28 January 2011

Msuya: Kuna uwezekano CCM kung'olewa

Na Tumaini Makene

WAZIRI Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Bw. Cleopa Msuya amesema kwa jinsi vuguvugu la kisiasa lilivyo kwa sasa nchini, si ajabu chama kingine
tofauti na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuchukua hatamu za kuongoza serikali.

Mbali na hilo, Bw. Msuya  (80)  amesema ni wazi kama hatua za dhati hazitachukuliwa kuweka mfumo mzuri wa kutatua matatizo ya wananchi, hususan vijana, hali kama iliyotokea nchini Tunisia na katika nchi nyingine za Misri, Algeria na Ivory Coast, inaweza kutokea Tanzania.

Lakini ameonesha matumaini kuwa mjadala wa katiba mpya ambao Serikali ya Rais Jakaya Kikwete imeuridhia, utasaidia hali kama hiyo isitokee kwani baadhi ya mifumo inayoweza kuepusha itajadiliwa kwa kina na hata  kuwekwa katika katiba, kwa manufaa ya Watanzania.

Kwa mujibu wa Bw. Msuya, katika mjadala unaonedelea nchini juu ya katiba mpya, ni vyema ikafikiriwa kama kuna haja ya kuendelea kuwa na bunge moja, huku yeye akipendekeza kuwapo wa mabunge mawili, kama ilivyo nchini Uingereza.

Mzee Msuya aliyasema hayo juzi,  alipofanya mahojiano maalum na magazeti ya  Kampuni ya Business Times Ltd, inayochapisha Majira, Business Times, Dar Leo na Spoti Starehe, nyumbani kwake jijini Dar es Salaam.

Akionekana kufurahishwa na namna Watanzania wengi wanavyoonesha utayari wa kutafuta maisha, alisema hiyo ni changamoto kwa serikali kwani inao wajibu wa kuonesha njia sahihi na kuweka mazingira bora ya wananchi wake kutumia fursa nyingi zilizopo.

Pamoja na kuisifia serikali katika baadhi ya maeneo, huku akionesha imani kuwa inaweza kurekebisha ili kulikwamua taifa hasa kwa kutumia fursa anuai ambazo Tanzania imebarikiwa kuwa nazo, Bw. Msuya alionekana kushangazwa na kusuasua kwa ushughulikiaji wa mambo muhimu kiasi cha kuzua minong'ono kwamba 'kuna mkono wa mtu hapo.'

Maendeleo yatokane na vipaumbele

Mzee Msuya alisema kuwa Tanzania ina kila kitu kinachoweza kuifanya nchi yoyote kuendelea kiuchumi, akisema "kwa mfano kwa nini tusiwe Qatar ya Afika Mashariki kwa kuzalisha gesi na kuweza kuuza gesi yetu ya asili kwa majirani. Mwalimu alisema kupanga ni kuchagua."

Akifafanua suala la umuhimu wa vipaumbele katika kuiwezesha nchi kuendelea, Bw. Msuya alisema kuwa haiwezekani maendeleo kupatikana kwa kufanya kila kitu kwa wakati mmoja.

"Unajua masuala ya maendeleo you need (unahitaji) kupanga, Mwalimu (Nyerere) alikuwa akisema kupanga ni kuchagua...ukijaribu kufanya kila kitu kwa wakati mmoja huwezi, lazima uwe na specific (malengo) target on some issues. Nitawapatia mfano...

"Kuna wakati baada ya uhuru serikali iliamua kutumia fursa za kiuchumi kwa majirani zetu, ndani ya muda fulani tukaamua kujenga reli ya TAZARA kwenda Zambia kwa msaada wa Wachina, tukajenga barabara ya lami kwenda huko mikoa ya kusini na tukajenga bomba la mafuta, TAZAMA, ilikuwa ni mipango ndani ya muda fulani, mnaacha mengine mna-concetrate.

"You have to select priorities  (lazima uwe na vipaumbele). Imekuwa ikiniuma sana mimi, lakini ni changamoto, maana sasa tunazo raslimali zaidi kuliko tulivyokuwa wakati ule, tunao watu, lakini results  (matunda) hayaonekani, sisi sio landrocked  kama walivyo baadhi ya majirani zetu, sisi si nusu jangwa kama kama Kenya kwa mfano.

Huku akinukuu maneno ya Balozi wa Ujerumani, Bw. Guido Hertz, ambaye aliwahi kuhojiwa na gazeti moja nchini na kuonesha mshangao juu ya umaskini uliokithiri wa Watanzania pamoja na utajiri wa raslimali zilizopo, akisema "ni vigumu kuelewa wala kuielezea hali hii," Mzee Msuya aliongeza;

"Tuna kila kitu kinachohitajika...kuna haja ya kujitazama upya, tuna raslimali za kila aina zikiwemo za asili, are we putting them on the best use  (tunazitumia inavyostahili ?)...tuna gesi ya asili, tuna akiba ya kutosha ya dhahabu, utalii pia...kuna hili ka kilimo kwanza, serikali imeshatamka ingawa kwa kuchelewa kidogo.

"Lakini nalo hatujalianza vizuri (la kilimo kwanza) kwa sababu hiyo hiyo ya kutopanga na kukosa vipaumbele...viwanda ni muhimu, suala la umeme ni critical (tatizo sugu) sasa lakini kuna possibilities (uwezekano) wa kugeuza coal (makaa ya mawe), umeme wa upepo na ule wa Rufiji ambao unazidi hata mahitaji yetu," alisema na kuongeza.

"Kinachotakiwa ni vipaumbele...sasa tuna raslimali watu ambazo zina ujuzi, maarifa na mafunzo. Suala la infrastructure (miundombinu)...ingawa serikali imejitahidi katika hili kwa kujenga barabara nyingi, lakini kuna tatizo la usafiri wa reli. Kuna kila haja ya kushughulikia reli ya kati, TAZARA na reli ya Tanga.

"Tujenge hizo ili mizigo kutoka bandarini isafirishwe, nasikia sasa wanajenga bandari sijui wapi, nyingine ya nchi kavu hapa...suala si kujenga bandari za nchi kavu, muhimu ni kujenga reli ili tuweze kuzifikia nchi jirani...ni changamoto ya kuanza kwa kutumia fursa zote hizo.

"Mimi nafurahi sana siku hizi unawaona Watanzania wanahangaika huku na huko, kila ukipita...hata hii ya machinga ni namna gani wananchi wanajitahidi, tunapaswa kuiona hiyo kama changamoto si laana, maana yake ni kuwa wananchi wako tayari kwa mabadiliko ya haraka, serikali inapaswa kusaidia hapo.

"Tufufue miundombinu yetu, hasa reli, spirit (ari) ya ujenzi wa barabara iliyopo sasa iendelezwe...concetrate on few key issues (kujikita katika mambo machache ya msingi)  lazima tujue hilo...lazima tujue tunaondoka vipi kwenda mbele baada ya miaka 50 ya uhuru," alisema Bw. Msuya, ambaye pamoja na umri wa miaka 80 bado anaonekana kuwa na nguvu.

Akijibu swali juu ya ukuaji wa uchumi kitakwimu na kuongezeka kwa umaskini miongoni mwa wananchi walio wengi, alisema pamoja na kuwa serikali haiwezi kuwawekea watu fedha mfukoni, isipokuwa mpaka wanapojishughulisha kwa ajili ya kujipatia kipato, serikali inapaswa kuweka mazingira maridhawa ya shughuli hizo.

Alisema ni watu wachache wanaoweza kupata ajira rasmi za ofisini katika sekta ya umma na binafsi, kwani wengi wa Watanzania wanapata ajira katika kilimo, lakini tatizo limekuwa ni bei ndogo.

"Katika kilimo watu wetu wanajishughulisha kweli, lakini tatizo limekuwa ni bei ndogo, ukiulizia tatizo ni nini utakuta ni gharama za usafiri, tunahitaji kwenda kwa kasi...ndiyo maana nikasema masuala ya miundombinu ya uchukuzi ni muhimu.

"Kwa mfano hakuna haja ya soko kuwa Dar es Salaam tu, kila mkulima aje kupata soko hapa, mkulima aliyeko Rukwa anaweza kuuza nje ya nchi Zambia huko," alisema Mzee Msuya.

Akizungumzia juu ya mazingira ya uwekezaji nchini, alisema kuwa ni mazuri lakini kuna kila haja ya kujikita na kuweka kipaumbele katika miundombinu ya reli na bandari na upatikanaji wa umeme wa uhakika na rahisi, sambamba na mawasiliano ya elektroniki, ili kujiongezea uhakika na uwekezaji.

Alisema hata jiografia ya Tanzania ni fursa ya kipekee inayoweza kutumiwa na nchi kunufaika kiuchumi kwani inazungukwa na nchi nane, ambazo nyingine hazina bahari wala ziwa, hivyo kutokuwa na bandari, hali ambayo inazifanya kutegemea nchi jirani kama Tanzania.

"Miaka 30 iliyopita Dubai haikuwa lolote, it was just a small..., lakini wameibadilisha kuwa moja ya miji mikubwa kama Singapore. Miaka 50 ijayo Tanzania inao uwezo kabisa wa kuwa nchi yenye uchumi wa kati, tunaweza kuweka malengo ya kuwa kama Korea Kusini, hata kama hatutawafikia kabisa, lakini tunaweza.

Mjadala wa katiba mpya

Katika suala la katiba mpya, Mzee Msuya alisema kuwa kuna kila haja ya vyombo vya utendaji kazi hasa vile vya kisheria kufanyiwa mabadiliko ili vifanye kazi inavyopaswa.

Pia alisema ni wakati mwafaka katika mjadala wa katiba mpya, Watanzania waanze kufikiria iwapo kuna haja ya kuendelea kuwa na bunge moja, huku yeye akionea mfumo wa mabunge mawili, ndiyo unafaa kwa sasa nchini kutokana na wabunge kupatikana kutoka katika makundi mbalimbali ya kijamii nchini.

"Sasa hata wasomi wanakimbilia kwenye siasa...tunao wabunge wanatokana na NGO sijui wapi huko, hivyo ni vyema watu wakafikiria hilo.

12 comments:

  1. Asante Mzee wetu Msuya kwa mawazo mema! Najuwa kuna watu wengi kama mimi watakupongeza, ila pia wapo wachache watakuponda kuwa ulikuwa wapi muda wote usiyatie vitendoni uliyoyasema! lakini nawakumbusha kuwa muda umebadilika, mazingira ya siasa uchumi, jamii, sayansi na technology vimebadilika kiasi kwamba kwa muda uliopita ingekuwa vigumu kutekeleza haya anayoyawaza leo Babu yetu Mzee Msuya. Mungu akujalie afya njema bado tunakuhitaji ushauri wako! Napenda pia gazeti la Majira mkatutafutie Mzee Mkapa na Mwinyi nao watusaidie kutoa maoni yao, kina Salim nk muwe na ziara hizi za mahojiano mlizozianza.

    Kuna mambo mengi ya Msingi aliyoyaongea Mzee Msuya. Mi nataka nigusie suala moja ama mawili!

    1. KATIBA

    Ni kweli tunahitaji mabadiliko makubwa ya katiba, si kama ilivyotaka kufanywa na Werema kuwa tufanye tu marekebisho katika maeneo huku wengine (Waziri Mwenye dhamana) akidai hatuna hela ya kuandika katiba mpya! Mimi nachotaka kusema ikiwa kama haya wananchi wanayoyataka kutokea ndani ya katiba yatapuuzwa basi wanachi wenyewe watajitawala hivyo gharama tunazozikwepa kuandika katiba mpya kwa kuwashirikisha wao wenyewe kwa kuchaguwa muundo wa ushiriki wao, gharama zake zitakuwa kubwa zaidi kuliko hizi tunazijitahidi kuzikwepa sasa hivi.

