28 December 2010

Mwanasheria Mkuu apinga katiba mpya

Grace Michael na Rabia Bakari

WAKATI Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Bw. John Mnyika akiwasilisha hoja binafsi ya mabadiliko ya katiba mpya, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema amesema kuwa haiwezekani kuandikwa upya na badala yake
kinachowezekana ni kuifanyia marekebisho iliyopo.

Hatua hizo mbili katika mjadala wa katiba mpya unaoendelea kupamba moto kila kukicha zilifikia katika sehemu na nyakati tofauti jana, ambapo Bw. Mnyika alikuwa anawasilisha nia yake hiyo kwenye ofisi za bunge na Jaji Werema akizungumza na waandishi wa habari, ikuru, baada ya kuapishwa kwa Jaji Mkuu, Mohamed Othman Chande.

Katika Ofisi za Bunge jijini Dar es Salaam, Bw. Mnyika aliwasilisha nia ya kutoa hoja binafsi katika Mkutano wa Bunge utakaoanza Februari 8, 2011 kuhusu kuanzishwa kwa mchakato wa mabadiliko ya katiba.

Bw. Mnyika aliwasilisha nia hiyo jana katika ofisi ndogo za bunge jijini Dar es Salaam katika Ofisi ya Katibu wa Bunge na kupokewa na Mkurugenzi wa Idara ya Taarifa, Bw. Eliakim Mrema kwa niaba ya katibu aliyekuwa likizo.

"Nimepokea taarifa hii, sisi kama taasisi, na kwa bahati mbaya au nzuri katibu yupo likizo hivyo naipokea mimi kwa niaba yake," alisema Bw. Mrema.
Kabla ya kuwasilisha taarifa hiyo, Bw. Mnyika alizungumza na waandishi wa habari katika moja ya kumbi za ofisi hiyo, na kudai kuwa, ameona upungufu mkubwa katika maeneo zaidi ya 90 katika katiba, na hivyo kuomba mawazo zaidi ya wananchi juu ya matatizo hayo na mapendekezo yao ya nini kifanyike.

"Katiba inayotumika hii leo ni ya mwaka 1977, tangu kipindi hicho kuna mabadiliko mengi yameshatokea kama ya kiuchumi, kiteknolojia; pili uundwaji wa katiba hiyo haukuwashirikisha wananchi; tatu katiba hii inakabiliwa na changamoto nyingi, mfano suala la Muungano na Tume ya Uchaguzi," alisema.

Alisema katiba ya sasa sio ya kufanyiwa marekebesho tena, bali kubadilishwa kabisa, kwani huwezi kuweka viraka katika upungufu mkubwa namna ile.

Alisema upungufu hayo yamegawanyika katika misingi mikuu mitatu, ikiwa ni pamoja na kasoro za ibara mbalimbali za katiba, zinazominya demokrasia na kunyonya haki za wengine ikiwemo mamlaka makubwa ya rais aliyopewa.

"Mapungufu mengine ni katika uchaguzi, Tume ya Uchaguzi kutokuwa huru pamoja na mfumo wa utendaji kwa ujumla, matokeo ya urais kutopingwa mahakamani, pamoja na mfumo wote wa uchaguzi kwa ujumla.

"Muingiliano wa mamlaka pamoja na taasisi za uwajibikaji mfano Tume ya maadili, TAKUKURU na kufanya vyombo hivyo kutokuwa huru," alidai.
Alisema kuwa msingi wa hayo yote ni katiba mpya, na kudai kuwa mapungufu mengine makubwa katika katiba ni pamoja na kuwa na baadhi ya mambo ambayo hayatumiki kabisa tangu yawekwe.

"Mfano kwenye katiba kuna sehemu inasema kutakuwa na chombo cha mamlaka ya katiba na hakijawahi kufanya kazi hata siku moja, kwani chombo hicho kilikuwa ni kwa ajili ya kushughulikia muungano tu.

Sasa huwezi kuwa na katiba yenye mashimo mengi kiasi hicho, suluhisho ni katiba mpya," alidai.

Bw. Mnyika aliwashangaa wote wanaokusanya maoni kwa wananchi ya kuuliza kama wanataka katiba mpya au la, kuwa kufanya hivyo ni makosa kwani wananchi tayari wameshaonesha kuwa wanataka katiba mpya, kinachotakiwa ni utekelezaji, na maoni yawe wakati wa kupitisha katiba mpya.

Alisema kuwa hoja yake anayotarajia kuwasilisha bungeni, rasimu yake itakuwa wazi wiki ya kwanza Januari, 2011 na wananchi wanaruhusiwa kuongeza na kutoa mawazo juu ya rasimu hiyo ya hoja.

"Kabla sijapeleka hoja bungeni nitaitoa hadharani ili kila mtu atoe maoni yake, ili nitakapoipeleka bungeni yasiwe ni mawazo yangu bali yenye mchango wa wananchi," aliongeza.

Alidai kuwa baada ya kuweka hadharani rasimu hiyo ya hoja, wananchi wanaweza kuchangia kupitia ofisi yake ya ubunge iliyopo Magomeni jijini Dar es Salaam; au kwa barua pepe <mbungeubungo@gmail.com>; au kwa simu namba 0783 552010; au kwa sanduku la barua, S.L.P 62066 Dar es Salaam.

"Na wiki ya pili ya Januari, 2011 nitafanya mkutano wa wazi Ubungo kukusanya mawazo ya jumla. Na nimefanya hivyo kutokana na unyeti wa suala lenyewe ili nitakapoiwasilisha bungeni iwe ni hoja yenye uzito, yenye mawazo ya wengi na si Mnyika pekee," alisema.
   
Aliongeza kuwa mfumo huo wa kuwasilisha hoja alioutumia ni wa pekee kidogo, kwani yupo bungeni kuwakilisha wananchi, na hivyo ameona ni bora kuwasilisha hoja za wananchi na si yake binafsi kama wafanyavyo wabunge wengi.

Kwa upande wake Jaji Werema ambaye ndiye mshauri mkuu wa Serikali katika masuala ya kisheria aliweka msimamo wake huo jana katika viwanja vya Ukulu, Dar es Salaam katika hafla ya kuapushwa kwa Jaji Mkuu wa Tanzania Mohamed Othuman Chande.

Kurekebisha na kuondoa mambo mengine ni ruksa lakini sio kuandika katiba mpya...tutafanya haya kulingana na mapendekezo au matakwa ya Watanzania hivyo hili halina tatizo litafanyika, alisema Jaji Werema.

Alisema kuwa haitakuwa vyema kama Watanzania watatofautiana kutokana na suala hili kwa kuwa linajadilika na linaweza kutekelezwa kwa manufaa ya wananchi na katika hili kila mmoja anatakiwa kusikilizwa kwa kuwa anao uhuru wa kusema na yuko sahihi.

Kutokana na hali hiyo, alitumia mwanya huo pia kuwaasa wanahabari kutokuwa wachochezi katika suala hili bali watumie kalamu zao vyema kuelimisha wananchi umuhimu wa katiba.

Ni vyema kalamu zenu mkazitumia vizuri kwa kuwa zikitumika vibaya zina madhara makubwa...zinaweza zikanyonga mtu, zinaweza kuleta machafuko, hivyo katika hili acheni ushabiki na muweke mbele maslahi ya Watanzania,” alisema Jaji Werema.

Akijibu swali kuhusu suala hilo kubebwa na wanasiasa, alisema kuwa kila jambo ni lazima liwe na mbebaji, hivyo hata katika suala la katiba ni lazima awepo mbebaji wa aina yoyote kwa kuwa matokeo yake ni matakwa ya Watanzania wote.

Tusivilaumu vyama vya siasa kwa sababu mambo yote hayo ni siasa na hili la katiba lingeweza kubebwa na mtu yoyote awe Profesa, mbunge, mwananchi au mtu yoyote,” alisema.

Akizungumzia uteuzi wa Jaji Mkuu, Jaji Werema alisema kuwa ni mtu mtulivu mwenye uwezo wa kuwaunganisha majaji wote mahali pa kazi lakini pia ni mtu mwenye uzoefu na anayeifahamu vyema sheria hivyo kuteuliwa kwake kutasaidia kuimarisha mhimili huo.

Naye Jaji Mkuu akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kula kiapo cha uaminifu, alisema kuwa ni wajibu wake kuhakikisha wananchi wanapata haki zao mapema na kuondoa malalamiko ya ucheleweshaji wa kesi.Changamoto zipo na hazijaanza na mimi lakini nitajitahidi kuhakikisha tunakuwa imara kwa kuwa na mahakimu wa kutosha na wenye ujuzi na sifa za kutosha ili waweze kukidhi mahitaji au matarajio ya wananchi.

Kwa upande wa Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhan, aliwaomba wananchi kuendelea kuheshimu mahakama na maamuzi yanayotolewa katika kila jambo hivyo kuachana na utamaduni wa kuchukua sheria mkononi.

10 comments:

  1. AG unahofu na ajira yako kwamba ukisema ibadilishwe utatolewa kwenye nafasi, watu muache kuwa wanafiki kwakuwa tu mliteuliwa na Rais sema ukweli hata kama hautompendeza aliyekuchagua kwakuwa unapokula kiapo unakula kwa kushika msahafu au biblia unaapa kwa Muumba wako na si kwa binadamu, wanasiasi waliowekwa na Rais wameonekana kumuogopa mno binadamu kuliko wanavyomuogopa muumba wao ambapo siku ya mwisho hatakuwepo Rais kusema kuwa ulikuwa unafuata maagizo yake kila mtu atasimama peke yake siku ya HUKUMU mnaonekana hamlitambui hilo, ila mngelitambua mngeacha unafiki wenu usio na maana.

    ReplyDelete
  2. Werema wenye kutoa rukhsa kubadilishwa au kuandikwa upya katiba ni sisi wananchi na si nyie makuadi wa JK a.k.a Gbabo na serikali dhalimu ya CCM. Mpende msipende moto umeshawashwa mkiendelea kujificha kwenye kichaka cha katiba mbovu iliyozungukwa na majani makavu mtaungua wote humo humo. Nasi hatuna huruma na nyie wezi wa CCM na serkali yake. Tutawaunguza mpaka yabaki majivu kwani moto wenu unatakiwa uwe mkali kuliko moto wa vibaka ambao ni wezi wadogo kulinganisha na nyie. Dawa mtoke humo ndani mlikojificha kwenye kichaka cha katiba kibovu tunaweza kuwaonea huruma au kuwachapa viboko kidogo tu. Mking'ang'ania tunawawasha moto wa petroli. Tumewachoka mafisi walafi mliojificha ndani ya katiba mbovu mkitafuna uchumi wetu.

    ReplyDelete
  3. Watanzania tuwe waungwana jamani! Jaji Werema amesema kweli kabisa. Si kila kitu kilichoko kwenye katiba yetu ni kibaya. Tena wakati mwingine ninawashangaa sana watu wanapolinganisha na jirani zetu Wakenya. Ni lazima watu watambue kuwa Kenya haijapata kuwa na katiba yao! Tofauti sana na Tanzania. Wakenya wenyewe wamekiri kwamba muasisi wa taifa la Tanzania aliwafanyia watanzania jambo moja kubwa sana kuwapa katiba. Katiba tuliyonayo ilitungwa mwaka 1977 ni mhimu sana kuelewa hilo. Pili ilifanywa wakati wa utulivu mkubwa sana wakati huo. Inawezekana kabisa mazingira yalikuwa tofauti na leo; mazingira ya chama kimoja cha siasa. Lakini ni lazima tukiri wakati ule ulikuwepo utulivu mkubwa kabisa kuliko sasa ambapo watu wanajadili katiba kwa jaziba tupu. Hatari ninayoina sasa upo uwezekano watu wakadai katiba kwa jaziba na hivyo kuweza kuleta madhara makubwa sana kwa taifa letu. Tukumbuke katiba siyo kitu cha mchezo mchezo hivi. Tunazungumzia uhai wa taifa na watu wake. Waziri mkuu alitoa mawazo mazuri kabisa lakini inashangaza wengine wakabeza sana.

    Ni hivi mimi ninaamini yapo mambo yanayohitaji mabadiliko kulingana na nyakati. Hata Marekani wamekuwa wakifanya hivyo. Jaji Werema amesema hata India wamefanya hivyo. Jamani tujadili mambo gani yanatuletea shida kisha tuyabadilishe. Tume ya uchaguzi, madaraka makubwa ya rais hayo ni mambo yanayozungumzika. Tunaweza kujadili kumwondolea rais madaraka makubwa aliyonayo japo kwa wakati uliopita ilikuwa vizuri ili kumwezesha rais wetu kufanya mambo kwa uhuru mkubwa zaidi ili kuwaletea watu wake maendeleo. Lakini mabadiliko ya kiuchumi ambayo yametokea yamesababisha rais naye awe mtafutaji wa mali ni mhimu sana apunguziwe madaraka. Asiyatumie kwa faida yake na marafiki zake na wanamtandao wenzake. Tena anaweza kuyatumia kuwa Dictor. Tume ya Uchaguzi lazima iridhishe makundi yote yanayogombea urais. Lazima ithibitishwe na bunge ichaguliwe na wagombea wenyewe ikibidi.

