Na Addolph Bruno
KOCHA wa Ngumi wa Klabu ya Ashanti, ambaye pia anatoa mafunzo ya kujitegemea, Rajabu Mhamila 'Super D' jana amepata msaada wa sh. 150,000 zitakazomwezesha kushiriki kozi ya 10 ya ukocha, iliyoandaliwa na Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT).
Msaada huo ambao ni wa pili kwa kocha huyo kupewa ulitolewa na mdau wa michezo, Zulfigal Ali kumwezesha Super D kufanikisha malengo yake ya kuendeleza mchezo wa ngumi kwa vijana, baada ya kushiriki kozi hiyo itakayoanza Desemba 14 hadi 24, mwaka huu Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana, wakati akimkabidhi pesa hizo Zulfigal alisema ameamua kufanya hivyo, ili kuungana na wadau wengine wa michezo ikiwemo serikali katika kuendeleza michezo.
"Michezo siku hizi hapa nchini ni ajira kwa vijana wetu na ili tuweze kufanikisha zaidi, tunatakiwa kuwawezesha walimu kwanza ambao watatoa mwanga kwa wengine ndiyo maana nimeguswa katika hili na kusaidia," alisema.
Naye Super D, alisema anashukuru na kuahidi kuzingatia kozi hiyo siku zote ili aweze kupanua ujuzi ambao utawawezesha kuwasaidia mabondia wanaochipukia hapa nchini.
Awali kocha huyo alipewa msaada wa vifaa vya michezo vyenye thamani ya sh. 300,000 kwa ajili ya mazoezi ya mabondia wanaohudhuria mafunzo yanayotolewa na kocha huyo.
No comments:
Post a Comment