01 March 2011

Kikwete ateua makatibu wakuu watano

Na Mwandishi Maalumu

RAIS Jakaya Kikwete amewateau makatibu wakuu watano wapya na kuwahamisha wengine wanne kutoka wizara moja kwenda nyingine.Taarifa iliyotolewa
Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Bw. Phillemon Luhanjo ilisema kuwa mabadiliko hayo yanatokana na muundo mpya wa serikali ambako Wizara ya Miundombinu imegawanywa katika wizara mbili na baadhi ya makatibu wakuu kustaafu kazi kwa mujibu wa sheria.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Kikwete amemteua Bw. Fanuel E. Mbonde kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ikulu. Kabla ya uteuzi wake Bw. Mbonde alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu.

Wengine walioteuliwa ni Bi. Hussein A. Kattanga kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Bw. John M. Haule kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa; Bw. Herbert E. Mrango kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi; na Bw. Eric K. Shitindi kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Kazi na Ajira.

Kabla ya uteuzi wake Bw. Kattanga alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto; Bw. Haule alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha; Bw. Mrango alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Bw. Shittindi alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Kuhusu uhamisho, Rais Kikwete amemhamisha Bw. Sazi B. Salula kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwenda kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais; Bibi Maimuna K. Tarishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwenda Wizara ya Maliasili na Utalii; Injinia Omar A. Chambo kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi akitokea Ukatibu Mkuu wa Wizara ya zamani ya Miundombinu; na Bibi Kijakazi R. Mtengwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.

Taarifa hiyo ya Ndugu Luhanjo imesema vile vile kuwa Dkt. Ladislaus C. Komba, aliyekuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii anapangiwa kazi maalumu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Aidha, taarifa hiyo imesema kuwa Rais Kikwete amemhamishia Bibi Elizabeth J Nyambibo Wizara ya Fedha na Uchumi ambako anachukua nafasi ya Naibu Katibu Mkuu iliyoachwa wazi na Bw. John H. Haule. Kabla ya uhamisho wake, Bi. Nyambibo alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Taarifa hiyo ya imesema kuwa uteuzi na uhamisho huo unaanza mara moja na makatibu wakuu wapya wataapishwa leo saa tatu asubuhi.

No comments:

Post a Comment