24 December 2010

Faru kulindwa kwa mitambo maalumu

Na Reuben Kagaruki

WIZARA ya Maliasili na Utalii itawawekea mitambo ya kisasa zaidi faru wanne waliobaki baada ya mwenzao kuuawa na majangili ili kuratibu mwenendo wa wanyama hao kila siku.Mbali na hatua hiyo, pia wizara hiyo
imesema itawapatia mbinu mpya askari wanaowalinda, zitakazowasaidia kukabiliana na uhalifu. Mikakati hiyo ilitangazwa Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Ladislaus Komba alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Alitaja mipango mingine ya wizara yake kuwa ni kuhakikisha faru hao wanalindwa kwa kujenga vituo vipya vya askari katika hifadhi hiyo, ili kupunguza ukubwa wa maeneo yanayokaguliwa na vikundi vya doria.

Faru huyo dume aliyepewa jina la George (12) ni kati ya watano walioletwa nchini kutoka Afrika Kusini Mei 21, mwaka huu na kuwaweka katika hifadhi ya Serengeti.

Faru hao walinununuliwa na familia ya Paul Tudor Jones, mwekezaji katika eneo linaloitwa Sasakwa lililopo wilaya ya Serengeti na mapori ya akiba ya Grumeti na Ikorongo na  hafla ya kuwapokea iliongozwa na Rais Jakaya Kikwete, ambaye alisema watapewa ulinzi mkali unaozidi wa rais.

Dkt. Komba aliwaambia waandishi wa habari kuwa tangu kuuawa kwa faru huyo msako wa kuwatafuta majangili uliohusika ulianzishwa  na uongozi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa kushirikiana na polisi kutoka Mugumu na kampuni ya Grumeti Reserves.

Alisema hadi kufikia Desemba 21 ,mwaka huu wafuatiliaji walifanikiwa kukamata watuhumiwa nane ambao hadi sasa wanaendelea kusaidia polisi.

"Katika kutafuta ushahidi wa silaha iliyotumika kuua faru huyo, chombo maalumu kilichotolewa na Franfurt Zoological Society kilitumika na kufanikiwa kupata kipande cha risasi ambacho kitasaidia katika uchunguzi," alisema Dkt. Komba.

Alisisitiza kuwa ulinzi wa faru hao na wanyama wengine umeimarishwa kwa kuongeza askari, magari na vitendea kazi muhimu kwenye maeneo yote yenye faru.Alisema wananchi wamehamasishwa ili washiriki kuwafichua wahalifu wanaotafutwa ambao walishiriki kuua faru hao.

"Wadau mbalimbali wameshirikishwa kuendeleza juhudi za kubaini mtandao wa wahalifu waliohusika na tukio hili," alisema. Faru hao baada ya kuuawa majangili walitoweka na pembe.

Alitoa mwito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na serikali kutoa ulinzi wa wanyamapori.

2 comments:

  1. kama kweli walipewa ulinzi kama wa rais, iweje wauauwe? mbona maswali ni mengi kuliko majibu, nahis kuna watu waliohusika ndani ya hifadhi humohumo. watuhumiwa wa kwanza wawe ni askari waliokuwa wanawalinda.

    ReplyDelete
  2. Sasa kama wanaliahidiwa watlindwa kama raisi iweje wauwawe au ilikuwa ni kauli ya kisiasa yaani siasa mpaka kwenye wanyama hii kweli BONGO na kama kweli alipewa ulinzi kama wa rais basi hayuna ulinzi TZ

    ReplyDelete