23 January 2012

Ruvuma yapaa kilimo cha mahindi, kahawa

Na Mwandishi Wetu

SEHEMU kubwa ya maisha ya Watanzania hutegemea kilimo, kwa kutambua hivyo
Mwalimu Julius Nyerere aliita ‘Kilimo Uti wa Mgongo.’
Pamoja na kauli hiyo, bado kuna kauli mbalimbali zilizoasisiwa na Mwalimu Nyerere pia viongozi wengine wa kitaifa kama ‘Kilimo cha Kufa na Kupona,’ ‘Kilimo cha Kijani’ ikiwa ni njia ya kuwatia moyo wakulima pamoja na kuongeza ufanisi wake kwa kutambua kwamba, kuyumba kwa kilimo ndio kuyumba kwa uchumi wa taifa.
Kwa kufanya hivyo, serikali kila mwaka hufanya juhudi kuhakikisha kuwa, wakulima nchini wanaboreshewa mazingira ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa, wanapata mavuno yanyoweza kuwanufaisha pamoja na kuongeza pato la Taifa.
Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa inayoitikia wito katika kuhakikisha kuwa, kila mwaka matokeo ya mavuno yanakuwa yenye mafanikio kulinganisha na mwaka uliopita.
Juhudi za Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Bi. Christine Ishengoma pamoja sekretarieti yake wamekuwa katika mikakati ya kuhakikisha kuwa, kilimo kinakuwa kimbilio la wana Ruvuma wengi kwa kuweka mikakati mbalimbali.
Mikakati hiyo imeonesha mafanikio kutokana na wakulima kunufaika na kilimo chao kwa kuweza kupata mafanikio na kuhimili vishindo vya maisha yao.
Mipango ya utekelezaji wa malengo ya kilimo yalianza kushika kasi katika msimu wa 2009/10 ambapo wakati huo Mkoa wa Ruvuma ulilenga kulima hekta 503,388 za mazao ya chakula na biashara zilizotarajiwa kutoa mazao ya tani 1,020,475.
Katika mazao hayo, mazao ya chakula yalikuwa hekta 393,323 yaliyotarajiwa kutoa tani 63,770. Kutokana na juhudi za Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kufikia Juni mwaka jana hekta 501,220 sawa na silimia 99 ya malengo zililimwa na kutoa mavuno ya tani 1,127,589 sawa na zaidi ya asilimia 10 ya malengo.
Katika juhudi hizo kwa mwaka huo, mazao ya chakula yalilimwa hekta 417,314 yaliyotoa mavuno ya tani 1,065,015 na mazao ya biashara hekta 83,906 na kutoa mavuno ya tani 40,983.
Juhudi za kuongeza uzalishaji katika kilimo zinazofanywa na Bi. Ishengoma pamoja na watendaji wake zinalenga kuhakikisha kwamba, hekta  555,072 za mazao ya chakula na biashara kwa mwaka 2010/11 zinalimwa na kuwa na matarajio ya kutoa tani 1,149,164.
Katika upande wa mazao ya biashara mkoa ulijiwekea malengo ya kulima hekta 105,807 kwa matarajio ya kupata mavuno kiasi tani 107,882. Eneo lililowekewa malengo kulimwa ni ongezeko la asilimia 10.3 zaidi ya awali.
Kutokana na kujali wakulima, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwa mwaka 2010/11 iliomba ruzuku ya pembejeo ya kutosheleza wakulima 300,000 sawa na tani 55,000, pamoja na juhudi hizo Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika imetenga vocha kwa wakulima 203,412 sawa na asilimia 68.7 ya maombi ya mkoa.
Pia, kutokana na utafiti uliofanywa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa msimu 2010/11 ulibaini kuwa, mkoa wote unahitaji jumla ya tani 57,000 za pembejeo.
Mchanganuo huo unaonesha kuwa, Halmashauri ya Wilaya ya Songea inahitaji pembejeo tani 19,550, Manispaa ya Songe inahitaji tani 2,300, Wilaya ya Mbinga inahitaji tani 15,525, Wilaya ya Namtumbo inahitaji tani 15,525 na pia Wilaya ya Tunduru inahitaji tani 4,600.     
Pamoja na kilimo kushika hatamu mkoani humo, kumekuwa na juhudi za dhati katika kuhakikisha Vyama vya Ushirika vinashiriki katika kuhakikisha maisha ya wananchi yanasonga mbele.
