06 September 2012
BRELA yaeleza siri ya tuzo yake ya dhahabu.
Na Mwandishi Wetu
BRELA ni taasisi iliyoanzishwa na serikali baada ya mabadiliko mbalimbali ya kiuchumi nchini katika miaka ya 90, serikali ilianzisha wakala mbalimbali kwa lengo la kuboresha huduma zake kwa wananchi.
Kabla ya mabadiilko hayo wakala hizo zilikuwa ni idara za serikali chini wizara mbalimbali Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ikiwa ni Idara moja wapo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa wakala hiyo, Bw.Esteriano Mahingila, anasema, tangu kuanzishwa mwaka 1997 BRELA imejitahidi kufanya kazi kwa bidii ili kuwahudumia wananchi jambo ambalo limesaidia pia kukuza uchumi wa nchi yetu na kujishindia tuzo mbalimbali ikiwamo ya hivi karibuni ya International Arch of Europe Quality Awards.
“Kwa sisi kufahamu kiu ya huduma ya wateja wetu ndiyo siri yetu ya kupigiwa kura nyingi na hatimaye kupewa tuzo ya ubora ya kimataifa katika kundi la utoaji huduma, tuzo iliyotolewa mwishoni mwa mwezi wa Aprili mwaka huu mjini Frankfurt nchini Ujerumani ikijumuisha mataifa sabini na saba Duniani kote,”anasema.
Anasema kuwa kwa kawaida taasisi yake inawahudumia watanzania na wageni na bila wao kufahamu huku watu wa nje wakifuatilia utoaji huduma wa wakala wake na hatimaye kuwapigia kura ya ushindi wa tuzo hiyo ya dhahabu.
Anafafanua kuwa taasisi yake siku zote imekuwa ikijitahidi kufahamu mahitaji ya wateja wake ili kutoa huduma ambazo wateja wake wanazihitaji pamoja na kufahamu matarajio yao.
“Tumekuwa tukijitahidi sana kupata maoni ya wateja wetu na kupitia baadhi ya vyombo vya habari, tumekuwa tukipata maoni ya wateja wetu kwamba wanatuonaje? Na nini matarajio yao kutoka kwetu, kutoka hapo inakuwa ni rahisi kwetu kuwahudumia wateja wetu kulingana na mahitaji yao kutoka kwetu,” anasema.
Siri nyingine ya mafanikio ni kujituma miongoni mwa wafanyakazi wa wakala wake, na kwamba umoja na miongoni mwao kufanya kazi kama timu ni siri nyingine ya mafanikio yao.
Anasema wakala wake pia umefanikiwa kujitegemea kwa asilimia mia moja na kufanya hivyo umetimiza matarajio ya serikali ya kuzibadili baadhi ya taasisi zake kuwa wakala na hatimaye ziweze kujitegemea na kuipunguzia serikali gharama za uendeshaji.
”Kwetu sisi hii ni changamoto, watu wanatutazama sisi, tunachokifanya sasa ni kuongeza juhudi katika kuwahudumia wananchi na hatimaye kuendelea kubaki kileleni miongoni mwa taasisi kama yetu hapa barani Afrika,”.
Anasema, wakala wake umejitahidi kuongeza ubora wa huduma zake kwa wananchi lakini kwa gharama nafuu.
Anasema kiwango cha ada za huduma zake kwa wananchi kimebaki kuwa kidogo kwani lengo lao ni kuwawezesha wananchi na wateja wao kupata huduma kwa gharama nafuu.
“Tunachokifanya sisi ni kuongeza wigo wa huduma zetu ili tuweze kutoa huduma kwa watu wengi zaidi na hatimaye kupata mapato ya kutosha kutuwezesha kujienedesha,” anasema.
Anasema katika hafla hiyo ya Jijini Frankfurt, aliitumia fursa hiyo pia kuwaomba wawekezaji kutoka nchi 77 zilizoshiriki mkutano huo kuja kuwekeza nchini.
Anabainisha kuwa katika mkutano huo, washiriki wengi walikuwa ni kutoka katika sekta binafsi, hivyo hiyo ilikuwa ni fursa nzuri kwa nchi yetu kuweza kujitangaza na kuvutia wawekezaji.
Anasema kwamba Tanzania imekuwa ni mwanachama wa mashirika mengi yanayosimamia haki miliki ya Dunia kama vile World Intellectual Property Organization (WIPO) na lile la African Regional Intellectual Property (RIPO).
Bw.Mahingila ambaye amehusika katika kuibadili wakala wake kutoka Idara ya Msajali wa makampuni hadi kuwa wakala unaojitegemea ni mjumbe wa Baraza la Uongozi la ARIPO kuanzia mwaka 1999 na amekuwa mwenyekiti wa baraza hilo kuanzia mwaka 2003-2005 na kwamba ameipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika ngazi ya kimataifa.
“Sisi kazi yetu kubwa ni kuzalisha na kuilea sekta binafsi nchini kwa maana ya kuwezesha kuanzishwa kwa biashara mbalimbali za ndani,”.
Mbali na kutengeneza ajira anafafanua kuwa wakala wake una shughulikia ulinzi wa hataza chini ya sheria ya hataza sura ya 217.
“Pia tunatoa ulinzi wa teknolojia mpya zinazobuniwa na watu mbalimbali kwa manufaa ya wabunifu hao,” anasema.
Anasema, idadi ya kampuni zinazosajiliwa imekuwa ikiongezeka kila mwaka, kwa mfano mwaka 2006/07 wakala wake ulisajili makampuni 4003, mwaka 2007/08 5234, mwaka 2008/09 makampuni 5357, mwaka 2009/10 makampuni 5278, mwaka 2010/11 7,058 na mwaka 2011 hadi Machi mwaka huu makampuni yaliyosajiliwa ni 5,768.
Kuhusu majina ya biashara yaliyosajiliwa na wakala wake kwa kipindi hicho anasema mwaka 2006/07 ni majina 8808,mwaka 2007/08 majina 9946 yalisajiliwa, mwaka 2008/09 11,708 , mwaka 2009/10 majina 11,127 yalipata usajili, mwaka 2010/11 majina 14,866 yalisajiliwa na mwaka 2011 hadi Machi mwaka huu majina 12,360 yalipata usajili.
“Kwa takwimu hizo utaona ni jinsi kumekuwa na maendeleo kwa maana ya ongezeko la watu wanaofanya biashara mbalimbali ama shughuli mbalimbali,” anasema.
Bw.Mahingila anatoa wito kwa wajasiriamali kuziwekea alama bidhaa zao ili ziweze kutambulika na hivyo kushindana katika soko la kimataifa.
“Hivi sasa tumeingia kwenye soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki, inawapasa wafanyabiashara wetu kuziwekea alama bidhaa zao ili ziweze kutambulika na hivyo kuweza kushindana,”.
Anawapongeza wabunifu mbalimbali wa kitanzania kwa kubuni bidhaa na huduma mbalimbali ambazo zimeweza kutengeneza ajira kwa Watanzania wengi.
“Tunasisitiza matumizi ya mtandao kwani kwa kufanya hivyo wateja wetu watapata huduma zetu kwa urahisi na bila usumbufu wowote,” anasema.
Kuhusu mafanikio mbalimbali ya wakala wake anasema kwamba huduma zimeboreshwa zaidi na kwamba wateja wanaweza kupata hati ya usajili wa kampuni ndani ya siku tano tofauti na hapo awali ambapo siku zilikuwa zaidi ya hapo.
“Kwakweli huduma zetu zimeboreka sana, kutokana na kuamua kwenda na wakati kwa kuwahudumia watanzania kwa uharaka na ubora zaidi," anasema.
Anasema ni matazamio ya serikali kuona kwamba watanzania wanapata huduma bora, zenye kiwango bora na kwa haraka ili waweze kutimiza matarajio yao kwa muda muafaka.
Anabainisha kwamba wakala wake utaendelea kutoa huduma bora kwa wateja wake ili kuhakikisha kwamba uchumi unakua kwa haraka zaidi kutokana na wananchi wengi kujihusisha na shughuli mbalimbali za uzalishaji mali.
“Kwa kweli hayo pia ni mafanikio, fomu zetu zote ziko kwenye mtandao, hili ni jambo la kujivunia kwani kwa kufanya hivyo tumewawezesha wateja wetu kupata huduma zetu kokote waliko bila kuwalazimu kuja kuchukua fomu hapa ofisini kwetu,”
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment