30 November 2010

CHADEMA yaonya CCM kuhusu azimio la kuwatimua.

Na Mwandishi wetu.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo kimetoa tahadhari kwa Chama Cha Mapinduzi, dhidi ya hatua yoyote ya kutumia mabavu badala ya sheria au kanuni, kuwafukuza bungeni wabunge
wake, baada ya kususia hotuba ya Rais Kikwete wakati akizindua bunge hivi karibuni.

Tahadhari hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi wa Haki, Sheria na Katiba wa CHADEMA, Bw. Tindu Lissu baada ya Majira kumuuliza chama chake kimejipanga namna gani kukabiliana na hoja ya kusudio la CCM kutaka wabunge wa CHADEMA wafukuzwe bungeni.

Hivi karibuni Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM, Bw. John Chiligati alinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari akisema kuwa chama chake kinakusudia kuwasilisha bungeni hoja ya kulitaka bunge kupitisha azimio la kuwafukuza wabunge wa CHADEMA, kwa 'kosa' la kususia hotuba ya rais bungeni.

Mbali ya kulaani uamuzi huo wa wabunge wa CHADEMA, Bw. Chiligati alisema kuwa kitendo chao ni uasi na uhaini dhidi ya demokrasia na utawala wa nchi.

Lakini Bw. Chiligati na hata viongozi wengine ambao wamejitokeza kulaani kitendo hicho, hawakutaja kifungu chochote cha sheria ya nchi wala kanuni ya bunge iliyovunjwa inayoweza kusababisha uasia na vurugu nchini, kama alivyodai katika taarifa yake.

Jana Majira lilitaka kujua CHADEMA wamejipanga vipi iwapo CCM wataweza kufikisha hoja yao bungeni na kutimiza kusudio lao kama ilivyowahi kutokea wakati alipofukuzwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Kabwe Zitto mwaka 2007 na hata juzi ambapo bunge lilikwepa kanuni inayosema kabla bunge halijamthibitisha waziri mkuu mteule, lazima mkuu wa kambi ya upinzani apewe nafasi ya kujadili.

Akizungumzia suala hilo, bw. Lissu alisema, "Wajaribu tu waone, wajaribu kutumia mabavu waone nini kitatokea, na ni vizuri pia wakajikumbushia nini kilitokea walipomfukuza Zitto bungeni, kisha wafikirie nini kitatokea iwapo wabunge 48 wa CHADEMA watafukuzwa bungeni, walete tu hiyo hoja tunasubiri.

"Wanajua hatujavunja kanuni wala sheria yoyote...hata ukikiuka kanuni ya bunge sheria inasema adhabu ya kwanza ni kuzuiwa kikao kimoja cha bunge...sasa kama hatujavunja sheria wala kanuni watatukamatia wapi, labda watunge sasa hivi hizo kanuni, hata kama wakitunga wataweza kuzirudisha nyuma?

"Wakitaka kufanya mambo kiharamia haramia wanaweza, lakini matokeo yake yatakuwa mabaya sana, labda watunge sheria sasa kuwa kumsusia rais ni kosa lakini hawataweza kurudisha nyuma ili zianze kufanya kazi," alisema Bw. Lissu ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni.

Baadhi ya wanasheria nchini akiwemo Mwanasheria Mkuu wa Serikali na aliyekuwa spika wa bunge la tisa, Bw. Samuel Sitta wamepata kunukuliwa katika vyombo vya habari wakisema kuwa kitendo cha CHADEMA cha kususia hotuba ya rais hakivunji sheria wala kanuni yeyote nchini, ingawa wote wawili hawakiungi mkono.

Kwa upande wao CHADEMA wamekuwa wakinukuliwa kwa nyakati tofauti juu ya msimamo wa chama chao baada ya kumsusia Rais Kikwete bungeni, wakisema tatizo si kumtambua au kutomtambua rais, bali mchakato uliomweka madarakani una mshikeli, wakisema matokeo ya kura yalichakachuliwa.

Wamekuwa wakikubali kuwa kwa mujibu wa katiba na sheria zilizopo, Rais Kikwete ni rais halali, lakini wamekuwa wakimfananisha na marais wa nchi zingine ambao huweza kupata urais bila ridhaa ya wananchi au kwa michakato isiyokuwa halali, lakini wakishachukua dola wanatambulika kikatiba na kisheria, lakini bado njia walizotumia zinakuwa si sahihi.