    Tunaweza kufikiria zaidi juu ya uchaguzi kuhojiwa! Maana inaweza kutokea kwa jinsi tabia yetu waafrika ilivyo tukawa na malumbano ya mahakamani kila wakati badala ya kushughulikia matatizo ya wananchi. Hivyo hilo tunaweza kufikiri kwa undani zaidi juu ya hilo. Mhimu ni kuwa na tume yenye kutenda haki itakayowaridhisha wote wanaoshindania nafasi ya urais.

    Kwa ujumla baadhi yetu hatuungi mkono kuvunja yote yaliyoko kwenye katiba. Badala yake tunaona ni vizuri kuyafanyia marekebisho mapungufu yote yanayoonekana kwenye katiba tuliyonayo. Na watanzania sio wakwanza kufanya hivyo hata nchi nyingine duniani zimefanya hivyo. Sipendi kabisa watu wanaolinganisha taifa letu na Kenya. Historia ya Kenya ni tofauti kabisa na Tanzania. Mtu yeyote anapaswa kufanya analysis ya Tanzania kipekee na siyo kulinganisha na nchi zingine kama Kenya. Nikiwa Muungwana naungana na Jaji Mwanasheria mkuu wa Serikali ni mtu mwenye busara anapaswa kusikilizwa na si kubeza kila kitu mladi eti tu yupo serikalini. Hivyo kila analosema ni hovyo hapana hiyo si busara hata kidogo. Analoshauri Jaji Werema ni la busara kabisa na yapaswa yeyote mwenye busara akubali ushauri wake. Na mimi nimoja wa wale wanaona ushauri wake ni wa maana sana kwa mazingira ya sasa ya Tanzania.

    Mungu Ibariki Africa, Mungu Ibariki Tanzania

    ReplyDelete
  4. jamani swala la katiba mpya au katiba kufanyiwa marekebisho si swala la mtu kutoka kitandani kwake asubuhi na kujiskia kutembelea vyombo vya habari kwenda kuongelea kitu anachojiskia yeye kuhusu katiba. mi labda niseme kitu kimoja, wala huu si wakati wa kutukana viongozi kwa sababu wamesoma na wanajua kuhusu sheria wala werema si mwenda wazimu kusema kwamba katiba mpya haiwezekani na kutoa wazo lake kuhusu marekebisho. ninyi mnaojifanya mnauchungu na nchi hii mngefanya juhudi za kuwakutanisha kila kundi ili wajadili matatizo yao wajue mapungufu yakowapi ndio sasa tujue kupiga kelele kuhusu katiba mpya. mfano wakulima wakutanishwe na viongozi wao wajadili kadhalika wavuvi, madaktari,na wafugaji, na hiyo ndio maana ya delegated legslation.kwani hiyo serikali ya ccm ndani yake haina wabunge na madiwani wa CHADEMA ambao pia ni wabovu? msijifanye nyie ndio wakombozi na wala msilifanye swala la katiba lichukue sura tofauti sisi sote ni watanzania lakini tukae mezani katika kijiji , kata, wilaya, mkoa na hatimaye taifa zima hili swala linazungumzika vita ikianza hapa msifikirie eti hao wakina mbowe au werema watabaki, watanzania tutakufa wao watakimbia kujihifadhi na watarudi baada ya vita.

    ReplyDelete
  5. Jamani mlitegemea nini? Werema ni mwanaseria mkuu wa serikali. Kazi yake ni kuitetea serikali! na bosi wao kwa kupitia mwakilishi wake (Celina Kombani) alishasema hakuna haja ya katiba mpya! Sasa yeye (Werema) angesemaje? Hii ndio itifaki! Sio Zito ambaye haijui, kazi kuropoka tu?
    Tunachopaswa sisi ni kupigania haki yetu ya kuandika katiba mpya, sio kusikiliza Kikwete, Kombani, Werema, au afande nanii anasemaje! Hawa wote ni watumishi wetu waliotuasi siku chache baada ya kuchukua madaraka yetu. Kabla ya uchaguzi walikuwa wanauma maneno-hawakuwa wazi kuhusu lolote zaidi ya kusema watajenga flyover ubungo lakini mpaka wanunue magari na majumba yao ya kifahari. Zikibaki ndio watawapa wachina ili wawakodishe wadanganyika kwa bei chee wajenge.

    ReplyDelete
  6. ni kitu gani tunaogopa kubadili katiba mpya?tume ziliundwa nyingi lakini yakachukuliwa machache kwa sababu zipi?nchi ni yetu sote jamani!katiba isimlenge aliyepo madarakani peke yake! tuijadili kwa pamoja wala haina sababu ya kuchukua muda mrefu

    ReplyDelete
  7. Nawashangaa wanaopinga kuandikwa kwa katiba mpya,nguo ikichakaa hununuliwa mpya,na si kuwekewa viraka.Gharama yake ni yetu wenyewe ,na tumekwisha lipa gharama nyingi ambazo hata hazina maana na sote tunazijua kwani zimeendelea kutuweka utumwani kwa sababu ya kukumbatia ubovu.Tume ngapi zimeundwa ,ambazo zimekua zikishauri kuundwa kwa katiba mpya ,lakini kwa kuzingatia masilahi yao watawala wetu wamekua wakizipuuza ili hali wameziteua wao.jee hizo siyo gharama kwa wewe mlipa kodi. Tuachane na hao akina werema kwa sababu ndio walewale ambao wanahofia masilahi yao.Yangelizingatiwa baadhi ya maoni ya viongozi tawala wa Zanzibar ambao hawakutaka muafaka, leo, muafaka usingekuwepo .Lakini kura ya maoni kutoka kwa wananchi imeleta udugu Zanzibar .Kwangu mimi ninajua serikali yetu ni mbovu ,imejaa Mifisadi kwa sababu ya ushindi wa kifisadi kuanzia ngazi za mitaa hadi juu, ninawaomba ,basi inatosha .Mmetuumiza vya kutosha.Ninajua hakuna wa kuwaadabisha , lakini kwa hili la katiba hata kama mtaendelea kubisha dalili zote zinaonyesha kamba imefikia pembamba, kama vilivyokuja vyama vingi nalo hili la katiba litaingia hivyo hivyo .Mungu hawezi kuona watu wake wakiendelea kutaabika kama vile hawajapata UHURU.Umasikini umetutafuna hadi kucha !

    ReplyDelete
  8. Wewe Mwanasheri ni tofauti gani za maoni na hizo tofauti zimetoka wapi, sisi bwana tunataka katiba mpya piga ua, hatukuelewi. Nyinyi ndio mnao mdanganya Rais kwa maslahi yenu binafsi. Kwanza wewe warema kama mwanasheria mkuu ni kitu gani umeshawasaidi hawa wananchi zaidi ya kupingapinga tu.

    Wewe jifikirie upo peke yako kuiongoza nchi na sheria zenu zinazowanyonya wananchi na kuwachanganya wananchi. Kweli umeingia mkataba ukashindwa kutekeleza makubaliano bado unapigwa fidia ni mkataba gani huo. Na bado wewe kama kioo chetu unatusaliti tena. Ni kwa nini mnafichaficha toeni makaratasi yote ya mkataba yaonyesheni yaonekane kama mnavyolia kulipa hilo deni.

    Wananchi wanataka utawala huu wewe unataka utawala huu je tutafika? Mambo ya katiba unataka kutupeleka kulekule kwa Tanesco, mlishauriwa mkapuuza sasa ngoma hio. Sisi tunataka katiba tuchakarike, tubanane vizuri. Kwanza ukifikiria ulicho ongea na haya maoni ya watu utajua watu wamechukizwa na kauli zako. Na hizi ndio dalili za kupanga maandamano nchi nzima. Hiki ni kibali tosha watanzania tujiandae tuungane kwa pamoja kuingia barabarani wao waendelee kumdanya huyo Rais huko Ikulu.

    ReplyDelete
  9. Nimefurahi sana kuona kuwa wananchi wanaweza kujadili mambo yanayowahusu bila kuogopa.Kabla ya 1992 isingewezekana hivyo.Ni kweli katiba si ya mtu wala ya chama, hivyo si vema kwa chama fulani kujidai kuhodhi katiba, hii ni mali yetu. Iwapo katiba ni mali yetu, ni busara sana kuipitia kwa utaratibu bila jazba wote wakishirikishwa kwa namna yoyote ile ili mradi mawazo ya wananchi yapatikane. Itakumbukwa kabla ya vyama vingi kuruhusiwa mwaka 1992 kura ya moani ilikataa mfumo wa vyama vingi pengine wananchi hawakuelimishwa vizuri maana yake, lakini kwa busara za Baba wa Taifa alishauri vyama viwepo na vikaruhusiwa sasa tunaona matunda yake, na hata mijadala hii ni matunda yake.Nashauri busara itumike, na si kukurupuka sababu chama fulani kimesema ua kinataka katiba, ila wananchi wanasema nini juu ya katiba ya sasa, si kila kilichopo ndani ya katiba ya sasa ni kibaya, yapo mambo mengi mazuri na yakufaa, lakini yapo mambo yanayohitaji marekebisho tuyafanyie kazi. Ushabiki na jazba ya kisiasa haitatusaidia, zaidi itawanufaisha wachache ambao sasa wanadhani wanaonewa na katiba iliyopo, watu hao wakipewa nafasi holela wataweka katiba inayowapendelea na lazima litaibuka kundi lingine litakalo pinga katiba hiyo nyingine, ndipo mwanzo wa vurugu, hao wanaodai sasa watakimbia mana wanazo fedha za kukimbilia, lakini wewe na mimi tutabaki tufe katika vibanda vyetu. Tukatae kutumiwa na watu,, tuwe sisi tunapotoa maamuzi magumu na ya msingi kwa faida yetu na vizazi vijavyo.

