08 June 2012
Nagu awageuzia kibao watendaji
Na Stephano Samo, Manyara
VIONGOZI wa serikali za mitaa na halmashauri ya wilaya wametajwa
kuwa ni chanzo cha migogoro inayotokea ndani ya jamii hapa nchini.
Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hanang mkoani Manyara Bi. Mary Nagu kwenye majumuisho ya ziara yake ya siku saba mjini hapa alipokuwa akizungumza na watendaji mbalimbali.
Bi. Nagu alisema, ni changamoto kwa watendaji wa vijiji na kata na
watendaji wa halmashauri kutowajipika ipasavyo katika kuwahudumia
wananchi badala yake wao ndiyo wamekuwa chanzo cha migogoro
wilayani hapo kwani hawatatui matatizo ya wananchi hivyo wanapaswa kubadili mwelekeo.
Mbunge huyo alisema kuwa, matatizo ya wananchi pindi yanapoachwa kutatuliwa kwa muda mrefu yanajenga usugu ambao ni kero ya kudumu.
Pia aliwaasa watendaji hao kuwa, ni lazima waache kukaa ofisini
badala yake wawe na desturi ya kuwatembelea wananchi kwenye makazi yao
kwani kwa kufanya hivyo wataweza kubaini matatizo ya wananchi haraka
na kuzitatua kero zinazowakabili haraka.
Akizungumzia migogoro ya wavamizi katika ardhi inayoendelea mjini hapa alisema, hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa ili kudhibiti hali hiyo.
Naye Mkuu wa wilaya hiyo Bi. Cristina Mdeme akizungumzia taharuki
zilizojitokeza kwenye mgogoro wa uvamizi wa Mto Nyamuri baada ya
wananchi zaidi ya 2,000 kufyeka miwa na migomba ya ndizi ya Bw.Sulemani
amewataka wananchi hao kuacha hasira kwani serikali itachukua hatua
haraka kutatua mgogoro huo.
Bi. Mdeme aliongeza kuwa ni marufuku kwa mtu yoyote kulima au kufanya
shughuli yoyote kwenye vyanzo vya maji na si hapa Nyamuri bali maeneo yote ya wilayani na nchi nzima kwani maji ni uhai wa watu na viumbe vyote
hai.
Akizungumzia Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi pamoja na Katiba Mpya
ya Tanzania Bi. Mdeme aliwataka wananchi wote hapa nchini washiriki kikamilifu kwenye kutoa maoni yao kwenye tume iliyoundwa sambamba na ushiriki wa sensa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment