01 March 2011

Wanafunzi IFM wagomea mitihani

Na Mwandishi Wetu

WANAFUNZI wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) wamegoma kuingia madarasani kufanya mitihani iliyotakiwa kuanza mapema leo kwa madai ya
kushinikiza uongozi kuwaruhusu wanafunzi wasiomaliza ada kufanya mitihani hiyo.

Mgomo huo ulianza jana asubuhi ambapo wanafunzi hao waligoma kuingia darasani kusubiri kuanza mitihani ambayo ilitakiwa ianze saa 2:00 asubuhi na kuamua kukusanyika katika eneo la wazi la chuo hicho na kuanza kuimba nyimbo za kushinikiza kudai haki hiyo.

Rais wa Serikali ya Wanafunzi, Bw. Boniphace Edward amesema kuwa wanafunzi hao hawajagoma bali wamekusanyika kudai haki zao.

Bw. Edward alisema moja ya madai yao ni kutaka wanafunzi wenzao walioshindwa kukamilisha ada kwa asilimia 70 kuruhusiwa kuingia kwenye vyumba vya mtihani na kufanya mitihani hiyo.

Madai mengine ni pamoja huduma mbaya kutoka kwa uongozi, lugha za manyanyaso pamoja na ucheleweshaji wa vitambulisho vya mitihani kwa waliokwishalipa ada.

"Wanafunzi hawajagoma bali tumekusanyika hapa ili kudai haki ya wengi ambao ni walala hoi ambao wameshindwa kukamilisha taratibu za ada na kutakiwa kutoingia kwenye mtihani, hivyo tutakaa hapa hadi menejimenti itakaporuhusu wenzetu hawa nao kufanya mtihani," alisema Bw. Edward.

Mmoja wa wanafunzi hao, Bw. Meshack Washanje wa kozi ya BBF alisema yeye ni mmoja wa wanafunzi wasiokamilisha asilimi 70 ya ada na alishaiomba menejimenti kuhusiana na matatizo hilo lakini hakupata ushirikianao zaidi ya kupewa majibu ya kejeli ya kutakiwa asitishe masomo kwa kushindwa kulipa ada.

Mwanafunzi mwingine ambaye alidai hajatimiza kiwango hicho cha malipo Leon Mboya alisema amefikisha asilimia 60 ya malipo lakini hata yeye pia licha ya kuandika barua ya kuomba kufanya mitihani, hajaruhusiwa.

Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Godwin Mjema alisema ameshangazwa na mgomo huo wa mtihani wakati tayari walishatoa tangazo la kuwataka wanafunzi wote kuingia madarasani na kufanya mtihani huku wale wasiomaliza taratibu za kulipia hadi leo walitakiwa kufanya mitahani hiyo na kuendelea kufanya utaribu wa kulipia.

"Kitendo hiki kimetushangaza na kutusikitisha, kwani tulishawatangazia wanafunzi wote waingie madarasani, na wale wasiomaliza ada wangeendelea kulipia na cha kushangaza zaidi leo tukakuta matangazo yao yakidai kuwa hakuna mitihani hiyo," amesema Prof. Mjema.

Prof. Mjema amasema Chuo hicho kianendeshwa kwa sheria na taratibu, lakini inashangaza hadai wakati mgomo huo unatokea hakuna taarifa rasmi iliyoifikia meza yake kuhusiana na madai yao.

No comments:

Post a Comment