    ReplyDelete
  10. kwanza niwapongeze watoa maoni wachache hapo juu ambao wameonyesha busara ya hali ya juu kuelelimisha wengine.mimi nipo nje ya nchi yangu kila siku najaribu kusoma maoni ya watanzania wenzangu.Nimegundua watanzania tunakoelekea tusipo chukua tahadhari mapema,tutaangamia au tutaangamiza wengine wasiopenda umwagaji wa damu au maafa kwa sababu ya ushabiki wa kipuuzi.Sijawahi kuona katiba inadaiwa kwa jaziba hata siku moja zaidi ya watu kutoa maoni yao nini kifanyike ili kufanikisha jambo kwa faida ya watanzania wote.Busara hainunuliwi dukani bali ni kipaji ambacho mtu anajaliwa na muumba wake.watanzania wanajiita wasomi ,wajuaji wa mambo wanazidi kuonyesha kuwa hawana busara kabisa tena mbaya heshima imetoweka.hivi kutukana kiongozi wa nchi au viongozi ni jambo la hatari sana,inaonekana malezi ya watu wanaotukana viongozi hata inawezekana wanatukana pia wazazi wao.ujuaji mwingi hata kwa kitu usichokijua utaleta maangamizi tusipokemeea tabia kama hii.Uongozi si kitu kirahisi kama baadhi ya watanzania wanavyofikiri.Badala ya kuwa watulivu na kutoa maoni nini kifanyike badala yake vitisho na matusi ndio vimetanda ndani ya magazeti,sasa tunasaidia nini ?sio kila jambo ni kulaumu tu ,toa mawazo watu wayapitie then yatendewe kazi.tusi sio wazo bali ni kuvuruga agenda.kama hoja ni katiba mpya basi toa mawazo iweje! na watu wengine wakitoa wazo sio kuwatukana maana ndio mawazo yao.Tusijifanye tunajua sana,usiasa usiingizwe kwenye mambo nyeti yanayohusu taifa letu.watoa maoni msichanganye wananchi waone kila linalofanywa na viongozi kuwa ni baya.ushauri wangu toeni mawazo mazuri ili yafanyiwe kazi.Ndio maana bwana mnyika amesema ataweka wazi mapungufu yaliyoko kwenye katiba yetu ili apate mawazo kutoka kwa watu mbalimbali kabla hajawasilisha mapendendekezo hayo bungeni.SISI watanzania ambao hatupo nyumbani inatuuma sana kuona ndugu zetu wanapoteza maisha eti kwa sababu ya ushabiki tu.msipoangalia mtauana na hao wanasiasa wenu wanakimbilia ughaibuni wakiwaacha mnauana bila hata kuwasaidia.Nakemea hiyo mbegu chafu ya watu waliojaa matusi na jazba badala ya kutanguliza busara ili kuliletea taifa letu amani ,mshikamano na maendeleo.fikiri kabla haujatamka neno baya,uangalie faida na hasara kwa taifa lako.Raisi sio kichaka cha matusi na yeye peke yake hawezi kujenga nchi ,tumpe ushirikiano sio kumtukana kila pakicha.Ni binadamu kama wewe,na pia haongozi nchi peke yake,ndio maana ana wasaidizi.mfano mzuri mpaka sasa yeye hajatamka neno lolote juu ya katiba mpya lakini unashangaa matusi anayotukanwa.Tubadilike watanzania tusiharibu amani tuliyonayo.MUNGU IBARIKI TANZANIA NA WATU WAKE;

    ReplyDelete