    Mjadala huu umeshajadiliwa na hatimaye Mbivu na mbichi tayari zimeonekana. Mimi ninamtazamo kuwa katiba hii lazima iandikwe upya, yale ya msingi kwenye katiba ya zamani tutayachukuwa na yale yanayohitajika kuingizwa kwenye katiba mpya tufanye hivyo. Ila yale yoote yasiyofaa tuyaondolee mbali!

    Mfano wajibu na Mipaka ya kazi kwa vyombo vya Ulinzi na Usalama bila kuacha hata chombo kimoja viwekwe wazi, Ukaguzi wa kimahesabu katika madaftari yao ya fedha yawekwe wazi, vyanzo vyao vya mapato na matumizi vielezwe kwa kina ili kuleta matumizi bora ya ofisi hizo, na pia kuondoa ukiritimba wa matumizi mabaya ya ofisi dhidi ya wenyewe kwa wenyewe ndani ya kila taasisi hizo.

    Huko ndiyo lazima tufike ili katiba mpya iwe na maana. Vinginevyo siasa yetu na Democrasia tunayoitaka hatuwezi kuifikia hata mbadilishe na mwandike katiba mara 100! Haiwezekani Chama kilichoko madarakani ambacho kimeniteua mimi leo nikiangushe kisa eti democracy, katika akili ya kibinadamu ya kawaida tu hili linahitaji usmart wa kutukuka!

    Unakuwa na uhakika gani huyo anayeingia hawezi ku hatarisha nafasi yako? Je matumizi ya pesa huku kwangu yamekaaje, Mhe Rais ananilinda kwa kiwango gani nk? Ni vitu vinavyofanya Democracy yetu icheleweshwe kukua kwa makusudi!

    Suala la katiba kumpunguzia mamlaka Rais ni jambo la muhimu, lakini vile vile mamlaka haya tuangalie tunamkabidhi nani, Ni Bunge au Mahakama! Faida na hasara ya kukabidhi mamlaka hayo kati ya vyombo hivyo viwili yote lazima vizingatiwe! Lazima tuondokane na Rais Mfalme, ni vizuri tumepata marais wote wastaarabu, ikija tukapata Rais mwendawazimu hapo mbeleni Ivory Coast, au Zimbabwe nk itaingia Tanzania.

    By Carwin 1

    ReplyDelete
  2. 2. UKUAJI WA UCHUMI
    Katika ukuaji wa uchumi takwimu zinatupa matumaini lakini hali bado ni tete sana nchini. Ukija ndani ya jiji la Dar es Salaam kuna matatizo kibao, Ukienda nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam au nje kidogo ya miji yote nchini hali si nzuri katika uhakika wa chakula, malazi bora, makazi, huduma za afya, upatikanaji wa elimu nk! Matatizo ni mengi japo pia zipo jitihada mbali mabli zilizofanyika katika kila sekta hali ni nafuu zaidi kuliko huko tulikotoka! Isipokuwa tu tumeshindwa kutafsiri hali ya uchumi kwa maisha ya watu wetu!

    Matumaini niliyokuwa nayo juu ya awamu hii mpya ya 4 ilikuwa ni kutransfom uchumi wa takwimu na uchumi mkuu kama alivyoujenga Mhe: Ben Mkapa kwa Wananchi wa kawaida kama ahadi ya Mhe: Jk alivyoitoa wakati anahitaji kwa mara ya kwanza kuingia Ikulu! Sote tulimwamini kwa hilo, pengine bado anahitaji muda!

    Kwa mawazo yangu, mimi nadhani hatujakosea ku introduce "Kilimo kwanza" kimekuja japo kwa kuchelewa lakini bado hatujakitia vitendoni kwa dhati kabisa kama Mhe: Pinda anavyohitaji tufanye. Nadhani wasimamizi bado hawajajipanga ingawa kila mmoja wao anauimba wimbo wa kilimo kwanza nadhani pengine kwa kumfurahisha PM ambapo haisaidii!!

    Nilitafsiri hivi wakati Jk anatoa ahadi ya kuupeleka uchumi mkuu mikononi mwa wananchi wa kawaida kwamba!

    a. 80% ya Watanzania ni wakulima, waliobakia na wafanyakazi na wachuuzi wachache!

    b. Zaidi ya 45% ya GDP inatokana na Kilimo

    Hivyo nikadhani sasa kama serikali lazima tuwe focused na kilimo! Kwamba, lazima watanzania wale 80% waguswe na sera za Kilimo kwa kuandaa mazingira bora ya kuvutia wawekezaji katika viwanda vya kati na vikubwa kwa ajili ya usindikaji wa mazao ya kilimo. Iwe nyama, ngozi, nyanya, matunda, mahindi, ngano, korosho, pamba nk tuyaongezee thamani tuanze kutumia mazao yetu wenyewe kama soko la ndani lakini na ziada tuuze kwenye soko la Afrika Mashariki na nyingine masoko ya nje zaidi! Hili lingeongeza Fedha za kigeni, ajira, kuboresha maisha ya watanzania, kupunguza utegemezi wa bajeti yetu nk!

    Lakini viwanda haviwezi kuwepo kama, wawekezaji hao hawatakuwa na uhakika wa upatikanaji wa malighafi, mfano kama tuna lima kwa kutegemea mvua ina maana tunalima kwa msimu, hivyo inamaana kuwa hata malighafi itapatikana kwa msimu halafu kiwanda kitafungwa msimu ukisha malizika. Nikadhani tafsiri ya serikali sasa ni kuhakikisha inaweka program ya uchimbaji visima kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji maji nchi nzima, ili malighafi isikosekani na viwanda viwe endelevu! hii pia ingeongeza ajira ya uhakika katika kundi kubwa la watanzania hasa vijana!

    Bila kusahau viwanda vidogo vidogo vingeweza kupewa msukumo wa kipekee kwa kuhakikisha vinaandaliwa mazingira bora ili watu binafsi nchini wasindike bidhaa zao na kuziuza hapa nchini na ziada kuuza nje katika soko wanaloweza kulifikia.

    Serikali jukumu lake kubwa ni kuandaa mazingira tu, na kuwasaidia watanzania kutafuta masoko na kuwasaidia kukabiliana na changamoto za kisoko huko wanapopeleka mazao yao na kupunguza ama kuondoa kabisa changamoto hizo kwa kushirikiana na wadau wote wa kilimo na ufugaji!

    Tanzania bila umasikini inawezekana kama tutajipanga vizuri, tudhamirie hasa kusaidiana kuleta maendeleo ya pamoja!

    Uchumi ni mpana na wapi tunaweza kusaidiana kurekebisha inawezekana tukaambizana lakini kwa leo natoa maoni haya machache niwape pia wenzangu nafasi ya kutoa maoni yao!

    Asanteni

    By Carwin 2

    ReplyDelete
  3. Inatia moyo kuona wazee waliokuwa viongozi wa ngazi ya juu katika nchi hii wanaacha utamaduni wa kinafiki na kuongea ukweli unaowagusa wananchi. Hii inakupa heshima ya kipekee Mzee Msuya kwa vile mojawapo ya matatizo yetu ni viongozi kutthubutu kueleza ukweli. Na pale wanapoeleza ukweli na kuachana na woga au unafiki wa kijinga (kama waliojitokeza kupinga malipo ya Dowans) wanabezwa, kuzomewa na hata kutishwa na vigogo wenzao ambao ni wanafiki watupu. Vigogo waogopao ukweli kama anaoutoa Mzee Msuya ni mazuzu wasio wasafi hata kidogo.

