01 December 2010

Kesi ya CHADEMA kupinga matokeo Desemba 20

Na Suleiman Abeid, Shinyanga

HATIMAYE Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Shinyanga kimefungua kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi ya
kiti cha ubunge  wa Jimbo la Shinyanga mjini yaliyomtangaza mgombea wa CCM Bw. Steven Masele kuwa ndiye mshindi.

Akizungumza na Majira kwa njia ya simu akitokea mkoani Tabora jana, Katibu wa CHADEMA mkoani Shinyanga, Bw. Nyangaki Shilungushela alisema kesi hiyo ilifunguliwa
juzi katika mahakama  hiyo.

Bw. Shilungushela alisema washtakiwa katika kesi hiyo ni Mkurugenzi wa Uchaguzi, Mwanasheria wa serikali na Bw. Steven Masele ambaye kwa sasa ni mbunge wa Jimbo la Shinyanga mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katibu huyo alisema kesi hiyo inatarajiwa kuanza kutajwa kwa mara ya kwanza katika mahakama hiyo Desemba 20, mwaka mwaka huu na kwamba CHADEMA katika kesi hiyo
itawakilishwa na wanasheria wake ambao pia ni mawakili wa kujitegemea nchini, Bw. Mabere Marando na Bw. Tundu Lissu.

Uamuzi wa CHADEMA kwenda mahakamani unatokana na kutoridhishwa na matokeo ya ubunge yaliyotangazwa na msimamizi msaidizi wa uchaguzi katika Jimbo la Shinyanga mjini, Bw. Festo Kang’ombe ambaye alidai kuwa mshindi katika uchaguzi huo ni mgombea wa CCM aliyepata kura 18,570 dhidi ya kura 18,569 alizopata mgombea wa CHADEMA, Bw. Philipo Shelembi.

Hali hiyo ilisababisha mtafaruku mkubwa miongoni mwa wanachama na wapenzi wa CHADEMA ambao walidai kura za mgombea wao zilikuwa zimechakachuliwa kwa lengo la kumtangaza mgombea wa CCM kuwa ndiye mshindi ambapo Jeshi la polisi lililazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya watu walioingia mitaani kupinga matokeo hayo.

1 comment:

  1. pETRO eUSEBIUS mSELEWADecember 1, 2010 at 9:24 AM

    Kwakuwa kesi ya CHADEMA itasimamiwa na waheshimiwa Mabere Marando na Tundu Lissu(Mb),haki itatendeka kwakuwa hawa wataieleza na kuisadia Mahakama kile kinachopasa kuonekana na kuelezwa.Kila la kheri CHADEMA katika harakati zenu za kudai haki kwa njia stahiki.Itadhihirika kama ni kweli mshindi alikuwa aliyetangazwa na kwa tofauti hiyo ya kura moja! Kama ulikuwa ni usanii wa CCM tutaambiwa na Mahakama yetu tukufu.Subira yavutwa na kheri!

    ReplyDelete