24 September 2012

Mfumo wa soko huria hautumiki ipasavyo ili kwenda na wakati



USHINDANI katika sekta ya biashara nchini, unaendelea kukua kwa kasi tangu Tanzania ilipotangaza kuingia kwenye mfumo wa soko huria ili kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Mabadiliko makubwa kiuchumi yamefanyika ili kuongeza kasi ya ushindani kibiashara katika sekta mbalimbali.

Ushindani huo umekuwa changamoto muhimu kwa baadhi ya wafanyabiashara waliozoea kufanya shughuli zao kwa ukiritimba kubuni njia mbadala za kukubalika kwenye soko linatoa nafasi kwa wateja au walaji kuamua wapi pa kwenda.

Ni wazi kuwa, wapo waliobadilika kwa kiasi kikubwa chini ya mfumo huu. Kwa mfano, enzi za ukiritimba ilikuwa jambo la kawaida kukuta baadhi ya benki zikifungwa saa sita mchana.

Kufungwa kwa benki hizo, kuliwapa fursa wafanyakazi kwenda kula na kurudi saa nane mchana au zaidi ya hapo.

Benki zingine zilifungwa saa 8:30 au tisa alasiri lakini wateja hawakuwa na mbadala.

Sekta ya benki nchini ni moja ya mifano iliyoonesha mabadiliko makubwa baada ya kuingia katika ushindani. Kila benki imeona umuhimu wa kubuni mbinu mbalimbali ili kuvutia wateja.

Lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha wanatoa huduma bora zinazokidhi mahitaji ya wateja wao kwa wakati. Pamoja na ushindani huo, kuna baadhi ya eneo ambayo wafanyabiashara wamejisahau au hawajapata ushindani wa kutosha.

Eneo hili ni la wafanyabiashara wa kawaida wenye maduka yanayouza bidhaa mbalimbali za majumbani zikiwemo nguo, viatu, vyombo vya chakula, vifaa vya umeme na nyingine.

Inapofika mchana au jioni ni kawaida kwa maduka mengi makubwa kufungwa bila wafanyabiashara husika kutambua kuwa, kufungwa kwa maduka hayo ndio muda muafaka wa wao kufanya biashara.

Wafanyakazi wengi wanapotoka kazini jioni, hutumia muda huo kununua bidhaa mbalimbali. Siku za Jumamosi na Jumapili, maduka mengi yaliyopo katikati ya jiji huwa yanafungwa.

Sisi tunasema kuwa, hilo ni kosa kubwa hivyo tufike wakati, wafanyabiashara wetu wabadili mitanzamo yao kwani bila kufanya hivyo wataanguka. Ni muhimu kwao kuangalia uwezekano wa kufanya biashara hata saa za usiku.

Maeneo muhimu kibiashara kama Kariakoo, jijini Dar es Salaam, yaandaliwe utaratibu wa kuwa na soko la usiku kwani huo ni muda mzuri kwa wateja wengi  kufanya manunuzi baada ya saa za kazi.

Imani yetu ni kwamba, wafanyabiashara watabadilisha mitazamo yao haraka ili kwenda na wakati vinginevyo watazidi kuanguka kibiashara, kumtafuta mchawi na kulalamikia.

No comments:

Post a Comment