Na Tumaini Makene.
BARAZA la Mawaziri jipya chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete limekutana kwa mara ya kwanza, ambapo
rais ametumia fursa hiyo 'kuwafunda' wateule wake, huku akiuelezea mkutano huo kuwa ni utangulizi wa maandalizi ya semina elekezi.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana Dar es Salaam, Rais Kikwete alikutana na mawaziri wote 21 na manaibu wao 29, jana ikulu Dar es Salaam, akiwaambia kuwa katika kipindi hiki cha pili cha uongozi wake, hakutakuwepo na muda wa kupoteza wala hatakuwa tayari kukubali maelezo juu ya kushindikana kwa majukumu ya msingi.
Utaratibu wa kuwapatia mawaziri semina elekezi ulianza katika serikali ya Rais Kikwete, mwanzoni mwa awamu yake ya kwanza, ambapo mawaziri na manaibu wao wote walipiga kambi Hoteli ya Ngurdoto, huko Arusha, iliyofuatiwa na nyingine ya watendaji wa serikali.
Tangu mwanzoni utaratibu huo ulipokewa kwa namna tofauti na wananchi ambapo wapo waliohoji busara ya matumizi ya gharama kubwa ya serikali, hoja ambazo zimeendelea kuibuliwa mpaka awamu ya kwanza ya Rais Kikwete ilipokuwa ikifikia ukingoni, ikihojiwa tathmini na ufanisi uliotokana na semina elekezi hizo.
Taarifa hiyo kutoka Kurugenzi ya Habari ya Ikulu, ilisema kuwa Rais Kikwete alitumia kikao hicho cha kwanza kilichochukua masaa matatu kuliambia baraza lake kuwa suala la vita dhidi ya rushwa ni suala la kikatiba na kuwataka kuhakikisha kuwa Mpango wa Pili wa Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Rushwa (NACSAP-11) unatekelezwa.
Pia ameripotiwa kuwataka mawaziri kusimamia mapato ya Serikali yasiyotokana na kodi na kudhibiti matumizi ya Serikali, huku akiwakumba viongozi hao kuzingatia maadili ya uongozi ikiwa ni pamoja na kusimamia sheria za nchi, kuheshimu sheria katika shughuli na mambo yao binafsi na pia kutunza siri za Serikali kwa mujibu wa kiapo chao.
Alitumia pia fursa hiyo kuwapongeza kwa mara nyingine mawaziri na manaibu mawaziri hao akiwaambia kuwa wanastahili pongezi kwa kubahatika kuteuliwa kutoka katika orodha ndefu ya wabunge wenye sifa za kushika nafasi walizonazo, "nimewateua kwa imani kuwa pamoja nanyi, tutatimiza matumaini ya wananchi wa Tanzania waliokichagua Chama cha Mapinduzi kiendelee kuongoza nchi yetu.”
"Ni imani yangu kuwa kwa mshikamano na ushirikiano wetu kama timu moja ya ushindi, tutatekeleza majukumu yote kwa uadilifu, uaminifu na ufanisi wa hali ya juu. Ufanisi wa Waziri ama Naibu Waziri katika utekelezaji wa majukumu yake unategemea sana ufahamu na uelewa wake wa masuala muhimu yanayohusu nchi, serikali na wizara anayoiongoza.”
"Katika mkutano huo ambao ameuelezea kama wa utangulizi wakati inaandaliwa Semina Elekezi, Rais Kikwete amewaelezea wateule wake maana ya Baraza la Mawaziri na majukumu yake, na kutaka kila waziri ahakikishe anatayarisha kalenda yake ya masuala muhimu ambayo anataka yajadiliwe na Baraza la Mawaziri kwa mwaka," ilisema taarifa hiyo kutoka ikulu.
Taarifa ilizidi kueleza kuwa Rais Kikwete pia aliwaeleza wateule wake kuhusu wajibu wa mawaziri bungeni, akisisitiza kuwa ni wajibu wa kila waziri kuhudhuria vikao vyote vya bunge, na kuwa ndani ya bunge mawaziri wote wa Serikali lazima wawajibike kwa pamoja.
"Ni muhimu ieleweke kuwa kama ilivyo kwa maamuzi ya Baraza la Mawaziri, uwajibikaji wa mawaziri bungeni ni wa pamoja. Kwa hiyo, hoja ya serikali bungeni ni hoja ya mawaziri wote na siyo waziri anayewasilisha hoja tu,” amenukuliwa Rais Kikwete akiliambia baraza lake la mawaziri.
Rais pia amewakumbusha wateule wake kuhusu uwajibikaji wa pamoja (collective responsibility) katika kuongoza nchi, akisisitiza kuwa uwajibikaji huo unaelezwa kwa ufasaha katika Hati Maalum (Instrument) ya Majukumu ya kila Wizara.
Kuhusu uhusiano kati ya waziri na rais, na kati ya waziri na waziri mkuu, Rais Kikwete aliwaambia kuwa pamoja na kwamba shughuli zote za utendaji Serikalini hutekelezwa kwa niaba ya Rais, lazima mawaziri wakumbuke kuwa waziri mkuu ndiye msimamizi wa shughuli za kila siku za serikali.
Rais Kikwete pia aliwataka kuhusiana vizuri kati ya waziri na naibu waziri wake akisema kuwa mipaka ya kazi zao inapaswa kuheshimika, kuepusha migogoro na hivyo kuweka nguzo muhimu katika mafanikio ya wizara, huku akisema kuwa ni wajibu wa waziri kumpangia kazi naibu wake katika wizara husika.
Katika mkutano huo, Rais Kikwete pia amezungumzia uhusiano kati ya waziri na katibu mkuu; uhusiano kati ya waziri wa nchi asiyekuwa na Portfolio na Katibu Mkuu; uhusiano kati ya naibu waziri na katibu mkuu, na uhusiano kati ya waziri na waziri wa sekta nyingine.
Rais Kikwete pia alitumia fursa hiyo kufafanua uhusiano kati ya wizara na wadau wengine; uhusiano baina ya wizara, mikoa na halmashauri; uhusiano na taasisi zilizo zhini ya wizara; uhusiano na wasaidizi wa mawaziri pamoja na utekelezaji wa maagizo ya viongozi wa kitaifa.
Rais Kikwete pia aliwaeleza viongozi hao kuhusu nyaraka muhimu ambazo wanapaswa kukabidhiwa na kuzipitia watakapofika wizarani ambazo ni pamoja na Taarifa ya Makabidhiano ya Ofisi, Katiba, ilani ya chama tawala, dira ya taifa, Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA).
Rais Kikwete pia aliwaeleza wateule wake kuhusu umuhimu wa kufahamu sera, sheria, kanuni, taratibu, mikakati, mipangomkakati, mpango na bajeti ya wizara, mpango wa kazi wa wizara na masharti ya kazi ya waziri.
Rais Kikwete pia alisisitiza umuhimu wa viongozi hao kuwasiliana na wananchi kwa maana ya kueleza mafanikio ya serikali na mipango ya serikali katika kushughulikia matatizo ya wananchi, akiwakumbusha kuvitumia kikamilifu vitengo vya mawasiliano katika wizara zao ambavyo ndivyo vyenye jukumu la kutoa taarifa kuhusu wizara inavyotelekeza majukumu yake.
“Uzoefu unaonyesha kuwa mawaziri wengi ni wazito kufanya mawasiliano na wananchi hata pale ambako wizara imefanya mambo mengi mazuri. Hivyo, mawaziri muwe mstari wa mbele kuelezea mafanikio ya utendaji wa serikali katika wizara zetu,” amenukuliwa Rais Kikwete akisema na kuongeza:
“Lazima ujengwe utamaduni wa kudumu wa kuwasiliana na wananchi wote ambao ndio waajiri wetu kupitia kura zao. Mawaziri wote tumieni Vitengo vyenu vya Mawasiliano na vyombo vya habari kwa ustadi ipasavyo,” amefafanua Rais Kikwete.
Huu ni utumizi wa fedha usio wa lazima...ndo ufisadi sasa huu! Kuna haja gani ya kuwaelekeza watu ambao wameshawahi kuwa Serikalini humohumo tena wengine Wizara hizohizo? Yaani Rais Kikwete ndo ameona huo aufanyao sasa ni utekelezaji wa majukumu yake.Sisi hatukuchagua mwalimu,tumechagua Rais.Ualimu wake wa Monduli auache hukohuko.Kila mtu ameshakabidhiwa vitendea kazi ,basi.Kama kila mwajiri angefungua darasa la hivyo la kufundisha hata vitu vya kawaida kama hivyo,kusingekuwa na maendeleo yoyote kwenye kazi.Waziri yupi alikuwa hajui uwajibikaji maana yake nini? Alipewaje Uwaziri sasa? Sio usanii huu? Hizi Semina elekezi zinakula mabilioni ya pesa.Badala ya wao kuanza kufanya kazi za kimaendeleo na kutumia fedha zilizopo kutekeleza ilani yao ya CCM,wanakaa vikao visivyo na maana kupeana posho tu hawana lolote.Nasisitiza CCM hawana jipya.Siku chache tu baada ya wao kuapishana,soda imepanda bei mitaani kwetu..sasa shilingi 600.Hawa hawana jipya.Wakimaliza hapo Ikulu watakwenda kuzitafuna hela zetu Ngurudoto au hata Ngurukurwa mwaka huu.Muda mwingi kuambiana tuuuuuuuuu kazi hakuna.Mmeshaanza usanii eeeh? Mtajiumbua wenyewe mwaka huu...wapinzani wataingia kipindi cha pili kumalizia mpira.Kwakuwa mmeshaanza ubadhiifu,sisi yetu macho na masikio.
ReplyDeleteHii semina ni muhimu sana kwa maziri hasa mawaziri wapya ili wapate kuelewa cha kufanya. Hakuna kozi ya uwaziri lakini waziri anahitajika kufanya majukumu yake viziri hiyo ni muhimu kwa rais ahakikihe mawaziri wote wawe na common understanding - Abdallah Bakari
ReplyDeleteMselewa - mbona una mawazo hayo. Mwajiri yeyote mwenye ujuzi ni lazima amfundishe yule mfanya kazi mpya taratibu za kazi na ushirikiano n.k. Mawaziri wanahitaji kuelezwa majukumu yao,maadili ya kazi, sera mpya zikavyofanya kazi na kadhalika. Hapo hakuna ubaya. Kumbuka kwamba hakuna Chuo kinachofundisha Uwaziri.Pia wanahitaji kuelezwa mipaka yao ili pasiwe na mgongano. MA
ReplyDelete