08 June 2012
Yondani azichonganisha Simba, yanga *Simba yatishia kushitaki FIFA
Na Elizabeth Mayemba
SAKATA la mchezaji Kelvin Yondan limezidi kuchukua sura mpya, baada ya Klabu ya Simba kujibu mapigo na kuonesha mkataba waliomuongezea mchezaji huyo, huku wakidai huo uliooneshwa na watani zao Yanga ni feki.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Aden Rage alisema Yondan ni mchezaji halali wa Simba kwa kuwa mwaka jana aliongeza mkataba wa kuichezea timu hiyo miaka miwili.
"Mkataba ambao Yanga wameuonesha katika vyombo vya habari naufananisha kama karatasi la chooni (toilet paper), sisi ndio tuna mkataba halali wa mchezaji huyo ambaye aliusaini akiwa chini ya mwanasheria Alan Maduhu na pia TFF (Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania) wanautambua," alisema.
Alisema atawashitaki Yanga, Shirikisho la la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), kwa kitendo chao cha kumsajili Yondan wakati bado ana makataba na klabu yake.
Mwenyekiti huyo alisema viongozi wa Yanga wamekuwa wakichanganya mara nyingi katika mambo ya soka kwani Ofisa Habari wa klabu hiyo juzi alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akidai kuwa walimsajili Yondani Novemba mwaka jana huku picha ikionesha amesaini juzi.
Rage alisema ushahidi wa picha katika mitandao unaonesha Yondan alisainishwa juzi usiku, kwani picha aliyopiga akiwa Ahmed Seif wakati akisaini inaonesha amevaa fulana ya timu ya soka ya Taifa ya Tanzania, (Taifa Stars) yenye nembo ya wadhamini wapya bia ya Kilimanjaro, ambao waliingia mkataba wa kuidhamini timu hiyo mwezi uliopita.
"Kwanza kuna picha ambayo inaonesha Yondani akiwa katika jezi ya mazoezi ya timu ya Taifa yenye nembo ya bia ya Kilimanjaro na kumbukumbu zinaonesha mkataba kati ya TBL na TFF ni Juni 9 mwaka huu, hivyo kwa haraka haraka tukio hilo limefanyika kipindi cha chini ya mwezi mmoja ingawa taarifa za ushahidi zinaonesha tukio hilo lilitokea jana (juzi)," alisema.
Alisema kitendo walichofanya Yanga si cha kistaarabu kwani kinautia aibu mchezo wa soka, hivyo jana aliwaagiza mawakili wa klabu hiyo kukaa na kuandaa mashitaka ya kupeleka FIFA.
Rage pia alionesha nakala ya mkataba ambao Simba ilisaini na Yondani Desemba mwaka jana, ikionesha amepata fedha taslimu sh. milioni 25 kwa miaka miwili.
Alisema Yondani ni mchezaji halali wa Simba aliye na mkataba hadi Mei 31, mwaka 2014, baada ya kuongeza mkataba na klabu yake, Desemba 23, mwaka jana kwani mkataba wa awali wa mchezaji huyo na Simba uliisha Mei 31, mwaka huu.
"Sheria za FIFA za hadhi na uhamisho wa wachezaji ziko wazi, katika kipengele cha 5 kifungu kidogo cha 2 kinasema kwamba mchezaji atasajiliwa kuichezea timu moja tu kwa wakati mmoja," alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment