28 January 2011

Kushuka ufaulu "form IV" hatari kwa maendeleo ya elimu-CWT

Na Gladness Mboma

CHAMA cha Walimu Tanzania  (CWT),  kimesema kiwango cha ufaulu kwa  daraja la kwanza hadi la tatu ni kidogo na hakifanani na matokeo ya
miaka iliyopita, jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo ya elimu nchini.

Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw. Ezekiah Oluoch aliyasema hayo Dar es Salaam jana alipozungumza na Majira ili kutoa ufafanuzi juu ya shule za serikali  kufanya vibaya katika mtihani wa kidato cha nne mwaka huu wakati shule binafsi, zikionekana kufaulisha wanafunzi wengi zaidi.

Alisema wanafunzi waliofanya mtihani huo na kupata daraja la kwanza hadi la tatu mwaka huu walikuwa asilimia 11 wakati mwaka 2010 walikuwa asilimia 16, hivyo ni wazi kuwa mwaka huu, wanafunzi wamefeli kuliko kawaida,” alisema Bw. Oluoch.

Alizitaja sababu zilizochangia matokeo mabaya mwaka huu kuwa ni pamoja na shule za kata kuwa na mwalimu mmoja au wawili hivyo wanafunzi wanaosoma katika shule husika, hawafundishwi ipasavyo na kugeuza shule hizo kuwa vijiwe vya mazungumzo.

Alisema hawategemei miujiza ya wanafunzi kufaulu wakati shule hazina walimu, na kwamba wanafunzi wa shule binafsi, wakifanya biashara, hivyo kuhakikisha elimu inayotolewa ni bora ili kuvutia wanafunzi.

“Pamoja na kwamba shule binafsi hazina walimu wa kutosha na wengi wao hawana taaluma ya ualimu, lakini wana sifa za kufundisha,” alisema.

Shule za serikali zimefanya vibaya kwa sababu ya ukosefu wa vitabu wakati zile za binafsi licha ya kwamba wanatoza karo ya juu, lakini wazazi bado wanawanunulia watoto wao vitabu.

Bw. Oluoch aliongeza kuwa, shule nyingi za serikali zipo vijijini katika mazingira duni wakati shule binafsi, zipo mjini na mazingira ya shule husika ni mazuri.

Alisema wanafunzi wa shule binafsi wanafaulu kwa sababu wanasoma masomo ya ziada muda wa jioni baada ya kutoka shule ambapo wanafunzi wa shule zinazomilikiwa na serikali baadhi yao wanasoma kidato cha kwanza hadi cha nne wakiwa majumbani.

Kitu kingine ambacho kinachangia shule binafsi kufanya vizuri ni kumaliza silabasi mapema wakati baadhi ya shule za serikali zikishindwa kumaliza kwa wakati.

Bw. Oluoch alitaja sababu zingine zinazochangia wanafunzi wa shule za serikali kufeli masomo yao kuwa ni pamoja na darasa moja kuwa na wanafunzi karibu 100 ambapo katika baadhi ya shule, mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 300, wakati shule binafsi mwalimu mmoja anafundisha watoto 40.

“Hakuna uwiano na shule za serikali, zitaendelea kufanya vibaya na zitabaki kuwa shule za watu maskini, wasitegemee hata siku moja zitafanya vizuri kama serikali haitarekebisha kasoro zilizopo,” alisema.

Alisema serikali ikae na kutafakari ni jinsi gani wataweza kuepusha mazingira hayo magumu katika shule za kata walizozianzisha kwa kuwalipa na kuwapa motisha walimu ili waweze kuwa na moyo wa kufundisha

9 comments:

  1. Hii hali haina mkakati wowote kwa kuwa hizo shule za kata ni kwa ajili ya watoto wa maskini na wakipato cha chini.
    Walioanzisha hizo shule za kata watoto wao hawasomi kata na wala hawatakaa wasome kata, watoto wao wanasoma shule za binafsi zenye waalimu na huduma zote, na wanalala huko,kero hawana,na ndo wanaofaulu.
    Shule gani za kata,waalimu hawajaliwi hata chembe,nani kaona shule ya sec ina mwalimu mmoja,ndo watoto wafaulu?
    Hizo bil.za dowans watengeneze mazingira mazuri ya shule na waalimu matokeo yatabadilika.wakae 40 drsn na mwalimu apate motisha wake. nenda marian ukaone,waalimu wanapewa motisha sasa hivi kwa kuwa kila mwaka wanakuwa kumi bora.
    Jamani, watoto wa mabosi wote wanasoma private,na harambee zao huko wanatoa kubwa kubwa,wasituvunge,tunawaona.
    Hiki ni kilio cha maskini na shule zao za kata!!!!!!!!

    ReplyDelete
  2. Serikali na wizara ya Elimu oneni aibu jamani, hivi mnafikiri matabaka mnayoyajenga yatakuwa na faida?
    Watoto wote wana haki ya kuelimishwa.

    ReplyDelete
  3. Lakini kwa nini tunaionea serikali peke yake? Hivi wabunge wetu wanafanya nini? Au wao wakilipwa posho tu wanaridhika?
    Wao wanaona nini? au Tuliwachagua wakaishi Dar?

    Nasikitika wabunge wetu wasivyo na huruma na nasikitika wengine tumewachagua tena wakale posho yao Dodoma.

    Sikuwahi kufikiri shule yenye wanafunzi karibu 100 wanakosa divion I, II na III. Wanafunzi wa kwanza shuleni wamepata division IV na 0. Jamani tutafikia maisha bora kwa kila mtanzania? Tutaacha kulima kwa jembe la mkono? Tutaacha kuponda kokoto? Tutaacha kuokota maplastiki?
    Hiki kizazi cha wanaofeli kitakapofikia kuwa wazazi watakuwa na hali gani? Au ndio mnatengeneza kundi la kutawaliwa?

    ReplyDelete
  4. Mi nashauri serikali kwa gharama zake iwasomeshe wanafunzi wote waliofeli miaka miwili tena wafanye mitihani upya.
    Hatuwezi kutoa michango mingi kiasi hiki kwenye shule za kata halafu wanafunzi wanaishia na Ziro.

    Gharama za kumsomesha mtoto shule ya kata ni sawa na private. Kuna michango kibao. Ulinzi, mitihani, test, makaratasi, chakula, n.k.

    Wabunge tuoneeni huruma. msisubiri tuwaletee barua rasmi kama wengine nimewasikia. wanataka mpaka wapelekewa barua rasmi ya matatizo ya wananchi.
    Tuoneeni huruma wananchi tuliojipinda kuwasomesha watoto wetu kwenye shule za kata. Hatuna uwezo wa kuwapeleka private kama ninyi, ila hata tukiwapeleka shule za kanumba mnazoziita, wapate angalau C moja. watoto wanatia huruma. wanajisomea wenyewe kwa vibatari bila mwalimu, kwa nini?
    Ondoeni mifumo huria kwenye elimu na afya.
    Biashara kwenye elimu inaua, haifai.

    ReplyDelete
  5. Shule hazijengwi na kuendeshwa kisiasa. Zinajengwa na kuendeshwa kitaalamu. Fedha zipo za kuboresha elimu nchini kwetu, ni kwamba tu ubinafsi,upotofu wa uzalendo, ufisani na matumizi mabaya ya fedha za wananchi vimetawala.
    Angalia mishahara ya wabunge, mawaziri, wakuu wa mashirika ya umma, magari ya serikali na mashirika, matumizi ya maofisini, safari na semina na mikutano ndipo utajua kwanini shule zinazorota. Hawa vigogo wetu hawajali kwani watoto wao wanasoma shule nzuri. Hao hao watoto wa walala hoi ndio watajawanyima usingiz hao vigogo na wanao wenye "privileges". Someni alama za nyakati mkiwa bado mwaweza kujirekebisha, enyi vigogo msioambilika. Angalieni yale ya Tunisia na Misri.

