24 December 2010

Twanga Pepeta kufanya mambo leo Tabata

Na Mwandishi Wetu

Bendi ya muziki wa dansi ya African Stars 'Twanga Pepeta' imewaomba wapenzi wao kujitoteza kwa wingi leo usiku kwenye onesho lao la Mkesha wa Krismasi, litakalofanyika katika Ukumbi wa  Da’ West Park Tabata.Akizungumza
Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa bendi hiyo Asha Baraka alisema onesho hilo litakuwa la aina yake, kwani mashabiki wa Twanga Pepeta pia watatumia fursa hiyo kuwafariji wanamuziki wa Twanga Pepeta kwa kifo cha mwanamuziki mwenzao, Abuu Semhando aliyefariki Jumamosi iliyopita kwa ajali ya pikipiki.

“Tunawaomba wapenzi wetu wajitokeze kwa wingi, ili tujumuike pamoja kama familia ya African Stars Entertainment,” Asha Baraka alisema.

“Hili litakuwa onesho letu la kwanza la wazi, tangu tumzike Semhando. Tumeandaa burudani nzuri kwa wapenzi wetu kwa ajili ya Krismasi,” alisema na kuongeza kuwa bendi hiyo kwa mara ya kwanza itatambulisha rasmi nyimbo zake mpya walizomshirikisha mwanamuziki nguli kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Bozi Boziana.

“Tutaonesha video ya nyimbo hizo kwa mashabiki wetu ukumbini, ikiwa ni zawadi ya Krismasi kwa mashabiki wetu,” aliongeza.

    Pia amesema rapa wa bendi hiyo Saulo Furgasom atazindua ‘rapu’ yake mpya kwenye onyesho hilo iliyoandaliwa na Bob Entertainment na kudhaminiwa na kinywaji cha Konyagi na Freditto Entertainment.

Naye mratibu wa onesho hilo Joseph Kapinga, alisema burudani hiyo itakuwa ya kipekee na maalumu kwa kusherekea mkesha wa Krismasi ambapo zawadi mbalimbali zitatolewa kwa maashabiki.“Twanga Pepeta watapiga albamu zao zote. Matumaini yetu ni kuwa watu watapata burudani ya kutosha kuliko siku nyingine,” alisema Kapinga.

Alisema mashabiki hao watapata uhondo wa nyimbo zilizopo katika albamu yao ya Mwana Dar es Salaam ambazo ni Shida ni Darasa, Rafiki Adui, Mwisho wa Ubaya ni Aibu, Nazi Haivunji Jiwe, Mwana Dar es Salaam iliyobeba jina la albamu na Sitaki Tena.

No comments:

Post a Comment