07 December 2010

CCK yajiunga kilio cha katiba

Na Zamzam Abdul

CHAMA Cha Kijamii (CCK), kimeandaa waraka ambao utachambua kasoro zilizopo kwenye katiba na kuzifikisha kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Bi. Celina Kombani ili aweze kutoa hoja rasmi kwa nini Tanzania inahitaji katiba mpya.Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa
Taifa wa chama hicho, Bw. Constantine Akitanda, alisema matatizo yaliyojitokeza katika uchaguzi uliopita, yalitokana na kasoro zilizopo kwenye katiba ambayo inatumika hivi sasa.

“Mambo mengi ambayo tumeyaona kuanzia muundo wa tume, usimamizi wa uchaguzi na utangazaji matokeo, yanahitaji kuangaliwa upya, haya yote yanaweza kusahihishwa na kutengenezwa vizuri kama katiba yetu itafanyiwa maboresho na kuandaliwa upya,” alisema.

Alisema chama hicho kipo mbioni kufanikisha lengo lake la kupata usajili wa kudumu ili kiweze kutoa mchango wa kifikra na kiuongozi nchini.

“Tumejipanga vizuri na tunaendelea kuwasiliana na Msajili wa Vyama vya Siasa ili kuhakikisha tunapata usajili wa kudumu, wanachama wapya pamoja na ofisi,” 'alisema Bw. Akitanda.

Amewataka wanachama wa chama hicho, kutoa ushirikiano wakati wote wa uhakiki ili usaili huo usikumbwe na matatizo yasiyokuwa ya lazima.
Alisema mbali ya kusubili mchakato wa kupata usajili, chama hicho kitaendelea kupiga vita vitendo vya ufisadi ambavyo bado vimekithiri nchini.
Bw. Akitanda alisema mfumo wa uchaguzi haukidhi mahitaji ya Taifa kuanzia uandikishaji, kuhesabu kura na kutangaza matokeo.

Msimamo wa chama hicho umekuja baada ya Bi. Kombani kusema kuwa hakuna haja ya kubadilisha katiba iliyopo kwa kuwa hakuna chama au kundi la watu ambalo limetoa madai rasmi ya kutaka katiba mpya.

2 comments:

  1. NDUGU ZANGU WATANZANIA WAZURI,katiba lazima ibadilike ili si tu kwamba twende na wakati, bali tupate mabadiliko ya kweli ambayo yanahitajika kwa watanzania wanaoendelea kuishi chini ya kadola ka moja huku idadi yao ikiongezeka kila kukicha.

    ReplyDelete
  2. MASHIRIKA YASIYO YA SERIKALI, VYAMA VYA SIASA NA WADAU WENGINE, TUSHIRIKIANE TUISHINIKIZE SERIKALI YETU IKUBALI KUBADILI KATIBA YA NCHI TUISHI KWA RAHA NA STAREHE. WATANZANIA HATUNA SHIDA NA AMANI KWANI AMANI TUNAYO NA ITAENDELEA KUWAPO TU, ILA TUNACHOHITAJI SANA NI MAENDELEO...UHAKIKA WA MAISHA BORA...KULA NA KUNYWA VIZURI...HILI LINAWEZEKANA TUKIBADILI KATIBA YETU.

    ReplyDelete