28 December 2010

Wachezaji Yanga kutolewa 'kafara'

Na Elizabeth Mayemba

UONGOZI wa Klabu ya Yanga, umepanga kuwaadhibu baadhi ya wachezaji wake wanaodaiwa kuwa ni vinara wa mgomo wa mazoezi yaliyofanyika Ijumaa katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.Wachezaji hao licha ya kugoma
mazoezi, pia walitishia wangegoma kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya AFC Leopard iliyochezwa juzi kwenye Uhuru, Dar es Salaam.

Licha ya kugoma kufanya mazoezi, wachezaji hao pia walitishia kugomea mechi dhidi ya AFC Leopard iliyofanyika juzi katika uwanja huo, ambayo hata walicheza na kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Habari za uhakika zilizopatikana Dar es Salaam jana, kutoka ndani ya klabu hiyo zilieleza kuwa uongozi wa Yanga, umepanga kutafuta kiini cha mgomo huo na endapo watabainika wachezaji walioanzisha chokochoko hizo watatolewa 'kafara'.

"Haikuwa picha nzuri hata kidogo, viongozi karibu wote walisikitishwa na mgomo huo na wamesema wapo wachezaji ambao siku zote ni mstari wa mbele katika kuanzisha minong'ono ya chini chini na baadaye yanatokea kama haya yaliyotokea," kilidai chanzo hicho.

Habari hizo zilidai kwamba malalamiko ya wachezaji hao yalikuwa ni sahihi, ila walichotakiwa kufanya ni kukaa na viongozi ili kujua hatima ya malipo yao, lakini badala yake wakagoma kufanya mazoezi.

Hata hivyo wachezaji walidaiwa kugoma baada ya kukasirishwa na mambo yanayofanywa na viongozi hao wa Yanga, kila walipokuwa wakitaka kulipwa fedha zao za usajili wa msimu huu.

Baada ya mgomo huo viongozi hao wa Yanga, wanadaiwa kukasirishwa na hatua hiyo na ndiyo maana jana jioni, walifanya kikao cha dharura na moja ya ajenda ilikuwa ni kuujadili mgomo huo.

Jana Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo ilipanga kukutana saa 11 jioni kwa lengo la kujadili ushiriki wa timu katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, Shirikisho (CAF) na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, pamoja na mbalimbali.

2 comments:

  1. Viongozzi acheni vitisho, walipeni wachezaji muone kama yote hayo yatatokea!

    ReplyDelete
  2. Viongozi mnataka msipowalipa watu mishahara yao wakae tu kimya?
    Acheni mabo ya zamani!
    Mkiwapa adhabu nitahama Yanga.

    ReplyDelete