23 January 2012

Jk,Tibaijuka watendaji hawa mnawaona?

Na Gladness Mboma

SERIKALI imekuwa ikipiga kelele kuhusu ujenzi holela hasa jijini Dar es Salaam,
ambapo watu wamekuwa wakijenga barabarabi na mabondeni bila kujali kwamba, kufanya hivyo ni kinyume na sheria za ardhi.
Watu wengine wamekuwa wakijenga hata katika maeneo yasiyohusika bila kujali kwamba, wanakwenda kinyume na mipango miji husika.
Siyo tu kuvunja sheria za ardhi, pia ni hatari kwa maisha yao, lakini ujenzi holela umekuwa kama tatizo sugu maeneo mengi nchini hususan Dar es Salaam.
Ninaandika makala haya kutokana na hali halisi ambayo kwa kiasi kikubwa inasababishwa na watendaji wetu wa chini nikimanisha viongozi wa Serikali za Mitaa.
Mara nyingi nimekuwa nikimweleza Rais Jakaya kikwete kupitia chambuzi zangu mbalimbali kwamba, wanaomuangusha katika utendaji ni watendaji wake wa chini na wala siyo vinginevyo.
Ujenzi holela kwa kiasi kikubwa umesababishwa na watendaji wetu nikimaanisha viongozi wa Serikali za Mitaa ambao wamewekwa karibu na wananchi kwa ajili ya kusimamia miundombinu mpangilio wa miji na mambo mengine katika maeneo wanayoishi wananchi.
Cha kusikitisha viongozi hao wamekuwa ni mstari wa mbele kuruhusu wananchi kujenga hovyo katika maeneo ambayo hayatakiwa ikiwemo barabarani kwa madai kwamba, maeneo hayo yana wenyewe.
Ninazungumza hivi kwa sababu nimeshuhudia tukio moja la mtu kujenga barabarani tena kwa kushawishiwa na watu wasiopenda maendeleo kwa madai tu ya kuwakomoa watu.
Ninachopenda kusema ni kwamba, mwananchi unapojenga barabarani hawawakomoi wananchi wenzako bali unaikomoa serikali.
Mtu kujenga nyumba bila kujali sehemu ya dharura hasa usafiri, ni kushindwa kufikiri.
Jamani, katika suala hili la barabara ni lazima tuwe makini tusikurupuke kujenga njiani eti kwa ajili ya kuwakomoa watu fulani wenye magari, tunaelekea wapi Watanzania?
Wiki hii kuna tukio moja la ajabu lilitokea katika maeneo ya Kimara Mavurunza, ambapo mwananchi mmoja alijenga njiani kwa madai kuwa ni eneo lake.
Wapenda maendeleo na wakazi ambao waliona ujenzi huo si sawa walilazimika kutoa taarifa kwa mjumbe husika, lakini cha kusikitisha na kushangaza mjumbe huyo alipokwenda katika eneo husika na kusema kuwa, ujenzi huo ni halali kwa sababu ni lake ila alichelewa kujenga, kweli huu ndio uongozi?
Viongozi wa stahili hii wanaokubaliana na vitu ambavyo vinazorotesha maendeleo ya serikali hawastahili kamwe katika jamii na wanatakiwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Rais Kikwete na Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Bi. Anna Tibaijuka naamini wanatambua jinsi watendaji wao wanavyowaangusha? kutokana na ujenzi holela kuendelea katika maeneo mbalimbali kutokana na watendaji wasiojua sheria za ardhi kuruhusu hali hiyo bila kuwa na chembe ya huruma kwa serikali yao.
Kutokana na hali hiyo, suala hilo lilipelekwa ngazi ya juu, Serikali za Mitaa nao, ambapo walifika eneo la tukio na kuonesha waziwazi kumtetea mtuhumiwa bila kuwa na vigezo vyovyote.
Kwa kiongozi yoyote mpenda maendeleo na anayezijua vyema sheria za ardhi na anayesikia jinsi serikali inavyopiga kelele juu ya mipango miji asingetaka kusikia hoja yoyote na badala yake angeamuru jengo hilo livunjwe.
Kama wananchi wenyewe wanashangzwa na hali ya ujenzi huo na kisha viongozi wanaona kawaida, hiyo ni kuwakatisha tamaa Watanzania.
Cha kusikitisha ni kwamba, mnunuaji wa kiwanja hicho aliponunua kiwanja hicho aliona kabisa mpangilio wa mipango miji unakoelekea, lakini kwa jeuri  aliamua kununua.
Lawama zangu zote ninawatupiwa watendaji wa serikali za mitaa mbao sasa wamekuwa ndio vyanzo vya kukubaliana na hali hiyo, hali inayosababisha mipango miji kuwa shagalabagala.
Serikali hususan wizara husika mnatakiwa kuwa macho na watendaji wenu, kwani wamekuwa ndio chanzo cha ujenzi holela wenyewe wakiongoza kwa kuuza maeneo ambayo yametengwa na serikali kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Suala hili lisipofuatiliwa na wananchi kuwa macho na watendaji hawa wabovu hakika mipango miji itageuka kuwa uchochoro.
Kila siku kunakuwepo na itilafu za umeme watu wanajenga barabarani, hilo gari la zimamoto litapitia wapi, achilia hali hiyo, wagonjwa watapitishiwa wapi kama njia zenyewe sasa zinajengwa na kubakizwa uchochoro.

Hivi watendaji nikimaanisha wajumbe wa nyumba kumi, na Serikali za Mitaa mnajua wajibu wa kazi zenu au mnakaa maofisi na kusubiria kuletewa taarifa za ugawaji wa viwanja.
Sasa basi kama mlikuwa hamjui kazi zenu leo ninawaeleza kwamba mnatakiwa kutembelea maeneo yenu kila siku na kuangalia miuondo mbinu na mipango miji inavyokwenda na kuwasimamia wananchi na siyo kukaa maofisi ili mfuatwe.
Kimara ni mji ambao kwa sasa umekuwa kwa kasi na umegeuka kichaka kwa sasa, kutokana na watendaji waliopewa thamana ya kuusimamia kutofanya hivyo na badala yake wananchi wanajenga wanavyotaka.
Serikali inatakiwa kuwa macho na watendaji hawa ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakididimiza jitihada za serikali na hivyo kuonekana haifanyi kazi.

No comments:

Post a Comment