    ReplyDelete
  4. Bora CCM ingolewe. Imeshapitwa na wakati na viongozi wake wamejaa kiburi na kujiono watadumu milele. CCM imeifikisha hii nchi mahali pabaya na kamwe hakutakuwa na njia ya kujinasua hapa tulipo iwapo chama hicho kiovu kitaendelea kuiongoza nchi hii.

    ReplyDelete
  5. Kwa kweli nimefurahishwa na mjadala huu wa mzee Msuya. Huyu ni mzee kwa kuigwa. Vipao mbele vya serikali yetu viko wapi? Kweli enzi zao na mzee nyerere walikuwa na vipaombele. Hata kama hawakufanikisha yote lakini waliacha reli zinafanya kazi. Ndege za ATC, bandari za Dar, Tanga na Mtwara. Viwanda vya nguo, nk.

    Waliomfuata walitakiwa kuangalia mapungufu na kurekebisha. Kama waliamua kubinafisisha huduma fulani, walitakiwa kuhakikisha wanawasimamia kwa mikataba yenye kuwasaidia wananchi.

    Hili la gasi linaniuma sana. Huwa nasikitika sana kuona malori ya mkaa unaoingia Dar kila siku. Ukipiga hesabu ni malori mangapi ya mkaa yanateketezwa kila mwaka. Kama tumepata bahati ya kuchimba gesi, uko wapi mpango wa kuacha kutumia mkaa na kuni? Tunamaliza misitu, huku dunia inalia na joto linaloongezeka. Tutaenda wapi? mvua zimepungua sana, joto limeongezeka na mavuno ya mkulima yamepungua sana. Bei za vyakula zimepanda kwa vile chakula hakitoshi.

    Tuuzieni basi gesi ya songo songo tupikie kama hamuwezi kutengeneza umeme wa kutosha?

    ReplyDelete
  6. Na kwanini ising'olewe? Unategemea nini kutoka chama kinachoendeshwa na watu kama akina Yusufu na akina Joni? Jeuri yao haiwapeleki popote ila shimoni.

    ReplyDelete
  7. Mzee MSUYA tunaomba utuulizie yale mshirika yaliyokuwa yana vuma ezi hizo kama SUDECO, NASACO nk kaburi la haya mashirika yako wapi? Kipindi hicho namba zake zilikuwa SU soma ule siku hizi ni TZ. CCM hata ife tutadai tu hata wajuu.

    ReplyDelete
  8. Hawa akina Yusufu na Joni dawa yao iko jikoni. Wanatakiwa kujifunza kutoka kwa wenzao, wanatia jeuri sana utafikiri wao ni miungu.

    Angalia Tunisia na yule anayejifanya kidume kule Ijipti yanayomtokea leo hii. Majeshi yao na masilaha kibao hawaoni ndani dhidi ya wanyonge. Wasije wakasingizia kuwa Ni Chadema au Dini vinapelekea kutokea yale tuyaonayo kule Ijipti.

    Vilio vya watanzania ni sawa na Ijipti, Tunisia na sehemu nyingine. Sisyemu wanajaribu kuyadinisha haya mambo ili watu wapuuze. Hiyo ni mbinu pori, utafika muda hata wanasisyemu wenzao watawageuka.

    Hao efuefuyuu na polisi wanapata mishahara kiduchuu. Wanaponea uporaji, wizi na dhulma za hapa na pale ili kusavaivu. Ndiyo marupurupu yao hayo.

    Iko siku wewe Usufu Makamba nitakupika kikwenzi. Kama sio wewe wanao na ndugu zenu wataipatapata. Tunajenga visasi. Ni ninyi mnaotufanya hivyo.

