Na Zahoro Mlanzi
KLABU ya Simba, imetangaza viingilio vya mchezo wao wa marudiano wa Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Elan de Mitsoudje kutoka Komoro kwamba
cha chini ni sh. 3,000 na cha juu sh. 20,000.
Mchezo huo unatarajiwa kupigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, lakini licha ya kutangaza viingilio hivyo, wapinzani wao ujio wao umekuwa na mashaka kutokana na juzi asubuhi kukosa usafiri wa kuja Dar es Salaam.
Akizungumza Makao Makuu ya klabu hiyo Mtaa wa Msimbazi jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Geofrey Nyange 'Kaburu', alisema wameamua kupanga viingilio hivyo ili wanachama wao na mashabiki wa soka wajitokeze kwa wingi kuishangilia timu hiyo ambayo inaiwakilisha nchi katika mashindano hayo.
"Viingilio ni vya kawaida kabisa ambapo Viti Maalum ni sh. 20,000, Jukwaa Kuu ni sh. 15,000, Jukwaa la kijani ni sh. 8,000 na mzunguko ni sh. 3,000 na kwamba mchezo huo utachezeshwa na waamuzi kutoka Rwanda na Zambia ambao kesho (leo) watatua nchini," alisema Kaburu.
Alisema wamechagua kutumia uwanja huo ili kuepusha gharama kwa kutumia Uwanja wa Taifa, kwani una makato makubwa, hivyo wakitumia uwanja huo waliouchagua utaweza kuepusha gharama hizo.
Akizungumzia ujio wa wapinzani wao, Kaburu alisema walipokea simu juzi kutoka Comoro ikiwaarifu kwamba, wangekuja siku hiyo, lakini ndege waliyopaswa kuja nayo, ilikwama Afika Kusini, hivyo walitegemea ndege ya jana mchana.
Alisema endapo kama ndege hiyo wataikosa itabidi wasubiri ndege nyingine kutoka Mombasa ambayo itatua nchini humo leo na ikishindikana kabisa watalazimika kutumia usafiri wa barabara wakiwa na msafara wa watu 30 na watakuja na mashabiki wao.
Mbali na hilo, aliongeza kwamba, kwa mujibu wa benchi la ufundi la timu hiyo, kikosi chao kinaendelea na mazoezi ambapo kimeongezwa nguvu na wachezaji Emmanuel Okwi na Rashid Gumbo, ambao walikuwa majeruhi, lakini kwa sasa wameanza mazoezi.
Alisema Hilary Echessa atakuwa nje ya uwanja kwa wiki mbili baada ya kuumia kifundo cha mguu na pia alitoa tahadhari kwa wanaouza jezi zao kinyume na taratibu na kwamba, watawachukulia hatua za kisheria.
No comments:
Post a Comment