20 August 2013

VIGOGO DECI CHINI YA ULINZI

Watuhumiwa waliotiwa hatiani kwa makosa ya kupokea fedha kupitia taasisi isiyo halali ya DECI, kinyume cha sheria wakiwa chini ya ulinzi mara baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 3 jela na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana. Washtakiwa hao ni Jackson Mtares, Dominick Kigendi, Timotheo ole Loitignye na Samwel Sifael Mtares


Na Rehema Mohamed
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana imewahukumu kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya sh. milioni 21 kila mmoja vigogo wanane kati ya watano wa Kampuni ya Development Entrepreneurship for Community Initiative (DECI), iliyokuwa ikiendesha na kusimamia mchezo wa upatu.

Mahakama hiyo pia imeamuru Serikali kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ifanye utaratibu wa kurudisha fedha zote za taasisi hiyo zilizothibitika mahakamani kuwa zilitokana na mchezo huo kwa wanachama waliopanda (fedha) zao DECI.
Fedha hizo zinakadiriwa kuwa zaidi ya sh. bilioni 10 zilizokuwa zimehifadhiwa katika akaunti na benki mbalimbali nchini.
Akisoma hukumu hiyo kwa niaba ya Hakimu Stuwart Sanga aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, Hakimu Aloyce Katemana, alisema upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili washtakiwa na kuwatia hatiani.
Aliwataja watuhumiwa waliotiwa hatiani kuwa ni Jackson Mtares, Dominick Kigendi, Timotheo Ole Loitignye na Samwel Sifael Mtares ambapo mshtakiwa Arbogast Kapilimba aliachiwa huru baada ya mahakama kushindwa kumtia hatiani katika mashtaka yote mawili yaliyokuwa yakiwakabili.
Hakimu Katemana alisema, katika shtaka la kwanza washtakiwa hao watatumikia adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya sh. milioni 3 kila mmoja.
Shtaka la pili watatumikia kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya sh.milioni 18 kila mmoja na kwamba adhabu zote zitakwenda pamoja.
Alisema ushahidi ulioletwa mahakamani hapo ulithibitisha kuwa washtakiwa hao walijihusisha na biashara ya kupokea fedha kutoka kwa wananchi kinyume cha sheria licha ya BoT kuwakataza kufanya hivyo.
Aliongeza kuwa, washtakiwa hao ambao ni Wachungaji wa Kanisa la Pentekoste, wakati wakitoa utetezi wao walikiri kosa hilo na kudai walifanya hivyo wakiwa na lengo la kuwakwamua waumini wao kutoka katika lindi la umaskini.
Alidai ilithibitika kuwa DECI haikuwa na biashara nyingine ya kuongeza kipato cha kuwawezesha kupata faida ya kuwalipa wanaopanda mbegu.
Hata hivyo, mshtakiwa Mtares na Loitignye, walifanikiwa kulipa faini ya sh. milioni 21 kila mmoja na kunusurika kwenda jela.
Kabla ya kusomwa hukumu hiyo, wakili wa Serikali Prosper Mwangamila, alisema ni rai ya upande wa mashtaka kuwa mali, magari, viwanja, nyumba na fedha zote zilizoshikiliwa katika kesi hiyo zinastahili kutaifishwa.
Alisema kuendesha biashara ya upatu na kupanda mbegu vyote ni makosa kisheria hivyo wote hawastahili kufaidika na mali hizo zilizotokana na biashara hiyo.
“Mheshimiwa hakimu, makosa ambayo watuhumiwa wametiwa hatiani yalikuwa na madhara makubwa kwa uchumi wa nchi yetu hivyo naomba mahakama yako itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwao na wengine wanaofikiria kufanya biashara hii,” alisema.
Kwa upande wake, wakili aliyekuwa akiwatetea washtakiwa hao, Hudson Ndusyepo, aliiomba mahakama hiyo iwape adhabu ndogo wateja wake kwani walitenda kosa hilo kwa kutojua sheria na walikuwa na nia njema katika uanzishwaji wa biashara hiyo.
“Kwa sababu washtakiwa hawana rekodi ya mashtaka huko nyuma, naomba wapewe adhabu ndogo kwa huruma ya mahakama yako kwani msukumo wa kufanya biashara hii ulikuwa kuwakomboa waumini wao katika lindi la umaskini,” alisema Bw. Ndusyepo.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kuendesha na kusimamia mradi wa upatu kinyume na kifungu 111A(1,3) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16.
Ilidaiwa kuwa, kati ya mwaka 2007 na Machi 2009, katika Makao Makuu ya DECI, yaliyopo Mabibo Mwisho, Dar es Salaam, washtakiwa waliendesha na kusimamia mradi wa upatu katika sehemu tofauti nchini kwa ahadi ya kuwapa wanachama wake fedha zaidi.
Fedha walizokuwa wakitoa kwa wanachama ni nyingi kuliko mradi waliokuwa wakiufanya.
Shtaka la pili ni kupokea amana za umma bila kuwa na leseni kinyume na kifungu cha 6(1,2) cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha namba 5 ya mwaka 2006 na kwamba, washtakiwa wote katika kipindi hicho, wakiwa kwenye Ofisi zao za DECI, walipokea amana kutoka kwa umma bila leseni.
DECI iliwanufaisha watu wengi hasa waliojiunga mwanzoni na baadaye kuibuka malumbano kati yao, Serikali na wanachama waliopinga hatua ya Serikali kusitisha shughuli zake kwa madai kuwa haiko kihalali.
Kusimamishwa kwa shughuli za DECI, kulitokana na uamuzi wa BoT kutoa taarifa ya kuw

2 comments:

  1. Mimi jina langu ni Regina Edward nilikuwa ni mmoja wa wanachama wa DECI. Naomba Serikali itufikirie kuturudishia pesa zetu, kwani tulifanya hivyo pia ni katika kujikwamua toka katika hali ngumu ya maisha.

    Serikali kwa kutoturudishia pesa hizo ambazo tumeambiwa zipo Benki Kuu. Ni kutumaliza kabisaa.

    Tunaomba sisi wanachama utaratibu ufuatwe ili tuweze kurudishiwa pesa zetu jamani. Na hasa sisi wanawake wajane tuna watoto wanahitaji kwenda shule na matibabu.

    Asante hili ndio ombi langu kwa Serikali. Kwani taarifa za leo zinaonesha Serikali haitorudisha pesa hizo jamani!!!

    ReplyDelete
  2. SERIKALI IPO IMESIKIA.shida utekelezaji tu. pole sana ndugu.

    ReplyDelete