01 March 2011

Hatma kesi ya Mpendazoe Alhamisi

Na Kulwa Mzee

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania inatarajia Machi 3, mwaka huu kutoa uamuzi wa ama kumruhusu aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo la Segerea kwa tiketi ya
CHADEMA, Bw. Fred Mpendazoe kulipa sh. milioni 15 au kutupilia mbali kesi yake kwa kuwa yuko nje ya muda.

Kesi hiyo ilikuwa inaendelea jana mbele ya Jaji Ibrahim Juma ambapo Wakili wa Mpendazoe, Bw. Peter Kibatala alikuwa tayari na mteja wake kulipa kiasi hicho cha fedha kwa mujibu wa sheria.

Baada ya kuwasilisha hoja ya kulipa sh. milioni 15, Wakili wa Mbunge wa Segerea, Dkt. Makongoro Mahanga, Bw. Jerome Msemwa aliwasilisha hoja ya kupinga kulipwa kwa fedha hizo hadi mahakama iangalie ni kiasi gani kinapaswa kulipwa na kwamba walalamikaji wako nje ya muda.

Hoja hiyo ilipingwa na Bw. Kibatala ambaye alisema Wakili Msemwa hana hoja ya msingi na kwamba malipo hayo yako kisheria, hivyo yalipwe na mwisho wa kesi wakishindwa watakaofaidika nazo ni walalamikiwa.

Alisema fedha zinatakiwa kulipwa zote, hivyo aliiomba mahakama kuruhusu malipo hayo yafanyike ili kesi ya msingi iendelee kusikilizwa.

Jaji Juma baada ya kusikiliza malumbano hayo ya kisheria aliahirisha kesi hadi Machi 3, mwaka huu kwa ajili ya kutoa uamuzi.

Wadaiwa katika kesi hiyo ni Mbunge wa Segerea, Dkt. Mahanga (CCM), Mwanasheria Mkuu wa serikali na Msimamizi wa Uchaguzi.

Bw. Mpendazoe alifungua kesi hiyo Namba 98 ya mwaka jana, akilalamikia ukiukwaji wa taratibu na sheria za uchaguzi katika jimbo hilo, analalamikia mwenendo mzima wa uchaguzi, mchakato wa uchaguzi katika jimbo hilo kwamba vilikiuka taratibu na sheria za uchaguzi.

Pia, anadai mwenendo wa ukusanyaji kura ulikuwa mbovu na ujumlishaji wa kura, kuhesabu na utangazaji wa matokeo ulikiuka taratibu na sheria za uchaguzi.

Anaiomba mahakama hiyo itengue ubunge katika jimbo hilo na kuamuru ufanyike uchaguzi mdogo au atangazwe yeye kuwa mbunge.

Awali, Bw. Mpendazoe aliomba mahakama hiyo imsamehe malipo ya sh milioni 15 (sh milioni 5 kwa kila mlalamikiwa) kwa kuwa hana uwezo huo, lakini ombi hilo lilitupiliwa mbali na mahakama, ikidaiwa ni hitaji la kisheria.

No comments:

Post a Comment