*Wachezaji watishia kugomea mazoezi
Na Elizabeth Mayemba
HALI imeonekana kuwa si shwari ndani ya Yanga, baada ya wachezaji wa timu hiyo kutishia kugoma kufanya mazoezi, endapo hawapalipwa fedha zao za usajili.Habari za uhakika zilizopatikana Dar es Salaam jana kutoka kwa
baadhi ya wachezaji hao zilidai kuwa wanadai karibu sh. milioni 70.
"Huo ndiyo utaratibu uliopo kwa kila mchezaji, pale anaposaini mkataba mpya hulipwa fedha zake za usajili, ambapo tunatakiwa kulipwa kwa vipindi vitatu, lakini tunashangaa kuona hatulipwi fedha zetu," alisema mmoja wa wachezaji wa timu hiyo ambaye hakupenda kuandikwa jina lake gazetini.
Alisema hii imekuwa ikiwakatisha tamaa mno, hali ambayo itawafanya wakose morali mazoezini na katika michuano inayowakabili.
Naye mchezaji mwingine ambaye pia hakutaka kutajwa jina, alisema kama hali hiyo ikiendelea hawaoni sababu ya kuendelea na mazoezi kwa kuwa hawana fedha.
Malalamiko hayo yameungwa mkono na mmoja wa viongozi wa klabu hiyo, ambaye alisema ni kweli wachezaji wanadai fedha zao za usajili na wametishia kugoma kuendelea na mazoezi endapo hawatalipwa.
"Kwa upande wetu hali kama hii si nzuri, hivyo tunafanya utaratibu wa kuona kama tutaweza kuchukua mkopo sehemu, ili tuwalipe wachezaji wetu," alisema kiongozi huyo ambaye naye aliomba asiandikwe jina lake.
Alisema watazungumza na wachezaji hao, ili wavute subira wakati uongozi ukishughulikia suala lao kwa haraka.
No comments:
Post a Comment