27 December 2010

Wasomi UDSM wamuaga Jaji Ramadhani wakidai katiba

Na Mwandishi Wetu

MWANGWI wa kilio cha ama kufanyika kwa marekebisho makubwa ya msingi ama kuwa na katiba mpya kabisa nchini, unazidi kusikika kila kukicha ambapo sasa imeelezwa kuwa Watanzania wawe makini katika kuijadili katiba ya sasa, ili kuepuka
kilichotokea katika Azimio la Arusha na maadili ya uongozi.

Akizungumza mwishoni mwa wiki katika hafla ya kuagwa na wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Augustino Ramadhan, ameendelea kusisitiza kuwa suala la kuwa na katiba mpya linazungumzika.

"Nimeshatoa msimamo wangu mara chungu mzima, suala hili
linazungumzika...mabadiliko ya katiba yanaweza kufanyika kwa namna mbili, ama kuziangalia zile kero na kuzitafutia dawa au kuwa na katiba mpya kabisa, lakini nimekwishasema mara kadhaa kuwa suala hilo linazungumzika huo ndiyo msimamo wangu," alisema Jaji Mkuu Ramadhan.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Lwekaza Mukandala alisema kuwa haja ya kuwa na katiba mpya imekuwepo kwa muda mrefu na wakati huu ni dhahiri, baada ya wadau wengi katika mchakato wake kuwa wamepaza
sauti zao juu ya suala hilo.

"...Haja imekuwepo miaka mingi...sasa ni dhahiri kabisa...watu wengi muhimu au wadau wakuu walikuwa hawajawa convinced (kushawishiwa) sasa wadau wengi wamezungumzia...hata matamshi ya Waziri Mkuu yanaonesha

kuwa hata serikali sasa imetambua umuhimu wake.
"Sasa tunachosubiri ni mchakato wa namna hayo mabadiliko makubwa ya katiba yatakayofanyika," alisema Prof. Mkandala, huku akionekana kukwepa swali la mapungufu yanayopaswa kufanyiwa mabadiliko hayo katika katiba ya sasa na vitu gani viwemo katika mabadiliko mapya;

"Hilo si jambo la kuzungumza sasa, nafikiri linahitaji utafiti wa kina, na hapa chuoni tayari kuna makundi ya watu mbalimbali yanafanya kazi hiyo tayari nafikiri wakati ukifika yatawasilishwa," alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sheria ya UDSM, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema kuwa yeye ataunga mkono makundi mawili, lile linalohitaji katiba mpya na lile linalohitaji mabadiliko makubwa na ya msingi katika katiba ya sasa.

Alisema kuwa Tanzania ni kati ya nchi zinazoongoza kwa kuwa na katiba nyingi katika Bara la Afrika na hata duniani kwa ujumla kwani imewahi kuwa na katiba nne na sasa iliyopo ni ya tano, tangu kupata uhuru mwaka
1961.

"Suala la katiba mpya liko wazi kabisa...watu wengi hawajui Tanzania inaongoza katika Bara la Afrika na pengine hata duniani kwa kuwa na katiba nyingi...katiba tano...katiba ya sasa ya mwaka 1977 ilichukua mifumo mbalimbali ya katiba duniani...lakini kwa kiasi kikubwa msingi wake ni ule wa Ufaransa.

"Maana Ufaransa wana rais mtendaji na waziri mkuu mtendaji...mabadiliko ya yaliyoko katika katiba ya sasa ambayo wengine wanayakejeli hayakutokana na zawadi ya serikali...yalitokana na mapambano ya wakati huo sisi tukiwa vijana chuo kikuu na wengine kama akina Shivji, Ringo Tenga, Mvungi na wengine;

"Tukayasema kwenye makongamano...mfano ukomo wa madaraka kwa rais kuwa na vipindi viwili madarakani, hivyo wakati Rais Mwinyi akiingia madarakani alikuwa akijua mapema kabisa kuwa atakuwa madarakani kwa vipindi viwili tu...pia suala la haki za binadamu kuingizwa katika katiba nalo lilitokana na mapambano hayo ya wanaharakati.

"Kwa kweli mimi nitaunga mkono wote wanaotaka katiba mpya au mabadiliko makubwa ya msingi...mjadala ukianza kuna mambo ambayo sisi tutayasema...upande wetu shule ya sheria tulikwishaanza tangu mwaka 2007, Profesa Mgongo Fimbo ameshatoa kitabu kabisa," alisema Prof. Kabudi na kuongeza;

"Lakini tuangalie kwa makini katika mjadala huu, tusifanye makosa kama ilivyokuwa katika Azimio la Arusha kulitupa lote na sasa tunaanza kulililia pamoja na miiko yote ya uongozi...ni ukweli kuwa katiba ya sasa ina mapungufu mengi sana."  

1 comment:

  1. HIVI NYIE MNAJIONGOPEA KILA SIKU ETI MTAUWASHA MOTO,HIZO NI NDOTO,NINI CHADEMA,HAPA HATA KAMA ATAKUJA BGAGBO MTALAMBISHWA MCHANGA TU,WAKATOLIKI WANACHOWAZA NI KUWA HAPA TANZANIA KUWA WAO NI WENGI,SIJUI WAMEJIPANGA NK,SHUKURUNI SANA WAISLAM WA HAPA BONGO NI WAVUMILIVU SANA,NDO MAANA WAPO KIMYA,LAKINI MSIPOJIREKEBISHA NA KUUENDELEZA HUO UDINI WENU,MSIFIKIRI MTASALIMIKA,LIKIVUNDA HAPONI MTU WACHENI CHOKOCHOKO ZITALIANGAMIZA TAIFA,KAMA MNAUCHUNGU BASI MNGALIUONESHA NA MAPEMA,IWEJE MNAKUMBUKA SHUKA KUMESHAKUCHA,KUNA ALIYEVURUNDA KTK NCHI HII KAMA JAMAA YENU BAUNSA MBONA MLIKUWA KIMYA,MNA CHUKI HAMNA UCHUNGU

    ReplyDelete