Na Amina Athumani
KOZI ya ukocha wa mpira wa kikapu, inatarajia kuanza leo katika viwanja vya Donbosco, Dar es Salaam ambayo itaendeshwa na mkufunzi kutoka Shirikisho la Kimataifa la
mchezo huo (FIBA) raia wa Kenya, Samwel Wanjohi.
Akizungumza kwa simu Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Alexanda Msofe alisema tayari mkufunzi huyo amewasili juzi usiku kwa ajili ya kuendesha kozi hiyo.
Alisema kozi hiyo imeandaliwa na TBF Kwa kushirikiana na FIBA Afrika na kwamba hiyo ni programu, inayoendeshwa na vyama vyote wanachama wa FIBA kwa lengo la kutaka kila mwanachama kuwa na maendeleo mazuri ya kufufua vipaji vipya vya mchezo huo.
Msofe alisema kozi hiyo itashirikisha makocha 26, kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania ambapo washiriki wake ni wale waliohitimu kozi ya awali ya ukocha ya Modulle 1, iliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Alisema kozi hiyo itawawezesha makocha hao kutoa mafunzo ya kinadharia na vitendo katika mikoa watakayokwenda kwa ajili ya kufundisha makocha wengine wasiokuwa na elimu ya ukocha ya mchezo huo na pia itasaidia kuibua vipaji vingi zaidi.
No comments:
Post a Comment