Mkoa wa Ruvuma una Vyama vya Ushirika ambavyo vinasaidia katika kukombo amaisha ya wana Ruvuma.
Pamoja na hivyo, kama ilivyo katika sekta zingine, katika sekta ya vyama vya ushirika nako changamoto ni nyingi ambapo wakati mwingine husababisha kutofikiwa malengo.
Changamoto kubwa katika sekta hiyo ni pamoja na kutokuwepo kwa masoko ya kuaminika kwa ununuzi wa mazao ya wakulima, upungufu wa watumishi wa fani ya ushirika katika halmashauri.
Uhaba wa mitaji katika vyama vya ushirika ni miongoni mwa mambo ambayo yanasababisha kuzorota kwa sekta hiyo, pia elimu ya ushirika bado ni ndogo kwa wanaushirika pamoja na wadau wa ushirika.
Kwa kuwa ushirika ni moja ya nyenzo muhimu katika kufikia mafanikio, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma imeweka mikakati ili kukabiliana na hali hiyo.
Miongoni mwayo ni pamoja na kuimarisha mfumo wa stakabadhi ghalani ili kuimarisha masoko ya wakulima, kuajiri watumishi wapya na kuwaendeleza wale waliokuwepo, kuimarisha vyama vilivyopo ili kujenga mitaji na taasisi za fedha kama mabenki pamoja na kuendeleza kutoa elimu ya elimu ya ushirika kwa wanaushirika na wadau.
Hali ya bishara kwa upande wa mazao ya kilimo kwa Mkoa wa Ruvuma bado inaridhisha kutokana na ubora na wingi wa mavuno kwa wakulima.
Pamoja na kuwepo kwa hali nzuri ya mavuno Ofisi ya Mkuu wa Mkoa inatoa angalizo kwa bidhaa zinazotoka viwandani kuwa, zinapanda kiholela na hivyo kusababoisha maisha magumu kwa wananchi.
Kwa kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa inahusika moja kwa moja katika kuhakikisha maisha ya wananchi yanakuwa ya faraja, ofisi hiyo imeweka utaratika katika kukabiliana na kupanda holela kwa bei za bidhaa.
Mikakati hiyo ni pamoja na kutoa elimu kwa wadau wote juu ya soko huria, kuendelea kukaa na wafanyabiashara ili kujali athari za upamndaji holeala kwa bidhaa na kuona uwezekano wa kuunda umoja wa walaji kwa lengo la kudhibiti upandaji holela wa bei.
Hatua nyingine ni kudhibiti uuzaji wa bidhaa bandia, uuzaji wa bidhaa zenye viwango dhaifu pia kutotumia vipimo sahihi na vifungashio sahihi.
Kwa kujua umuhimu wa kuaznisha usindiakji wa kahawa, Mkoa wa Ruvuma kwa sasa una jumla ya viwanda vitatu vya usindikaji kahawa katika Wilaya ya Mbinga.
Viwanda hivyo vinamilikiwa Kampuni za DAE Ltd, Mbinga Coffee Curing Company na LIMA Ltd ambapo kuna kiwanda kimoja cha kubangua korosho wilayani Tunduru kinachomilikiwa na Afrika Ltd.
Katika kipindi cha Mwezi Mei 2010-Oktoba 2010 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa imeweza kutoa leseni 925 za bishara za aina mbalimbali, utoaji wa leseni za vileo zimefikia 536 hadi Oktoba mwaka jana.
Juhudi zinazofanywa na Ofisi ya Mkuu wa MKoa wa Ruvuma ni kuhakikisha kuwa, lengo lililokusuduwa na serikali katika kuhakikisha kuwa wananchi wanaondokana na umasikini wa kipato.
Katika kuhakikisha hilo, ofisi imekuwa ikishawishi wananchi kuingia katika biashara kwa kuwa, kufanya hivyo kunawakomboa wananchi ikiwa ni pamoja na kuiingizia serikali mapato.
Kwa mfano, mwaka 2010 MKoa wa Ruvuma kupitia nyumba za kulala wageni umeweza kukusanya ushuru kiasi cha sh. 19,280,910, pia ukaguzi wa leseni za biashara ulifanyika na kuiingizia mkoa sh. 1,792,600 kutokana na vyanzo mbalimbali ikiwemo wafanyabiashara wasiokuwa na leseni, ada za matangazo pamoja na ushuru wa soko.
Wananchi wa Ruvuma wametakiwa kuchangamkia kilimo pamoja na biashara ili kuhakikisha wanabadili maisha yao ikiwa ni pamoja na kuondoa njaa nchini.

No comments:

Post a Comment