30 November 2010

Baraza la Kikwete kubwa-FemAct.

Na Flora Amon.

MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) ukishirikiana na mashirika mengine 50 yanayotetea usawa wa kijinsia, haki za binadamu na ukombozi wa wanawake kimapinduzi (FemAct) umesema
kuwa baraza la mawaziri la awamu ya tano limekuwa kubwa tofauti na baraza lililopita ambapo ongezeko lake sawa na asilimia 12.

Ongezeko la ukubwa wa baraza hilo, wamesema ni kitendo kinachoonesha dhahiri kuwa bado changamoto zilizokuwepo katika serikali iliyopita zitaendelea, mfano matumizi na makubwa katika uendeshaji wa serikali hayatapungua.

Katika taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari jana na kusainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Bi. Lilian Liundi imesema kuwa pamoja na wanaharakati hao kufurahishwa na uteuzi huo, idadi ya wanawake walioteuliwa kuwa mawaziri katika baraza ni ndogo tofauti na baraza lilopita.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo jumla ya mawaziri 29 waliteuliwa kati ya hao wanaume ni 22 sawa na asilimia 76 na wanawake ni wanane, sawa na asilimia 24.

Manaibu mawaziri wapo 21 ambapo wanaume ni 18 sawa na asilimia 86, na wanawake ni watatu sawa na asilimia 14 ambapo hao walitarajia kuwa kipindi muafaka cha kufikia asilimia 50 kwa 50, haikufikia hatua hiyo.

Taarifa hiyo ilisema kuwa hao kama wana-FemAct walitarajia pia ukubwa wa baraza hili ungepunguzwa ili  kusaidia kusukuma na kubana rasirimali zaidi kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi wote wanawake kwa wanaume, wazee kwa vijana, watu wanaoishi na changamoto za ulemavu, VVU na Ukimwi na wote waliotengwa pembezoni sambamba na usimamizi wa rasirimali za taifa na usimamizi wa utawala bora na uwajibikaji kwa mtazamo wa kijinsia.

Taarifa hiyo ilisema kuwa FemAct ina imani kabisa kuwa huu ni wakati mzuri wa kuangalia upya sera ya soko huria na kuanza kutafakari mfumo wa uchumi mbadala na kuhakikisha wananchi wote wanashiriki na kufaidi rasilimali za nchi.

1 comment:

  1. wanawake atawapa ukuu wa wilaya kama ilivyo kawaida yake.

    ReplyDelete