi kuhusu ubora wake.
Alipotakiwa kueleza vitu vinavyoweza kusababisha mabomu kulipuyka alisema vipo vyanzo vingi ikiwemo moto na radi na kwamba baada ya uchunguzi wa kina watajua chanzo halisi ya tukio hilo na kwamba ya hewa ulikuwa safi.
Alipoulizwa kuhusu umbali ambao mabomu hayo yanaweza kwenda alisema ni kilomita 22 ikipigwa kwenye mzinga wake na kwa mlipuko kama ulivyotokea inaweza kuwa kilomita tano hadi 11.
Alisisitiza kuwa JWTZ haina mpango wowote kuhamisha kambi hiyo kwa kuwa ni muhimu kwa ulinzi na usalama wa Taifa na kuwaomba wananchi kuheshimu sheria ya kukaa jirani na kambi za jeshi kwa kuwa lipo kwa ajili ya usalama wao wenyewe na kwamba kambi hiyo ilijengwa mwaka 1971.
Alisema wakati kambi hiyo ilipojengwa eneo hilo lilikuwa pori huku kukiwa na Shule ya Sekondari ya Pugu pekee na kwamba wananchi walifuta kambi hiyo lakini si jukumu lao kuwahamisha na kwamba wanalazimika kuishi nao jirani kama Jamii.
Alisema zipo uchunguzi wa aina mbili ikiwemo ya kwao kama JWTZ na ile ya serikali ambayo hata wao watahojiwa kama wahusika.
Awali akitoa taarifa ya tukio hilo kwa Rais Kikwete Mkuu wa Kikosi hicho Luteni Kanali Aloyce Mwanjile, alisema jumla ya gahala 23 za silaha ziliteketea, magari mawili ya maji, magari mawili mapya kabisa ambayo yalikuwa hayjaanza kufanya kazi pamoja na Ofisi zote za kambi ziliathirika licha ya zile zilizoteketea kabisa.
Alisema pia mabweni ya askari iliteketea na vitu vyote huku mwanajeshi moja akijeruhiwa mkononi.
Alitaja maeneo ambayo mabomu hayo yalisambaa kuwa ni Pugu Kajiungeni, Yombo Vituka, Tabarta, Gombo la Mboto, Kivule na maeneo ya Tazara.
Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa JWTZ Luteni Kanali Kapambala Mgawe,alisema kati ya watu 20 waliothibitishwa kupoteza maisha katika tukio hilo 13 walikufa kwa mabomu hayo huku saba wakipoteza maisha kutokana na mshtuko.
Alisema hadi jana mchana jumla ya watu 300 waliripotiwa kujeruhiwa na kuwaomba wananchi kupata taarifa sahihi kutoka katika Jeshi hilo au viongozi wa serikali na si za mitaani zinazoweza kuwachanganya.
Majira ilishuhudia umati wa watu wakiendelea kuwatambua watoto na ndugu zao katika uwanja wa Uhuru huku wadau mbalimbali wakiwemo chama cha Msalaba Mwekundu, Kampuni ya Vinnjwaji sayona, Tume ya Taiga ya kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) zikitoa misaada ya aina mbalimbali.
Serikali iliwaomba wananchi ambao wanatafuta ndugu zao au wale walio na watoto wasiowajua kuwapeleka katika uwanja huo au vituo vya polisi ili waweze kutambuliwa na ndugu zao.
Imeandaliwa na John Daniel, Benjamin Masese na Rabia Bakari
Inaonesha JWTZ wanapuuza sana sera ya Afya, Usalama na Mazingira(HSE) katika maeneo yao.
ReplyDeleteWawajibishwe mara moja na lazime iwepo accountability kwa yeyote aliezembea kazi yake.
Kuna silaha zimeteketea lakini pia inawezekana huu ulikuwa mpango wa baadhi ya wahujumu kuiba silaha hizo kwa matumizi ya kihalifu na hata ya kihaini! Don't leave any stone...!
Roho za raia zimepotea, mali zao pia. Serikali, kwa upande wake, lazima IFIDIE hasara hii na ikiwezekana mahakama zitumike kuwapa fundisho watendaji waliozembea.
Tathmini ifanywe kuangalia usalama wa ghala zote za silaha nchini zilizo karibu na maeneo ya wanachi.
Kuna conspiracy hapa.
ReplyDelete