06 December 2010

MGAWO WA UMEME

*Kafulila amtaka Ngeleja ang'oke
*Aandaa hoja binafsi ya kutokuwa na imani naye


Na Grace Michael

MBUNGE wa Jimbo la Kigoma Kusini, Bw. David Kafulila amesema anakusudia kuwasilisha hoja binafsi bungeni kwa kulitaka bunge kuazimia kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri wa Nishati ya Madini, Bw. William Ngeleja kutokana na
kushindwa kusimamia utekelezaji wa sera ya nishati na mpango kabambe wa usambazaji umeme hali iliyosababisha migawo ya nishati hiyo ndani ya miaka miwili ya uongozi wake.

Kusudio hilo limo ndani ya taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari jana ambapo alisema kuwa tatizo la kukatika kwa umeme lina athari kubwa ndani ya jamii kwa kuwa hupunguza uzalishaji wa bidhaa viwandani na kuathiri mwenendo mzima wa ukuaji wa uchumi.

"Tangu mwaka 2006, serikali imeshindwa japo kupunguza tatizo hili la mgawo wa umeme. Viongozi wakuu wa serikali na hasa Waziri wa Nishati na Madini mara kadhaa wamekuwa akipotosha watanzania kuwa serikali inashughulikia kwamba mgawo wa umeme utakuwa historia  lakini siku hadi siku sekta ya umeme imevuka upeo wa viongozi hawa kiasi cha kauli zao kupoteza imani kwa Watanzania.

“Serikali ione kwamba suala la mgawo wa umeme linaathiri maendeleo kuliko hata mtikisiko wa uchumi, hivyo ifanye maazimio magumu kwa kutenga fedha za kutosha kutekeleza mradi mkubwa wa umeme wa uhakika, kwa mfano Stigler’s gorge (2000MW), Mnazi Bay 300MW na kufufua KIWIRA 200MW. Miradi yote hii inaweza kuendeshwa na sekta binafsi iwapo tutaweka mazingira mazuri ya uwezekezaji,” ilisema sehemu ya taarifa yake.

Mbunge huyo alipendekeza kutokana na tatizo hilo, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inatakiwa kuachana na ujenzi wa majengo na badala yake ijielekeze kwenye uwekezaji wa uzalishaji umeme ili kutatua kabisa tatizo hilo nchini.

Alisema kuwa TANESCO haistahili kubebeshwa hata chembe ya lawama katika mkataba wa RICHIMOND na baadaye DOWANS kwa kuwa serikali ndiyo iliyoielekeza TANESCO iingie mikataba hiyo na baadaye bunge kutoa azimio la kuvunjwa kwa mkataba na TANESCO, hivyo huo ni mzigo wa serikali unaotokana na ukosefu wa umakini, woga na kutowajibika kiuongozi kwa viongozi wa serikali.

Bw. Kafulila alisema serikali haipaswi kujitenga na gharama zitokanazo na udhaifu wa TANESCO katika hatua zote, kwani serikali ndio msingi wa matatizo yote ya TANESCO na hivyo inawajibika kubeba deni lote.

Alisema kuwa kwa kuwa serikali itapaswa kulipa deni hili kutoka katika fedha za walipa kodi wa Tanzania na kwamba fedha hizi zitaondolewa katika bajeti ya elimu, afya na kadhalika, ni lazima serikali itoe maelezo ya kina ya sakata zima mpaka kufika hapa ilipofikia.

“Haiwezekani serikali itumie kodi ya wananchi kulipa deni la mabilioni ya fedha kwa kampuni ambayo serikali imeshindwa kuthibitisha uhalali wake na hata kutaja mmiliki wake, kwa kuwa Taifa linaingia hasara kubwa ya mabilioni haya ya fedha kutokana na udhaifu wa serikali kusimamia mikataba na mpango mzima wa nishati, nakusudia kupeleka hoja binafsi bungeni katika Bunge la Februari ya kwa nini serikali isiwajibike kwa kuliingiza Taifa hasara kwenye sekta ya umeme.

"Shirikisho la wenye Viwanda nchini mara kwa mara limekuwa likieleza namna ambavyo wanachama wake wanaathirika na mgawo wa umeme. Mifano ya viwanda vya saruji imekuwa ikitolewa ambapo mgawo wa umeme unaongeza gharama za kuzalisha kwa kiwango cha dola za marekani 10 kwa kila mfuko wa kilo 50, hivyo kuongeza gharama, kupata hasara na kushindwa kulipa kodi serikalini," alisema.