    ReplyDelete
  9. Nyie Watanzania mbumbumbu,kila jambo lazima mseme maneno ya hovyo,huyo mzee kazungumzia mambo elekezi sana badala ya kuchangia aliyosema mnaanza ccm iondolewe madarakani kitu ambacho kwa sasa hakiwezekani mpaka miaka mitano imalizike,la muhimu mzee huyu kazungumzia kuna umuhimu mkubwa kwa vyombo vya sheria vifanyiwe mabadiliko makubwa ni jambo la muhimu sana,nchi hii inakosa usimamizi wa waliopewa madaraka,mahakimu,majaji,mawakili,polisi na vyombo vingine vya kusimamia sheria havifanyi kazi ipasavyo,bila kuwa na muono mbali hata tukibadilisha katiba mara mia mambo yatazidi kuwa hovyo,watanzania wengi mabadiliko ya katiba wanayozungumzia ni yale yanayotamkwa na wanasiasa lakini ambayo yanamuathiri mwanasiasa lakini yeye mtz ukimwambia nini kinakusibu kwenye katiba ya zamani hajui lolote,tunalo tatizo kubwa katika vyombo vya kusimamia sheria,kwa kweli vinahitaji udhibiti wa hali ya juu na utendaji kazi wake pia udhibitiwe hasa katika kushughulikia matatizo na malalamiko ya wananchi. FIKIRI UCHANGIE HOJA YA KUBORESHA KATIBA USIJIDANGANYE AU USIDANGANYWE NA WANASIASA CCM ITAONDOKA MADARAKANI KABLA YA 2015

    ReplyDelete
  10. Naweza kusema alichoongea Mzee wetu Cleopa Msuya ni sahihi kabisa.
    Kwanza chama tawala inabidi kijitazame upya, kwa kuwa ndio wameshikilia muhumili mkuu wa taifa letu kwa muda mrefu.
    Mbali na taifa letu kuwa na rasilimali nyingi katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, nchi yetu imekuwa moja ya nchi fukara zaidi duniani na hali hiyo imesababishwa na uongozi mbaya wa viongozi wa chama cha mapinduzi.
    Kuna suala kama la mgawo wa umeme, limekuwa ni suala la muda mrefu linalosumbua nchi yetu, mbali na nchi yetu kuwa na vyanzo vingi vya nishati hiyo muhimu.
    Hali hiyo imekuwa ikitetewa na viongozi kuwa mtikisiko wa uchumi duniani, kitu cha kujiuliza ni kwamba mbona nchi nyingine zinazotuzunguka na hazina vyanzo vingi vya nishati kama Tanzania hatusikii tatizo la mgao wa umeme?

    ReplyDelete
  11. Tatizo la Tanzania,kama ilivyo kwa ncgi nyingi za Dunia ya Tatu,ni kuwa na utajiri wa maneno lakini uhaba wa vitendo.Imagine Msuya wakati akiwa madarakani angejaribu kutekeleza kwa vitendo japo robo tu ya haya anayohubiri sasa,Tanzania ingekuwa wapi hivi sasa.

    Na japo anastahili pongezi kwa aliyosema,bado kuna elements za unafiki ambapo anauma na kupulizia.Nusu anataka kueleza ukweli lakini wakati huohuo anakwepa kuwalaumu watawala waliopo madarakani,in fact anawasifia,ilhali sote tunatambua kuwa viongozi tulionao sasa wamedhamiria kukwangua hata kile kidogo kilichoachwa (kwa bahati mbaya?) na akina Msuya.

    Sidhani kama kuna Mtanzania anayehitaji lecture kutoka kwa watu kama Msuya ambao kwa kiasi kikubwa ndio chanzo cha nchi yetu kugeuka shamba la bibi na laughing stock (kwa umasikini wa kupindukia licha ya utajiri lukuki tulionao)

    ReplyDelete
  12. we evarist makamasi kweli yani umeshindwa hata kusoma alichosema unaropoka tuu...hujui kipindi cha mwl..kilifanyika nini alipoainisha TAZAMA NA TAZARA kwa mifano hukuelewa...unalinganisha na nini kilichofanyika sasa? Msiwe mnakurupuka tuu...
    Wewe kama ni kada wa CCM ambao kila kukicha kukosolewa kwenu ni vita! we Kalaghabao!!

    ReplyDelete