20 December 2012
Mwanamke apasuliwa kichwa na mchi
Na Severin Blasio, Morogoro
WATU wanne wamefariki dunia mkoani Morogoro katika matukio tofauti likiwemo la mwanamke mmoja kupasuliwa kichwa na mke mwenzake kwa mchi wa kutwangia wakati wakigombea mali.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Faustine Shilogile, alimtaja mwanamke aliyeuwawa kuwa ni Joyce Masasila (21), mkazi wa Mlimba, wilayani Kilombero.
Alisema tukio hilo limetokea juzi saa mbili usiku katika Kitongoji cha Mfiliga, ambapo mwanamke aliyesababisha mauaji hayo ni Bi. Magreth Ngasa.
Aliongeza kuwa, kifo hicho kilisababishwa na ugomvi uliotokea kati yao ambapo marehemu alikuwa akimtambia mtuhumiwa kuwa hana kitu chochote katika nyumba anayoishi.
“Maneno hayo yalimtia hasira mke mwenzake hivyo aliamua kuchukua mchi wa kutwangia, kumpiga nao kichwani na
kusababisha kifo chake papo hapo,” alisema.
Kamanda Shilogile alisema, mtuhumiwa anashikiliwa polisi na atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
Katika tukio jingine, mkulima na mkazi wa Kijiji cha Didimuka, kilichopo Kata ya Lundi, Tarafa ya Matombo, wilayani Morogoro,
Sababu Abdallah (40), amefariki dunia baada ya kuangukiwa na
mti wa msufi.
Tukio hilo limetokea juzi, saa tisa alasiri kijijini hapo ambapo chanzo cha kifo hicho ni upepo mkali ulioambatana na mvua
ambao uliangusha mti huo na kusababisha kifo chake.
Kamanda Shilogile alisema, katika tukio hilo watu wawili walijeruhiwa Bi. Mariam Husen (mke wa marehemu) alieyepata jeraha kichwani na Mwimb Athumani ambaye alivunjika mguu.
Katika tukio la tatu, mkazi wa Wilaya ya Gairo, mkoani humo,
Idd Shaban (17), amefariki dunia baada ya pikipiki aliyokuwa akiendesha yenye namba za usajiri T140 BFS, aina ya Sun Lg,
kupoteza mwelekeo, kugonga mti na kusababisha kifo chake.
Tukio hilo lilitokea juzi, saa 12 jioni, katika eneo la Chogoali ambapo chanzo cha ajali ni mwendo kasi wa marahemu.
Wakati huo huo, mwanafunzi wa darasa la nne, Winfrida Charlse, amefariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na gari yenye namba za usajiri T 769 BEX, aina ya Steer Tipa mali ya Kampuni ya CCECC ya Dar es Salaam, inayotengeneza barabara ya wakati akiendesha baiskeli.
Kamanda Shilogile alisema, tukio hilo limetokea juzi, saa mbili asubuhi katika eneo la Mkindo Darajani, Barabara ya Turiani- Morogoro na chanzo cha ajali ni mwendo kasi wa dereva wa
gari ambalo lilikuwa likiendeshwa na Bw. Brayson Paulo (40),
mkazi wa Kihonda Manispaa ya Morogoro iliyokuwa ikitokea Turiani kwenda Morogoro.
Alisema marehemu aligongwa na gari hiyo akiwa gurioni na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Chiaz Turiani na dereva anashikiliwa polisi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment