20 September 2012

Tushirikiane kukomesha mauaji ya vikongwe



Na Rabia Bakari

TANZANIA imekuwa ikikumbwa na mikasa kadhaa ya kutisha na ukatili, inayofanywa na baadhi ya watu wenye tamaa ya mali na wasiojali utu wa wenzao.

Mikasa hiyo ni pamoja na uchunaji ngozi za watu, mauaji ya kutisha na unyofoaji wa viungo vya binadamu, mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi na mauaji ya vikongwe.

Unyama huo hutokea kwa sababu moja ama nyingine lakini sababu kubwa ni tamaa ya mali, ambayo imesababisha nchi hii ya kidiplomasia kuingia kwenye doa kubwa hata kutishia baadhi
ya wageni kuogopa kutembelea, ushahidi ninao.

Lakini pamoja na hayo yote, vyombo vya dola na serikali kwa ujumla, vyombo vya habari, wanaharakati na jamii imekuwa mstari wa mbele kusimama na kupiga kelele sambamba na kuchukua hatua stahiki ili kukomesha vitendo hivyo.

Juhudi hizo zimefanikisha baadhi ya mauaji ya kinyama kupungua kama sio kukoma kabisa, mauaji hayo ni pamoja na ya watu wenye ulemavu wa ngozi, uchunaji wa ngozi za watu pamoja na unyofoaji wa viungo vya binadamu.

Ila, kilichofanya nishike kalamu leo hii ni mauaji ya vikongwe ambayo, pamoja na juhudi zinazofanywa na serikali na vyombo vyake vya dola, jamii na wanaharakiti wa haki za
binadamu juu ya mauaji hayo yamezidi kutikisa, kiasi cha kuonekana kama uzee ni laana.

Ni juhudi ndogo kutokana na ukweli wa jambo lenyewe, kwani iko wazi hata katika vyombo vyetu vya habari.

Kumekuwa kukiripotiwa kuhusu mauaji ya wazee hasa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa imani ya kishirikina, lakini hakuna ufuatiliaji wa kina wala kujua mamlaka husika zimechukua hatua gani juu ya jambo hilo.

Hali hiyo imezidi kuwapa nguvu wauaji kiasi cha mauaji hayo kuendelea kana kwamba wanaokufa ni 'kuku' ama 'wanyama wasio na thamani yoyote' na jamii kubaki kusikitika bila kuchukua hatua madhubuti.

Tumeshuhudia mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yakipewa kipaumbele na mikakati lukuki ya kukomesha na kweli yakapungua na hata sasa kutosikika sana, kwanini juhudi hizi
zisitumike na katika mauaji ya vikongwe?

Swali la kujiuliza ni kwamba huyo mzee hakua mchawi ujana wake wote? Kwanini aonekane mchawi akishazeeka? Na huyo anaua wazee kwa kigezo hicho, kibali kapata wapi? na yeye ni
nani na kwanini?

Kibaya zaidi, wazee hawa si tu wanauwa, bali wanauawa kinyama, kwa kucharangwa mapanga, kuchinjwa kama kuku na udhalilishaji usio na kifani? Kwanini? Ni ushirikina huo ama
kuna ajenda nyingine ndani yake?

Wengine wamekuwa wakipata vitisho vya kuhama vijiji ama kutotoa siri yoyote inayohusu mauaji hayo, kiasi cha kusababisha ukimya usio na tija na unaochangia mauaji hayo kuzidi kwa kasi kubwa.

Lakini ukweli uliopo ni kwamba hakuna wa kuwalinda wazee hawa kikamilifu, na ndio maana matukio hayo yanakuwa endelevu.

Wapo wanaharakati wachache na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayojaribu kujitolea na kuhakikisha angalau mauaji hayo yanakuwa historia, lakini juhudi hizo bila wadau muhimu
ni sawa na hakuna.

Shirika lisilo la kiserikali la Helpage International kwa kiasi kikubwa limejitahidi kusimamia haki za wazee sambamba na kuwaleta pamoja ili kuangalia namna gani matatizo ya
wazee yatasimamiwa ili kupungua kama sio kwisha kabisa.

Katika mkutano wao hivi karibuni uliowakutanisha wazee na wanahabari ndipo nilipopata fursa ya kugundua mengi yaliyojificha nyuma ya mauaji ya wazee hao, na wengine kutoa ushuhuda wa kunusurika kufa, sambamba na kupokea barua za  vitisho kutoka kwa wauaji. 

Maelezo na simulizi za wazee hao zilifanya nijisikie vibaya mno, kwani nikiwa kama kijana nami nina wazazi ambao wanazidi kusogea kwa kasi katika kundi hilo la uzee.

Akisoma azimio hilo kwa niaba ya wazee wengine, Bi. Theresa Minja kutoka Taasisi ya Mtandao wa Kinga Jamii anataka hatua madhubuti kukomesha mauaji ya wazee zichukuliwe.


Anasisitiza kuwa ikiwezekana kuliko hata zilizochukuliwa wakati wa kupambana na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.

Waandishi nao kwa upande wetu, tujitokeze na kupambana na mauaji hayo kwa kalamu kama ambavyo tumekuwa mstari wa mbele siku zote kupambana na udhalimu unaofanywa na watu mbalimbali katika taifa hili, na mfano mzuri ni mapambano baada ya kutokea mauaji ya mwandishi marehemu David Mwangosi.

Kalamu zetu zina nguvu, tamko la wazee hili lituguse wote, tufanye kazi kwa nguvu zetu zote ili kutetea haki ya msingi ya kuishi ambayo kila mmoja anapaswa kuwa nayo.

Wazee ni dhahabu, wazee ni hazina, badala ya kuwanyanyasa, kuwadhalilisha na kuwaona wasiofaa katika jamii, tuwatumie vyema kwa mambo yenye manufaa, tuwatumie wao kama njia ya wengine kujiandaa na uzee wenye heshima.

rabia.bakari@gmail.com


No comments:

Post a Comment