17 January 2011

Savio yaendeleza wimbi la ushindi

Na Amina Athumani

MABINGWA watetezi wa Ligi ya Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (RBA), Savio imeendeleza wimbi la ushindi katika mashindano ya ligi hiyo yaliyofanyika jana Uwanja wa ndani Taifa, Dar es Salaam ambapo timu hiyo
iliibuka na ushindi wa pointi 77-41 dhidi ya TP Stars.

Mabingwa hao ndiyo wanaoongoza katika msimamo wa ligi hiyo kwa kushinda michezo yote mitatu, iliyocheza tangu kuanza kwa ligi hiyo ambapo katika mchezo wa jana hadi kufikia mapunziko Savio ilikuwa ikiongoza kwa pointi 30-18.

UDSM ambayo ilizuiwa kuingia uwanjani wiki iliyopita kutokana na kutokamilisha taratibu za usajili wa wachezaji wake, jana ilifungwa na Tanzania Prisons kwa pointi 78-60. Timu hiyo iliruhusiwa baada ya kukamilisha usajiliwa wake.

Katika mchezo mwingine Vijana, iliibuka na ushindi wa pointi 60-55 dhidi ya Oilars huku, Chang'ombe United ikiilaza Airwing kwa pointi 82-55.

Akizungumzia michuano hiyo, Mkurugenzi wa Mashindano Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BD), Zabron Manase alisema ligi hiyo inaendelea vizuri ingawa bado mdhamini wa mashindano hayo hajapatikana.

"Tangu ligi hii ilipoanza wiki mbili zilizopita, tunaiendesha kama BD na hatujapata mdhamini yeyote hadi sasa hivyo tunaomba wadau wa mpira wa kikapu kujitokeza, ili kuidhamini ligi hii kwani timu zote zimeonesha ari ya kwa kushiriki kwa moyo mmoja bila ya kinyongo cha kukosa mdhamini," alisema Manase.

No comments:

Post a Comment