17 January 2011

Villa kucheza mechi kibao za kirafiki

Na Shaban Mbegu

TIMU ya Villa Squad, imepanga kucheza mechi nyingi za kirafiki ili kujiandaa vyema Ligi Daraja la Kwanza hatua ya Tisa Bora iliyoapangwa kuanza Januari 30 mwaka huu.Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Ofisa habari wa
Villa, Idd Godigodi alisema kwa sasa timu yake inaendelea na mazoezi ya kila siku ambayo yanafanyika kwenye Uwanja wake uliopo Jangwani.

"Katika kuhakikisha tunarudi Ligi Kuu msimu ujao, tumejipanga kuhakimisha tunacheza michezo mingi ya kujipima nguvu ambayo tuna imani itatusaidia katika hatua ya Tisa Bora," alisema Godigodi.

Godigodi alisema hadi sasa tayari wamecheza mechi 10 za kirafiki lakini wanatarajia kucheza mechi nyingine nyingi zaidi kwa ajili ya kujiimarisha kabla ya kuanza kwa Ligi hiyo.Alisema wameamua kuiandaa vyema timu hiyo kutokana na katika hatua hiyo ya Tisa Bora, timu nyingi zimejiandaa vizuri na kila moja inataka kucheza Ligi Kuu.

Timu zinazotarajiwa kucheza ligi hiyo ni TMK United, Villa, Moro United za Dar es Salaam, Polisi Morogoro, Moran ya Manyara, Coastal Union ya Tanga, Oljoro JKT ya Arusha, Rhino ya Morogoro na Prisons ya Mbeya zinatarajiwa kutoa nne zitakazocheza Ligi Kuu msimu ujao.

No comments:

Post a Comment