07 December 2010

Malalamiko ya wachinjaji yafanyiwa kazi

Na Rehema Mohamed

MANISPAA ya Ilala, Dar es Salaam, imeanza kushughulikia malalamiko yaliyotolewa wiki iliyopita na wachinjaji mifugo katika machinjio ya Vingunguti.Baadhi ya malalamiko hayo ni pamoja na uboreshwaji wa maeneo ya kuchinjia, choo, umeme na usafi wa
ndani katika machinjio hayo.

Akizungumza katika kikao na wafanyabiashara wa nyama kilichofanyika jana katika eneo la machinjio hayo, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Bw. Gabriel Fuime, alisema suala la umeme limeshugulikiwa kwa kununua jenereta mpya ambayo itazalisha umeme wakati wote.

Alisema tatizo la usafi pia limefanyiwa kazi kwa kuongeza idadi ya wafanyakazi ambao watafanya kazi hiyo pamoja na kukodisha magari 10 ambayo yatazoa mbolea iliyojaa ndani ya machinjio.

“Lengo letu ni kufanya ukarabati na kuboresha miundombinu yote ya machinjio kwani sehemu kubwa ya malalamiko haya, yametokana na machinjio kuzidiwa uwezo wa utoaji huduma.

“Awali machinjio haya yalikuwa kwa ajili ya kuchinja ng'ombe kati ya 18 hadi 20, hivi sasa idadi hiyo imeongezeka na ng'ombe wanaochinjwa kwa siku ni zaidi ya 300,” alisema.Katika mkutano huo, wafanyabiashara walikubaliana kuanzishwa kwa utaratibu wa vitambulisho kwa wafanyakazi, wachinjaji na wafanyabiashara wa nyama ndani ya machinjio.

Bw. Fuime alisema, vitambulisho hivyo vitawafanya watambuane, na kuahidi kukamilisha mpango huo, uvaaji viatu maalumu na kote nyeupe.
Wafanyabiashara hao, wameazimia upigwaji marufuku uuzwaji holele wa nyama kwa rejareja ndani ya machinjio, ubebaji wa nyama katika mifuko ya rambo, pikipiki na uuzaji wa mbuzi barabarani badala ya mnadani Pugu.

Malalamiko mengine ambayo yalitolewa na wafanyabiashara katika kikao hicho ni kwamba, wanapokwenda kulipia ushuru wa mifugo katika mnada wa Pugu, hulipishwa sh. 3,600 wakati risiti wanazopewa zikiandikwa sh. 600.

Malalamiko mengine ni kulipishwa sh. 2,500 ya ushuru wa uchinjaji katika machinjio hayo bila kupewa risiti. Bw. Fuime alipokea malalamiko hayo na kuahidi kuyafikisha wizarani.

1 comment:

  1. Kwa nini tunaendekeza utaratibu huu wa kusubiri mpaka kutokee matatizo, watu wagome, n.k. ndiyo hatua zichukuliwe? Hao viongozi wa Manispaa walikuwa wapi muda wote?

    Hizo hatua zinazodaiwa kuchukuliwa sasa hivi zimeazimwa wapi? Mbona hawajaacha kukusanya ushuru hata siku moja?

    Ni lazima tabia hii ikomeshwe! Viongozi wasiowajibika waondolewe kazini kwani hawana haki miliki ya kuhodhi ofisi walizo nazo. Tuache kuoneana aibu, tuache uswahiba kazini, tufanye kazi kwa maslahi ya watanzania.

    ReplyDelete