Akizungumzia madhara ya mgawo wa umeme alisema kuwa gharama za uzalishaji zinaongezeka ambapo vijana wanaojishughulisha na kazi zinazotegemea umeme hupoteza zaidi ya asilimia 45 ya mapato yao kutokana na kutumia jenereta ili kupata umeme wa kutoa huduma kwa wateja wao lakini pia bei za bidhaa kupanda kutokana na gharama za uzalishaji kuongezeka.

“Kusimama kwa shughuli nyingi za huduma kama benki, hospitali, vyuo na shule, na hata vyombo vya habari katika utendaji wake hivyo hatuwezi kukubali uzembe wa wachache katika hili,” alisema.

Alisema bila nishati ya umeme wa uhakika utekelezaji wa MKUKUTA, au kufikiwa kwa MALENGO YA MILENIA haitawezekana na wala haitawezekana kufanikisha mpango wowote wa mapinduzi ama ya uchumi wala ya huduma.

“Kwa kasi ya ukuaji wa uchumi ya sasa ya takribani asilimia 7 kwa mwaka, uzalishaji wa umeme unapaswa kukua kwa zaidi ya asilimia 15 kwa mwaka. Mahitaji ya Umeme nchini ni zaidi ya megawati 1500 kwa mwaka, uwezo wetu ni kuzalisha megawati 1034 lakini kiasi kinachozalishwa ni megawati 690 tu kutokana na uchakavu wa mitambo na kupotea kwa umeme mwingi kwenye njia za kusafirisha.
Hali hii ni mbaya sana kwa uchumi na inahitaji mikakati ya lazima kushughulikia,” alisema Bw. Kafulila.

Kutokana na hali hii alisema ni lazima Watanzania wawe wakali inapotokea watu waliopewa madaraka wanashindwa kutoa majibu ya msingi kuhusu masuala nyeti kama umeme.

Msingi mkubwa wa tatizo la umeme Tanzania ni serikali kufumbia macho miradi ya umeme ya uhakika ambayo ingetoa majibu ya kudumu ya tatizo hili na badala yake imebaki inasimamia sekta hiyo kwa kudunduliza ikitumia mitambo ya kukodi ambayo kwa miaka sasa, tangu IPTL mwaka 1994 hadi Aggreko, Songas, Richmond, Dowans imekuwa ikinyonya vibaya uchumi wa Taifa ambapo asilimia 86 ya mapato ya TANESCO yanatumika kulipia umeme unaozalishwa na mitambo ya kukodi ambayo inazalisha takribani asilimia 45 tu ya umeme wote.

Alisema wakati Watanzania wakizungumzia mgawo wa umeme, pembeni wanakabiliwa na deni la zaidi ya bilioni 185 ambazo kwa uamuzi wa Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa (ICC) wanapaswa kuilipa kampuni ya Dowans, ambayo mpaka sasa serikali imekosa ujasiri kusema mmiliki wake ni nani lakini imekiri kushindwa kesi mahakama ya kimataifa.

“Mkataba ule ulikuwa ni wa miezi 24 na wenye thamani ya sh bilioni 172. Lakini kwa ukosefu wa uongozi na siasa duni ndani ya mfumo wa utawala wetu tunalipia sh bilioni 185 tena bila kupata umeme. Bilioni 185 zingetosha kuongeza 200MW za umeme kwenye grid ya Taifa lakini sasa zinakwenda kulipwa kizembe.

"Huu ni unyama usiovumilika kwa Watanzania maskini. Na ni unyama zaidi kwa wananchi masikini wa vijijini ambao  asilimia 98 hawajui radha ya umeme lakini kodi zao sasa zinakwenda kutumika kijinga kabisa,” alisema.

2 comments:

  1. Jamani habari za asubuhi. Tulishasema bila mabadiliko ya safu za viongozi wa juu watanzania tutaendelea kunyanyasika hadi kufa. Wanaoitetea serikali ya CCM sasa watuambae kwa kina mgao huu unatokana na nini??? Sio ufisaji??

    ReplyDelete
  2. Kwa kweli hii Tanzania inaboa kwakweli. Wametufanya wanaichi wadanganyika pure. Hivi hamouni aibu viongozi. Mnataka tulipe kodi then umeme ni wamgao, hayo mapato siye tutayapataje yataingiaje. wakati mchana hakuna umeme na kazi zetu zinahitaji umeme. Kodi itatoka wapi nyie viongozi, ufisadi tuuuu! mmezidi bwana, acheni. Ngeleja fuatilia hilo kwa makini.

    ReplyDelete