Na John Gagarini, Kibaha
WANAFUNZI wawili wa sekondari wamekufa na watu wengine wanne kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kugonga mnazi.Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Absalom Mwakyoma alisema kuwa ajali hiyo ilitokea
Desemba Mosi mwaka huu majira ya saa 1:45 usiku katika Kijiji cha Kiguza barabara ya Kilwa wilayani Mkuranga.Kamanda Mwakyoma alisema kuwa gari hilo lenye namba za usajili T 608 APK aina ya Toyota Hilux lilikuwa likiendeshwa na Bi. Anna Kangidaly (56) mkazi wa Tegeta Jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa gari hilo ambalo haikufahamika lilikuwa linatoka wapi liliacha njia na kugonga mnazi na kusababisha vifo vya wanafunzi hao.
Aliwataja wanafunzi waliokufa kuwa ni Aziza Abdallah (15) ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Tinge ambaye alifariki baada ya kufikishwa kwenye hospitali ya
Wilaya ya Mkuranga na Nasoro Mchurubi (15) mwanafunzi wa Shule ya sekondari ya Mguruwe, Kilwa ambaye alifia Hospitali ya Muhimbili.
Aliwataja majeruhi kuwa ni Siyenu Nobileki (16), mwanafunzi wa Sekondari ya Miguruwe, Kilwa, Asia Mohamed (38) mfanyabiashara mkazi wa Kunduchi, Amina Said Kibuli (50) wa Charambe na Maria Ngokoya (55) mkulima mkazi wa Kawe ambao walitibiwa kwenye hospitali ya Mkuranga na kuruhusiwa.
Kamanda Mwakyoma alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo bado hakijafahamika mara moja na dereva anashikiliwa na jeshi hilo kwa uchunguzi zaidi juu ya tukio hilo.
No comments:
Post a Comment