Wamekuwa wakisema kuwa kwa jinsi sheria za nchi zilivyo sasa, kwa kuzingatia makosa yaliyojitokeza wakati wa uchaguzi, Rais Kikwete amewekwa madarakani na Tume ya Uchaguzi (NEC), kwani ndiyo pekee yenye mamlaka ya kumtambua na kumtangaza mshindi wa urais, huku haki ya kuhoji ushindi huo kisheria mahakamani ikiminywa.

Wachambuzi wa mambo ya kisiasa wamekuwa wakiona uamuzi wa CHADEMA kumsusia rais ni ukuaji wa demokrasia wa hali ya juu; lakini wao wakisema ni kitendo cha kudai haki kwa amani, huku wakipeleka ujumbe mzito kwa wananchi na jumuiya ya kimataifa, juu ya mfumo mbovu wa usimamizi wa uchaguzi na umuhimu wa katiba mpya nchini.

4 comments:

  1. pETRO eUSEBIUS mSELEWANovember 30, 2010 at 9:38 AM

    CCM ndo zao kutishia nyau.Chiligati kawaita wenzake wahaini halafu yeye ndiye 'waliyemhaini' kwenye uwaziri.Kujua Sheria ni tunu kubwa sana.Chadema wana Wanasheria mahiri sana ndani na nje ya Bunge.Nje ya Bunge yuko Mh.Mabere Nyaucho Marando.Ndani wapo akina Mh.Tundu Lissu na Mustapha Akonaay.CCM wasitegemee eti CHADEMA watakurupuka au walikurupuka kuamua jambo bila kupitia Sheria za nchi.Lissu kiboko katika medani yetu hii.Marando ndo usiseme.Najivunia sana kusoma na Mh.Marando katika Shule moja(katika wakati tofauti)ya Songea Boys.Hata 'Msongea Boys' mwenzake,Jaji Mkuu Mstaafu,Mh.Barnabas Samatta anamfahamu vyema.CCM waandike wameumia..ni sheria tu kwenda mbele.Kuhoji,kudai,kukwepa,kukosoa,kukubali,kupembua,kuumbua na kukataa kwa CHADEMA kutafuata Sheria.Subira yavutwa na heri!

    ReplyDelete
  2. Jaji Mkuu alidai kwamba CHADEMA hawajavunja Sheria yoyote, sasa watawafukuza kwa Sheria ipi wandugu? Pia CHADEMA sidhani kama walilitambulisha rasmi Bunge kwamba "hawamtambui" Rais na kama hawajafanya hivyo kwa nini wanafanyia kazi taarifa za kwenye magazeti?

    ReplyDelete
  3. Mini nadhani kuna watu wanafikiri wanapokuwa viongozi wa CCM katika ngazi ya juu, ambapo wameupata kwa ushirikina, wanadhani ndiyo mwisho wa yote na wanasahau kuwa mpanda ngazi hushuka. Wambulu wa Manyara wanafahamu sana kilichompata Marmo mwaka huu!!

    ReplyDelete
  4. Huyo aliyesoma ha hawa wanasheria yeye ana nini kama siyo domo kaya kwenye magazeti? Ina maana chadema kazi yao ni kufuatilia na kufanyia kazi kila kinacho andikwa magazetini hata kama ni uchochezi? Yeye kama wao ni wanasheria, je, na yeye ni mwanasheria? Mbona ana lugha ya uchokozi na uchochezi. Ina maana CCM hawana wanasheria? malumbano yametuchosha, tunataka utendaji, kila mfa maji haachi kutapatapa hilo tunalijua tangu zama. Mtawapa watu faida kwa kusoma maugomvi hadi lini? Madomo kaya hawa ndio vichochezi imara nchini. Wao wakipewa uongozi, wanataka kusema ndiyo watafanya maisha ya watanzania wote yabadilike within a fortnight? Wengine wanao andika hawana hata morals, hawana ethics, hawana discipline, hawana diplomacy,wana zero tolerance, too vocal na wanaandika hovyo hovyo tu na hivyo kukifanya chama cha chadema kuonekana ni cha wapika majungu usiku na mchana.

    ReplyDelete