    ReplyDelete
  6. Serikali imepuuza idara ya ukaguzi wa shule ikafikiri kuna kitakachoendelea, Shule hazikaguliwi na nyingine zina miaka kumi hazijui kama kuna watu wanaitwa wakaguzi wa shule. Maslahi ya wakaguzi ni kichekesho, mkaguzi anayeongoza mikoa miwili anazidiwa mshahara na deo anayeongoza wilaya moja. Huyo mkaguzi hana nyumba wala marupurupu mengine, zaidi ya kukata tamaa atafanyaje? Fedha za kukagulia shule hakuna. Kwa ujumla serikali imepuuza elimu. Labda ni mkikakati ya kuzalisha watu wasioweza kuhoji uchakachuaji wa kura. Lakini dawa yenu inachemka pamoja na mikakati hiyo mtang'ka tu. Tumechoshwa.

    ReplyDelete
  7. Mimi ushauri wangu badala ya kuwa na shule za sekondari tu kuwe pia na shule za ufundi ambapo mwananfunzi akimaliza anaweza kwenda kujiajiri mwenyewe. Mimi napendekeza kuwa kuwe na wastani kwa wanafunzi wanaoweza kwenda sekondari na wenye wastani wa chini ni vizuri kuwaingiza kwenye shule za ufundi. Mapendekezo kwenye shule za ufundi kuwe na michipuo yote ambapo mwananfunzi anaweza kuchagua kwa mfano ufundi selemara, ushonaji, upishi, wahudumu (wafundishwe customer care na uaminifu), utengenezaji wa vitu vidovidogo kama bites,juice, maziwa ya mgando (yorgat), n.k.
    Mimi binafsi naona hili ni jambo zuri kwani si wanafunzi wote wanauwezo wa kumudu masomo ya sekondari. Kwa upande wa wale wanaochaguliwa kuendelea na sekondari kuwe na monthly test na wastani ambao mwanafunzi anatakiwa kufikisha ili kuweza kuweka standard otherwise tutarajie matokeo kama tunayoyaona sasa. Haya matokeo ni uzenbe wa serikali na wizara inayohusika kuingia siasa kwenye maisha ya wototo wasio na hatia.
    YAKITOKEA KAMA YA TUNISIA AU MISRI NANI WA KULAUMIWA??? RAISI NA SERIKALI YAKE YOTE KWANI HAYA NDIO MATUNDA YAO.

    ReplyDelete
  8. ubabe kwenye suala la elimu si kitu kizuri maana huwa tunaona majibu ya wanasiasa hasa mawaziri wa utumishi, elimu na tamisemi wanavwajibu walimu hata pale anapodai haki kwa sheria. Jamani wananchi tuandamane kuiondoa ccm madarakani. Pia serikari inaona idara muhimu hata humu mashuleni wakuu wa shule huwasikiliza wahasibu tu.

    ReplyDelete
  9. Turudishe mitahani ya darasa la nne, kidato cha pili, na hakuna mwanafunzi kuendele kama amefeli hata kama atakariri darasa mara 3 bora atoke akiwa ameelewa.

    Suala jingine Mwl Nyerere hakuwa mjinga alipoanzisha mashule nakuweka vipindi vya kilimo, ufundi na sayansi kimu, waliofail enzi hizo masomo mengine hawakutoka bure bali waliendeleza stadi walizozipata shule na maisha yalikwenda mbele.

    Vyuo vya walimu pia mbali na kufundishwa ualimu pia walifundishwa mambo mengine ya ziada kama sanaa, michezo sayansi kimu n.k JAMANI YAKALE NI DHAHABU ALIYELETA MSAMIATI HUO HAKUWA MJINGA, HEBU WIZARA YA ELIMU IGEUKE NYUMA NA KUREJESHA MITAALA YA ZAMANI.

    WAALIMU PIA WAPEWE HESHIMA YAO BILA MWALIMU HATA HAO WANAOJIITA MAWAZIRI AU MAKATIBU WAKUU WASINGEKUWA KATIKA NAFASI HIZO

    ReplyDelete