22 October 2013

SIMBA, YANGA ZAINGIZA MIL.500/-



Na Fatuma Rashid

  Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) ya watani wa jadi Simba na Yanga iliyochezwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya mabao 3-3, imeingiza sh.milioni 500,727,000.


Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema kuwa katika mechi hiyo mashabiki walikuwa ni 57,422 ndiyo waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo namba 63 kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.

  Wambura alisema kuwa tiketi 131 hazikuuzwa ambazo ni 90 za VIP A, 40 za VIP B na moja ya VIP C ambapo tiketi zilizochapwa kwa ajili ya mechi hiyo ni 57,558 ambayo ndiyo idadi ya viti vilivyopo kwenye uwanja huo.

  Alisema kuwa mapato hayo yaligawanywa ambapo kila klabu ilipata mgawo wa sh. milioni 123,025,564.32 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 76,382,084.75.

  Wambura aliongeza kuwa mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 62,555,371.69, tiketi sh. 7,309,104, gharama za mechi sh. 37,533,223.01, Kamati ya Ligi sh. 37,533,223.01, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh.18,766,611.51 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 14,596,253.39.

No comments:

Post a Comment